Dar/Moshi. Wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani zikiingia siku ya tisa leo Septemba 5, baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali na wapambe wao wanatumia lugha za makabila pasipokuwa na wakalimani.
Baadhi ya maeneo ambayo matumizi ya lugha za makabila yanaonekana kushamiri pasipo uwepo wa mtafsiri wa lugha ni mikoa ya Kanda ya Ziwa wanatumia lugha ya Kisukuma na Kanda ya Kaskazini mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Hata hivyo, matumizi ya lugha za makabila majukwaani katika uchaguzi huo katika baadhi ya maeneo, kumewaibua wasomi wakiwamo walimu ambao wamepinga suala hilo wakisema linakiuka kanuni za uchaguzi na linapalilia ukabila.
Katika Mkoa wa Kilimanjaro, baadhi ya wagombea na wapambe wao hutumia lugha ya kichaga kwa maeneo ya uchagani na Kipare kwa maeneo ya upareni, huku Manyara na Arusha wakitumia lugha ya Kimeru, Kimasai na Kibarbaig.
Matumizi hayo ya lugha za makabila bila uwepo wa mtafsiri, kunakiuka Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na Madiwani za mwaka 2025 ambazo zimetengenezwa chini ya kifungu cha 162 cha sheria ya uchaguzi ya 2024.
Kifungu cha 2.1(n) cha kanuni hizo zimechapwa katika gazeti la Serikali (GN) namba 249 la Aprili 18,2025 kinataka lugha ya Kiswahili ndio itumike katika kampeni, isipokuwa tu kama lugha hiyo itakuwa haieleweki, itatafsiriwa.
Kulingana na kifungu hicho, kinasema:- “Kuhakikisha kuwa, lugha ya Kiswahili itakuwa ndio lugha itakayotumika katika kampeni za uchaguzi. Iwapo lugha hiyo haieleweki, na itakapolazimu, mgombea atazungumza katika lugha ya Kiswahili na mkalimani atatafsiri katika lugha inayoeleweka kwa jamii husika.”
Kanuni hizo zilisainiwa Aprili 12, 2025 na Jaji Jacob Mwambelege kwa niaba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Dk Jim Yonazi ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbali na wadau hao, lakini kanuni hizo zilisainiwa na makatibu wakuu wa vyama vya siasa 18 vinavyoshiriki uchaguzi huo, isipokuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kimeweka msimamo wa kutoshiriki bila kuwapo kwa mabadiliko ya sheria na mifumo ya uchaguzi.
Hata hivyo, pamoja na takwa hilo la kisheria, baadhi ya wagombea ubunge na udiwani na wapambe wao katika mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa, wanadaiwa kuzungumza kwa lugha za makabila yao pasipokuwepo mkalimani.
Baadhi ya video zilizosambaa mitandaoni hususan katika makundi Songozi (Whatsapp), yanaonyesha baadhi ya wagombea na wapambe wakiongea kilugha majukwaani, bila uwepo wa mkalimani kwa lengo la kutafsiri kinachosemwa.
“Hiyo kanuni ukiisoma vizuri inataka huyo mgombea yeye aongee Kiswahili halafu ndio awepo mkalimani wa kutafsiri kwenda Kimasai, Kisukuma, Kipare na lugha zingine. Lakini kinachofanyika ni tofauti kabisa,”alisema wakili Peter Mshikilwa.
“Hata ukienda leo uchagani, upareni au hata usukumani, sio wote wanaoishi huko wanatoka katika makabila hayo. Kuna wafanyakazi wapo pale kikazi na wana haki ya kupiga kura. Unapoongea kilugha hawezi kuelewa sera zako,”amesema.
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele amesema suala hilo limewekwa wazi katika Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025.
Amerejea matakwa ya kanuni hiyo 2.1(n) inayosema mgombea au chama cha siasa kinapaswa; “Kuhakikisha kuwa, lugha ya Kiswahili itakuwa ndio lugha itakayotumika katika kampeni za uchaguzi. Iwapo lugha hiyo haieleweki, na itakapolazimu, mgombea atazungumza katika lugha ya Kiswahili na mkalimani atatafsiri katika lugha inayoeleweka kwa jamii husika.”
Akifafanua zaidi Jaji Mwambegele amesema; “Ni kosa, lakini hata mgombea mwenyewe afikirie sasa kwamba anaweza kuongea kwa lugha isiyoeleweka na wote, anakuwa hajafikisha ujumbe kwa baadhi ya watu na hasara inakuwa kwake.”
Akizungumzia suala la baadhi ya wagombea kuzungumza kilugha majukwani, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk George Kahangwa amesema kwa sababu Tanzania ina mchangamano wa watu mbalimbali
Akizungumza na gazeti hili, amesema Tanzania ya sasa inaendelea kuchangamana na umefika wakati jimbo moja lina watu zaidi ya wale wenye asili ya eneo husika.
Kutumia lugha, Dk Kahangwa amesema maana yake kuna watu hawatasikia ujumbe unaotolewa, hivyo Kiswahili ni lugha sahihi zaidi kutumika.
“Sasa hivi ukienda mkoa wowote utawakuta wamasai na mashuka yao, sasa ukitumia lugha mama hawatakuelewa,” amesema mwanazuoni huyo.
Amesema hata wagombea kwa sasa haizingatiwi mtu wa asili fulani akagombee kwenye eneo lake la asili, hivyo itakuwa vigumu wao kujua lugha ya asili ya eneo husika,”alisisitiza mchambuzi huyo wa siasa na msomi na kuongeza;-
“Tanzania ambayo tunaendelea kumuomba Mungu adumishe uhuru, umoja na mshikamano, moja ya vitu vilivyotupa mambo hayo, ni lugha ya Kiswahili.”
Hata hivyo, Dk Kahangwa ameeleza kufanya hivyo ni kuendekeza ukabila.
Mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa, Dk Avith Mushi alisema kutumia lugha ya asili kuzungumza na wananchi wenye asili ya lugha husika ni jambo zuri na linaongeza uelewa wa sekta na kufikisha ujumbe kwa walengwa.
“Kucharaza kilugha ni kitu kizuri na mimi naliona jambo zuri. Kwa kuwa ni mbunge na anasikilizwa na watu anaowawakilisha, sio vibaya akizungumza nao kwa lugha wanayoielewa zaidi,” amesema Dk Mushi akizungumza na gazeti hili.
Kwa mujibu wa Dk Mushi, hilo litakuza utamaduni na kwamba watu watazidi kuheshimu lugha, wengine wasiohusika watafuatilia na kwamba inakuwa na faida kwa mgombea na haitakuwa na athari kwa kuwa wanaelewana vema.
“Tanzania hii nilichojifunza, Kiswahili kinajulikana zaidi mijini, lakini vijijini huko kuna watu Kiswahili kinawasumbua sana,” amesema Dk Mushi.
Baadhi ya walimu waliohojiwa na gazeti hili leo Septemba 4,2025, walipinga matumizi ya lugha za makabila majukwaani pasipokuwepo wakalimani, wakisema ni ukiukwaji wa kanuni na kuwabagua wapiga kura wasio na asili ya makabila hayo.
Akitoa maoni yake, Mwalimu Wilfred Mauki wa Shule ya Sekondari ya Mawenzi mjini Moshi, alisema suala la matumizi ya kilugha katika majukwaa ni changamoto kwani sio Watanzania wote wanajua lugha hizo na inahamasisha zaidi ukabila.
“Hii ina speedup (inaongeza kasi) ya ukabila. Anaongea hivyo ili waone huyu ni mwenzetu lakini sifa mojawapo ya kugombea urais, ubunge na udiwani ni kujua kuongea lugha ya Kiswahili au Kiingereza, sio lugha ya kabila lako,”amesema.
Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Stephen Mnguto, amesema matumizi ya lugha nje ya Kiswahili katika majukwaa ya kampeni za uchaguzi mkuu sio sahihi kwa kuwa sio lugha ya Taifa.
“Sio sahihi kabisa mgombea kuongea kilugha kinyume kabisa na kanuni na pengine wanaofanya hivyo hawajasoma kanuni na kuzielewa. Lugha tuliyokubaliana kama taifa ni Kiswahili. Hatutafuti kiongozi wa kabila,”amesema.
“Ukifuatilia sana baadhi ya wanaongea kilugha ni kutaka kuwaonyesha wapiga kura kuwa hata sisi ni watu wa hapa lakini ukifuatilia sana wanaishi zaidi mjini. Wanatumia kilugha kuwashawishi kuwa wao si wa kuja,”amesisitza Mnguto.
Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi), Juma Issihaka na Bakari Kiango (Dar)