Dodoma. Unamkumbuka msanii wa zamani wa Bongo Fleva, Kedmon Ainea maarufu kama Ainea, aliyewahi kutamba miaka ya 2000 kupitia vibao kama “Sina Mpango Naye” aliyomshirikisha Mr Blue na “Somebody” akiwa na Shetta. Sasa ameokoka na ni mchungaji wa Kanisa la Anglikana Tanzania.
Kwa sasa, Ainea ameachana rasmi na muziki wa dunia na kugeukia uimbaji wa muziki wa injili.
Mbali na hilo, ameshahitimu stashahada ya uchungaji (diploma) na anasubiri kupangiwa kituo cha kazi kama mchungaji wa Kanisa la Anglikana.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Septemba 4, 2025, jijini Dodoma, Ainea amesema mabadiliko hayo hayakuwa rahisi, lakini aliamini ni mpango wa Mungu aliyemtoa kwenye maisha ya muziki wa Bongo Fleva ili amtumikie kwa njia ya huduma ya kiroho.
Akitazama nyuma, Ainea anasema alizaliwa na kukulia katika familia ya kichungaji, na tangu akiwa mtoto alikuwa sehemu ya mafundisho ya Kikristo kupitia shule ya Jumapili (Sunday School), hadi alipokuwa kijana na kujitambua.
Mwaka 2007, Ainea alihamia jijini Dar es Salaam ili kukuza kipaji chake cha uimbaji kupitia muziki wa Bongo Fleva. Baada ya miaka mitatu ya jitihada, mwaka 2010 alitoa wimbo wake wa kwanza uitwao “Moyo Utaniuma”, aliourekodi kwenye studio za Combination Sound chini ya mtayarishaji Prodyuza Man Water.
Ingawa wimbo huo haukupata mafanikio makubwa, mwaka mmoja baadaye alijipanga upya na kuachia wimbo “Sina Mpango Naye” akimshirikisha Mr Blue, ambao ulimtambulisha rasmi kwenye tasnia ya Bongo Fleva.
“Huu mwaka ndiyo niliotoa ‘hit song ya sina mpango naye’ na ndio ukawa mwanzo wa kutambulika kwenye anga la muziki wa bongo fleva,” amesema Ainea
Amesema hakuishia hapo mwaka 2013 alitoa wimbo mwingine kwa kumshirikisha mwanamuziki Shetta wa ‘Somebody’ ambao nao ulifanya vizuri kwenye muziki wa bongo fleva.
Ainea amesema mwaka 2018 alipokuwa studio anaandaa nyimbo zake alikuja mchungaji mmoja aliyemtaja kwa jina la Amani Kiwale wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kutoka mkoani Njombe ambaye alikwenda kurekodi nyimbo zake za dini kwenye studio hiyo.

Baada ya mchungaji huyo kufika alimwambia kuwa Mungu anamwambia kuwa yeye (Ainea) ni mtumishi wa Mungu kwa hiyo inabidi aachane na muziki wa dunia aanze kumwimbia Mungu.
Amesema baada ya kuambiwa hivyo alikubali kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu na iko siku atamtumikia Mungu kwa njia ya uimbaji.
Hata hivyo, mchungaji huyo aliendelea kusema naye kila mara alipokuwa anakwenda kurekodi nyimbo zake kuhusu kuokoka na kumtumikia Mungu na yeye alikuwa anamkubalia tu alikuwa habishani naye.
Ainea amesema siku moja alipokuwa anaandaa nyimbo zake wakiwa na yule mchungaji studio usiku wa manane alisikia sauti ikimwambia anatakiwa aende akaungane na yule mchungaji kuomba, kwani mchungaji huyo alikuwa upande wa pili wa studio alikuwa anaomba, lakini Ainea alikuwa hajui anaomba nini.
Amesema baada ya yule mchungaji kumaliza kuomba alimfuata na kumwambia kuwa Mungu amemwambia ampe zawadi ambapo alimpa zawadi ya Biblia ya agano jipya ndogo na kisha kuomba naye na kumwongoza sala ya toba.
Amesema baada ya hapo alianza kusali Kanisa la BCIC kwa Askofu Sylivester Gamanywa na kuachana na masuala ya muziki, hali iliyomfanya ashindwane na meneja wake kwani muda wa kufanya kazi yeye alikuwa anakwenda kanisani.
Ainea anasema baada ya kuona hawezi kuendelea na muziki na kilichompeleka Dar es Salaam ilikuwa ni muziki aliamua kurudi Dodoma kuendelea na maisha.
Amesema baada ya kurudi Dodoma haikuwa rahisi kwani alikuwa hana shughuli yoyote ya kufanya na hakujua wapi aanzie na ndipo alipoanza kazi ya kutengeneza sofa kwa kushirikiana na mtu ambaye tayari alikuwa na ofisi.
“Ile ofisi ya kutengeneza sofa ilikuwa karibu na barabara zinapopita daladala kwa hiyo watu walikuwa wananishangaa inafika hatua hadi daladala zinasimama ili wanione maana walivyokuwa wananiona nilipokuwa Dar ni tofauti na wanavyoniona sasa, wengine walikuwa wanasema ni yeye na wengine wanasema siyo yeye,” amesema.
Amesema pamoja na hayo yote aliendelea kutengeneza sofa ili kujipatia kipato hadi ilipofika mwaka 2022 alipoanza masomo yake ya uchungaji kwenye chuo cha Uchungaji cha Msalato Theological College kilichopo Dodoma na kuhitimu diploma ya uchungaji ambapo kwa sasa anasubiri kupangiwa kituo cha kazi.
Kwa kujua kuwa atakuwa mtumishi wa Mungu, Ainea alijiepusha kuchora tattoo kwenye mwili wake na hata rasta alizokuwa amefuga alizinyoa pindi tu alipookoka isipokuwa kutoboa sikio moja ambalo anasema halijaziba mpaka sasa japo huwa havai tena hereni.
Amesema baada ya kuokoka alimwomba Mungu amuondolee umaarufu na abakie kama mtu wa kawaida asiyekuwa na umaarufu wowote maisha ambayo ameyaishi mpaka sasa.
Baada ya kuokoka Ainea ametoa nyimbo tatu za injili ikiwemo Nimesikia ambao aliurekodi na video baada ya kuokoka na nyimbo nyingine mbili ambazo hazina video.
“Kwa sasa sitaki kuwa mtu maarufu nataka kumtumikia Mungu, na ndiyo maana japo mnajua kuwa mimi ni mwimbaji lakini sijatoa nyimbo nyingi baada ya kuokoka kwa sababu nataka kuwahubiri watu waokoke wamjue Mungu badala ya kuimba tu,” amesema Ainea.
Amesema baada ya kuokoka na kurudi Dodoma idadi kubwa ya marafiki ambao alikuwa anafahamiana nao kwa kupitia kazi ya muziki amepotezana nao amebaki na wale ambao anafahamiana nao nje ya muziki na kwamba hilo halimpi shida.
Kwa sasa amefungua studio ya kurekodi nyimbo ambayo ipo Kata ya Dodoma Makulu Mtaa wa Msangalalee Magharibi jijini Dodoma.
Kifo cha Sam wa Ukweli kilimsikitisha:
Ainea anasema kifo cha Sam wa Ukweli kilichotokea Juni, 2018 kilimsikitisha na kumkumbusha kuwa anatakiwa kujiandaa muda wowote kwani alitoka kuzungumza naye na kumweleza mipango yake mizuri aliyokuwa ameipanga kuhusu kutrend kwenye anga la muziki wa bongo fleva.
Amesema Sam wa Ukweli alimpigia na kumweleza mpango wake wa kumshirikisha Diamond na Ali Kiba kwenye wimbo mmoja na kwamba wimbo huo ungekuwa mzuri lakini wiki moja baada ya kuzungumza naye alisikia kuwa rafiki yake huyo amefariki kabla ya kukamilisha mipango yake.
“Hili lilinifikirisha sana kwamba tunatakiwa kujiandaa muda wowote na kifo maana mipango tunayoipanga bila Mungu ni kazi bure,” amesema Ainea.