Polisi yawashikilia 15 kwa kubandika SSH 2530 bila kibali

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu 15 waliokuwa wanatumia namba za gari za SSH 2530 baada ya Septemba Mosi mwaka huu Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime kutoa onyo ya matumizi ya namba hizo.

Misime alitangaza baadhi ya watu kubandika namba hizo kwenye magari yao kinyume na sheria ambapo ilikuwa inaanza kuchukua sura mpya ya kuendelea kubandikwa kwa namba hizo.

Mtu yeyote anayebandika namba hizo baada ya kufuatiliwa kwenye mifumo ya usajili, itahesabika hilo ni kosa la kisheria na atakayekamatwa atakuwa anatuhumiwa kwa kosa la kuendesha chombo cha moto bila ya kuwa na usajili wa namba rasmi.


Hayo yamesemwa leo Septemba 4, 2025 na Kamanda wa Kanda hiyo Jumanne Muliro alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya usalama ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 Marejeo ya Mwaka 1973 yaliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, mtu yeyote anayeendesha chombo cha moto bila kuwa na usajili rasmi na namba halali za usajili anatenda kosa la jinai.

“Ni makosa na swala hili ni kosa kisheria kwa sababu namba hizi hazipo kwenye mfumo wa usajili wa vyombo vya moto lakini pia ni kinyume cha sheria za usalama barabarani,” amesema Kamanda Muliro.

Pia, Kamanda Muliro amesema Agosti 11, 2025, Polisi limemkamata dereva aliyefahamika kwa jina la Ramadhani Makala, mkazi wa Tabata, kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.


Amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia gari aina ya Fuso, ambalo ndani yake kulikutwa magunia ya mahindi na mchele yaliyokuwa yamechanganywa na magunia 13 ya bangi.

“Mtuhumiwa huyu amehojiwa kwa kina yeye pamoja na wengine waliohusika na biashara hii ya haramu watashughulikiwa vikali na sheria za nchi,”amesema Muliro.

Aidha, Muliro amesema Agosti 12 hadi 22, mwaka huu jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata watu wawili ambao ni Hassan Hamis mkazi wa Tandale na Elia Mapunda mkazi wa Goba kwa tuhuma za kujihusisha na mtandao wa wizi wa pikipiki.

“Walikutwa na pikipiki sita pamoja na injini ambazo zingine zilikuwa zimesambaratishwa, zikihusishwa na matukio ya wizi maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na wao watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Amesema pikipiki hizo zilizokamatwa uchunguzi unakamilishwa na wamiliki wapatikane huku baadhi yao wamepatikana na hatua za kisheria zinachukuliwa ili kukomesha tabia ya wizi wa pikipiki.


Katika hatua nyingine, amesema wamekamata watuhumiwa watatu waliotajwa kuhusika na matukio ya uvunjaji nyumba na wizi wa vifaa vya kielektroniki wakati familia zimeondoka mchana.

Amesema watuhumiwa hao ni Gift Shaban, Hussein Ali na Riziki Ramadhan wote wakiwa wakazi wa Manzese na wamekamatwa wakiwa na simu mpya za aina tofauti pamoja na runinga zinazodaiwa kuibwa katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Amesema watuhumiwa wote hao watatachukuliwa hatua za kisheria kwa kushirikiana na vyombo vingine vya sheria.

Vilevile Muliro ametoa wito kwa familia katika kusherehekea Sikukuu ya Maulid kesho Septemba 5, 2025 kutokuacha nyumba bila kuwa na mtu.

“Kesho watu wanapokwenda mate.bezini wahakikishe kuna mtu wanamuacha nyumbani kwa ajili ya usalama,” amesema.