UKIONA mchezaji anasajiliwa na hizi timu zetu mbili kubwa za Kariakoo, yaani Simba na Yanga ukute ana kitu ambacho zimekitathimini na kuona kama kinaweza kusaidia kuimarisha vikosi vyao.
Sasa mchezaji kusajiliwa huwa ni jambo moja na kwenda kuipa timu iliyomsajili matunda chanya hubakia kuwa jambo lingine ambalo linaweza kutokea au lisitokee.
Kijiweni hapa huwa tunashangaa sana tunapoona baadhi ya watu wanawashawishi wachezaji wazawa nchini wasikubali kujiunga na Yanga na Simba au hata Azam FC kwa sababu eti huko kuna wachezaji wazuri na wao hawatopata nafasi ya kutosha ya kucheza.
Ushauri wao mara nyingi huwa wa kuwataka wabakie katika klabu wanazozichezea ili waendelee kupata nafasi mara kwa mara kwa ajili ya kulinda vipaji vyao.
Hata kijiwe kinaamini fursa ya mchezaji kujiunga na Yanga au Simba haitakiwi kuchezewa hata kidogo na inapokuja mkononi itumiwe vizuri kwa vile huwa ni nadra kujirudia.
Hizo ni timu ambazo zinalipa mishahara mizuri na mikubwa lakini zina huduma za viwango vya juu nchini kuliko vingine zikichagizwa na uwepo wa wataalam waliobobea katika masuala ya ufundi na tiba.
Kwa hiyo mnaoanza kumtisha kipa Yakoub Suleiman aliyeamua kujiunga na Simba akitokea JKT Tanzania hatuwaungi mkono kwa vile mnampa imani ya woga badala ya kumjaza ujasiri ambao utasaidia kipaji chake.
Yakoub hatakiwi kuogopa kupambana na kipa Mousa Camara na badala yake anapaswa kuamini inawezekana yeye kuwa chaguo la kwanza, pia akaendelea kuilinda nafasi yake katika timu ya taifa.
Cha muhimu anatakiwa kutovipa kipaumbele vitendo vya kianasa na mitindo mibaya ya maisha ambayo itaporomosha kiwango chake na badala yake anapaswa kujituma katika viwanja vya mazoezi ili kulishawishi benchi la ufundi kumpa nafasi zaidi.