NLD yaja na misingi kwa wananchi, ikishinda urais

Tanga. Chama cha National League for Democracy (NLD) kimezindua rasmi kampeni zake na kuwanadi wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, huku kikieleza dira na misingi sita kitakayotumia katika uongozi wa nchi endapo kitapewa ridhaa na wananchi.

Akizungumza katika uzinduzi huo leo Alhamisi Septemba 4, 2025, mgombea urais kupitia chama hicho, Doyo Hassan Doyo amesema NLD imeandaa dira ya Taifa inayolenga kujenga ustawi wa jamii, kuimarisha uzalendo, haki na maendeleo, pamoja na kuweka msingi wa uwajibikaji, uongozi bora na ujenzi wa taasisi imara zitakazowajibika kwa wananchi.


Doyo ameitaja misingi sita ya chama hicho kama ilivyoainishwa katika ilani ya uchaguzi kuwa ni uzalendo, akisema Serikali ya NLD haitaruhusu madaraka kutumika kama miradi ya kifamilia au binafsi kwa ajili ya kunufaisha watu wachache.

Mgombea huyo amesema msingi mwingine kila Mtanzania atahakikishiwa haki bila kujali jinsia, dini, kabila au hali ya kiuchumi.

Doyo ametaja pia msingi wa uwajibikaji na uongozi wenye maadili akisisitiza kuwa viongozi na taasisi za umma, watawajibika kwa wananchi, huku rasilimali za Taifa zikiheshimiwa na kutumika kwa manufaa ya wote.


Ameutaja pia msingi wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na kijamii akisema Serikali ya chama hicho itatekeleza miradi mikubwa ya uchumi, ikiwamo ununuzi wa meli kubwa ya uvuvi kwa ajili ya kuwasaidia wavuvi wa Tanga.

Pia, Doyo amesema suala la ujenzi wa taasisi imara za umma utasaidia kuweka misingi ya uwajibikaji na hatua stahiki kuchukuliwa pale makosa yanapotokea.

Ametaja suala la maendeleo endelevu aliyosema yatazingatia hifadhi ya mazingira na matumizi ya teknolojia kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Chama cha NLD kimejengwa juu ya misingi ya haki, usawa, demokrasia na maendeleo jumuishi. Dira yetu ni kuwa na Tanzania yenye uchumi wa kisasa unaoleta maendeleo kwa wote bila ubaguzi, Taifa lenye watu huru, wenye maarifa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na maamuzi ya kitaifa,” amesema Doyo.


Mwenyekiti wa Kigoda cha Wazee wa NLD Taifa, Pozi Matwanga akimnadi mgombe huyo kwa wananchi waliojitokeza uwanjani hpo, amesema iwapo Doyo atachaguliwa kuwa Rais, Serikali yake itahakikisha vijana wanapata ajira endelevu badala ya kutegemea bodaboda pekee, huku sekta ya kilimo ikipewa msukumo wa kipekee kuinua pato la Taifa kupitia mazao ya chakula na biashara.

“Serikali ya NLD itaboresha ajira kwa vijana, itaimarisha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kuhakikisha wazee wanapata matibabu bora,” amesema Matwanga.

Naibu Katibu Mkuu wa NLD Zanzibar, Ahmed Salim Hammad amempongeza mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan kwa kitendo cha kuruhusu Serikali anayoiongoza kutoa magari ya kampeni kwa wagombea urais wa vyama vyote vilivyo na wagombea.

Naibu Katibu Mkuu wa NLD Tanzania Bara, Ramadhani Mwikalo amewataka wakazi wa Tanga kumpa kura nyingi Doyo huku akisisitiza kuwa ni mzaliwa wa mkoa huo na ameahidi kuwa Serikali ya NLD itakapoundwa, itaondoa mizani yote kwenye barabara kuu.

Aidha, Mwanasiasa mkongwe wa Tanga, Keya Ahmed Keya amewahimiza wananchi kufanya tafakuri ya kina kabla ya kupiga kura.

“Nawaomba wakazi wa Tanga, mtafakari vizuri. Mkiona changamoto zenu hazijapatiwa majibu, basi siku ya kupiga kura mfanye maamuzi sahihi,” amesema Keya.