MO Dewji Ajiondoa Uenyekiti Simba, Amteua Crescentius Magori – Global Publishers



Mwaka mmoja tangu kuteuliwa kuongoza Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, bilionea na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji (MO), ametangaza kujiondoa katika nafasi hiyo na kumteua Crescentius Magori kuwa Mwenyekiti mpya.

Akitangaza uamuzi huo leo, Septemba 4, 2025, MO alisema amebanwa na majukumu binafsi na mara nyingi kukosa muda wa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kila siku za klabu, hivyo akabaini nafasi hiyo inapaswa kushikiliwa na mtu aliye karibu zaidi na mwenendo wa klabu.

Hata hivyo, alibainisha kuwa ataendelea kubaki Rais na Mwekezaji Mkuu wa Simba SC, huku akiwashukuru wajumbe wa bodi waliotangulia kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya klabu hiyo kongwe.

Kwa mujibu wa Katiba ya Simba Sports Club Company Limited, Rais ana mamlaka ya kuteua viongozi wa bodi. Kupitia mamlaka hayo, MO amemteua Magori kushika nafasi ya Mwenyekiti na kuteua wajumbe saba wa bodi upande wake:

  • Barbara Gonzalez

  • Hussein Kitta

  • Azim Dewji

  • Rashid Shangazi

  • Swedi Mkwabi

  • Zuly Chandoo

  • George Ruhango