ALIYEKUWA kinara wa mabao wa Kagera Sugar msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara, Peter Lwasa amejiunga na kikosi cha Pamba Jiji ya Mwanza kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji ambalo lilionekana kuwa butu.
Lwasa raia wa Uganda alimaliza msimu uliopita akiwa na mabaio manane akishika nafasi ya 11 katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Bara, Charles Ahoua wa Simba akiwa kinara na mabao 16 na ujio wake Pamba umemfanya aungane nyota mwenzake kutoka Uganda, John Nakibinge aliyejiunga na timu hiyo msimu uliopita.
Lwasa alitambulishwa na timu hiyo juzi Jumanne katika mitandao ya kijamii ya timu hiyo sambamba na beki, Hemed Chambela.
Akizungumzia usajili huo katika mazungumzo na kampuni ya uzalishaji bidhaa mbalimbali kutoka nchini Uganda, juzi jijini hapa, Mlezi wa Pamba Jiji, Said Mtanda alisema mchezaji huyo anakuja kuongeza ubora kwenye kikosi hicho.
Mtanda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza alisema mikakati ya Pamba haitaishia kwa nyota hao wawili, Peter Lwasa na John Nakibinge, kwani wamedhamiria kuleta nyota wanaocheza timu ya taifa ya nchi hiyo huku akimtaja Allan Okello (kwa utani)
“Sisi na Uganda tumekuwa karibu na tayari tuna wachezaji wawili kutoka Uganda kwenye timu yetu, tumemsajili Peter Lwasa na yupo John Nakibinge,” alisema Mtanda na kuongeza;
“Sisi Pamba Jiji tutaendelea kuleta wachezaji kutoka Uganda na tunataka tulete wachezaji wa timu ya taifa ya Uganda kwenye kikosi chetu ili kuongeza ushindani, hata Allan Okelo tutamleta (huku akicheka).”
Lwasa ni nyota wa 11 kusajiliwa na Pamba msimu huu, wengine ni Henry Lutonja, Shaphan Siwa, Arijifu Ali, Hassan Kibailo, Abdallah Hamis, Amos Kadikilo, Abdallah Iddi, Brian Eshanda, Abdulmajid Mangalo, Denis Richard na Hemed Chambela.
Ofisa Habari wa Pamba Jiji, Moses William amesema; “Sasahivi kwenye idara yetu ya ushambuliaji tuko kamili tunaye Tegis Momanyi, Abddallah Iddi na Peter Lwasa kwahiyo hatuna hofu kabisa juu ya mabao, mashabiki wasubirie tu ligi ianze.”