Mkongwe agusia bato jipya Simba

UWEPO wa Moussa Camara kama kipa namba moja ndani ya Simba unaelezwa ni changamoto kubwa anayokwenda kukabiliana nayo, kipa mpya wa kikosi hicho, Yakoub Suleiman aliyetua hivi karibuni akitokea kwa maafande wa JKT Tanzania.

Yakoub ambaye ni kipa namba moja wa timu ya taifa, Taifa Stars kwa sasa, ametua Msimbazi sambamba na beki wa kati, Wilson Nangu waliyekuwa wakicheza wote JKT Tanzania na sasa bado hawajajiunga na Wekundu hao kwa vile wana jukumu la kucheza mechi mbili wakiwa na Stars.

Hata hivyo, Yakoub ambaye ni usajili mpya ndani ya Simba eneo la langoni baada ya kuondoka Aishi Manula, amepewa maujanja ya kufanya ili kuendeleza ubora aliouonyesha msimu uliopita alipokuwa katika kikosi cha maafande.

Kipa mkongwe ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa, Peter Manyika Sr, ndiye aliyeyasema hayo alipozungumza na Mwanaspoti, ambapo alisema anaona Yakoub bado ana nafasi ya kuonyesha ubora mbele ya Camara.

Manyika aliyewahi kuidakia Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars  na pia kupita katika klabu za Sigara na Mtibwa Sugar, alisema ili Yakoub asipite njia za makipa wengine wazawa wanaowekwa benchi na wageni, kwanza akubali uwezo wa anayemkuta, kisha aitumie fursa hiyo kujiongeza.

“Ushauri wangu kwake anakwenda Simba sehemu ambayo kuna mtu tayari ni namba moja, hivyo lazima aanzie pembeni,” alisema Manyika ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa wa Namungo baada ya msimu uliopita kuitumikia Dodoma Jiji.

“Unajua ukikaa pale benchini kama huna kocha ambaye anaweza kukontroo kiwango ulichokuwa nacho awali, inakuwa ngumu kuendelea kuwa bora, lazima ushuke.

“Ukweli ni kwamba timu kubwa kama zile zinakuwa na mashabiki wengi, unapokuwa pale unafuatiliwa sana tofauti na sehemu nyingine, unapokuwa katika timu ndogo unacheza mara kwa mara na makosa unayoyafanya yanavumilika, kuliko makosa ukiyafanya unapokuwa timu kubwa.

“Aitumie nafasi hiyo ya kukaa nje kumsoma mwenzake, hakuna kipa ambaye hana makosa, hivyo udhaifu wa mwenzako unatakiwa kuutumia kama fursa kwako,” alisema Manyika.

Ndani ya Simba, Camara amefanikiwa kuwa kipa namba moja tangu atue hapo msimu uliopita 2024-25, huku akifanikiwa kumaliza na clean-sheet 19 zikiwa ni nyingi zaidi ya makipa wengine katika Ligi Kuu Bara, lakini akiiwezesha Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Wakati Camara raia wa Mali anacheza mechi 28 za ligi kati ya 30, wazawa Aishi Manula, Ally Salim na Hussein Abel walikuwa benchini.

Hata hivyo, Manula alikutana na wakati mgumu zaidi kwani alianza kupoteza nafasi tangu msimu wa 2023-2024 alipotua Ayoub Lakred, na mwisho wa msimu wa 2024-2025 mkataba wake ulipomalizika akatua Azam. Kabla ya kutua Simba, Camara alitwaa tuzo mbili za CIS ya Guinea akiwa kama Kipa Bora wa Afrika Magharibi na pia Kipa Bora wa Guinea.

Kwa ujumla, misimu ya hivi karibuni makipa wazawa wamekuwa hawana nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza katika timu nne bora za juu kwenye ligi ambazo ni Yanga, Simba, Azam na Singida Black Stars.

Ndani ya Yanga, Djigui Diarra raia wa Mali anawaweka benchi Aboutwalib Mshery na Khomeiny Abubakar.

Msimu uliopita Azam iliyomaliza ligi katika nafasi ya tatu, Mustafa Mohamed wa Sudan kabla ya msimu huu 2025-2026 kujiunga na Al Hilal, alimuweka benchi mzawa Zuberi Foba. Safari hii Manula ana kazi ya kukaa langoni mbele ya Muivory Coast, Issa Fofana.

Kwa upande wa Singida Black Stars, tangu ujio wa Amas Obasogie, raia wa Nigeria aliyetua wakati wa dirisha dogo msimu uliopita amewaweka benchi wazawa Hussein Masalanga na Metacha Mnata.