Rais wa zamani wa Peru, Alejandro Toledo amehukumiwa kifungo cha miaka 13 na miezi minne jela kwa tuhuma za utakatitishaji fedha akiwa madarakani.
Toledo (78) anaingia kwenye orodha ya marais wastaafu wengine watano ambao wamehukumiwa kwenda jela kwa tuhuma za ufisadi wakiwa madarakani.
Imelezwa kuwa Toledo, aliyekuwa rais kuanzia 2001 hadi 2006, alikutwa na hatia ya kutumia fedha za rushwa kutoka kwa kampuni ya ujenzi ya Brazil ya Odebrecht, ambayo sasa inajulikana kama Nononor.
Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, Toledo na mkewe pia walitumia Dola 5.1milioni kununua nyumba na ofisi katika kitongoji cha Lima.
Pia inaelezwa alitumua fedha hizo kufanya malipo baada kupokea fedha kutoka kampuni ya Costa Rica ambayo aliiunda mwenyewe ili kuzitumia fedha hizo haramu.
Kifungo hicho ni kingine cha mara ya pili kutokana na makosa aliyoyatenda kiongozi huyo kipindi cha uongozi wake, kwani Oktoba 2024 alihukumuwa kifungo cha miaka 20 na miezi sita jela.
Baada ya kukutwa na hatia ya kupokea fedha zisizo halali kutoka kampuni ya Odebrecht ili kuipa kampuni hiyo ukandarasi wenye faida kubwa.
Hata hivyo, kiongozi huyo amekanusha mashtaka ya utakatishaji fedha na kueleza kuwa huenda Serikali ikawa imekula njama na waendesha mashtaka ili kufanikisha hukumu hiyo ambayo yeye hakustahili.
Hukumu hiyo imetolewa huku marais wengine wawili wa zamani, Ollanta Humala na Pedro Castillo, wakiwa wanaendelea kushikiliwa katika kituo maalumu kilichojengwa kwa ajili ya viongozi wa zamani wa nchi.
Rais wa zamani Martin Vizcarra pia alikuwa akishikiliwa katika kituo hicho, licha ya Mahakama Muu ya Peru kutoa amri ya kuachiwa.
Vizcarra alifungwa jela mwezi uliopita kabla ya kusikilizwa kwa kesi yake, ambapo upande wa mashtaka umemtaka ahukumiwe kifungo cha miaka 15. Lakini yeye alikana mashtaka yote yaliotokewa dhidi yake, akisema kuwa ni aina ya mateso ya kisiasa.
Kiongozi mwingine wa zamani, Pedro Pablo Kuczynski, 86, kwa sasa yuko mahakamani kwa madai ya kuhusika na ufisadi huku waendesha mashtaka wakipendejeza afungwe kifungo cha miaka 35 jela.
Elidaima Mangela kwa msaada wa Mashirika