Rotary yatakiwa kugusa maisha, kujielekeza vijijini

Dar es Salaam. Uongozi na wanachama wa Klabu ya Rotary Club ya Bahari Dar es Salaam wametakiwa kupanua wigo wa huduma zao ili kuwafikia watu wengi zaidi katika sekta mbalimbali nchini.

Wito huo umetolewa na Gavana Mkuu wa Rotary anayesimamia Tanzania na Uganda, Christine Kyeyune Kawooya, katika mkutano maalumu na wanachama wa klabu hiyo ambao umefanyika leo Septemba 4, 2025 jijini Dar es Salaam.

Kawooya ameipongeza klabu hiyo kwa mchango wake katika nyanja za elimu, afya, uhifadhi wa mazingira na huduma za kijamii.

Pia, amesisitiza haja ya kuongeza juhudi zaidi ili kuendelea kugusa maisha ya watu wengi na kuimarisha utamaduni wa kujitolea.

Aidha, ameeleza umuhimu wa kuimarisha Mfuko wa Rotary (Rotary Foundation) kwa kuongeza michango ya wanachama kupitia ushirikiano na makampuni binafsi pamoja na serikali, ili kufanikisha miradi ya maendeleo ya kijamii.

 “Rotary Club ya Bahari imeonyesha uongozi na kujitolea, lakini mahitaji bado ni makubwa. Lazima tuendelee kubuni, kushirikiana na kupanua wigo wetu kuhakikisha hakuna jamii inayosalia nyuma,” amesema.

Ameongeza kuwa juhudi kama hizo zitawezesha klabu kukuza Rotary nchini na kufikia kiwango kingine.

“Rotary Club ya Bahari imefanikiwa kutekeleza miradi inayoshughulikia baadhi ya changamoto kubwa zaidi za kijamii,” amebainisha.

Amehimiza klabu isiishie kujikita mijini pekee bali pia kupanua uanachama kwa kuanzisha klabu nyingi zaidi maeneo mbalimbali.

Pia, amesisitiza klabu hiyo kuwapa kipaumbele maeneo mawili ambayo ni kupunguza vifo vya mama na watoto pamoja na kuimarisha mpango wa W.A.S.H. ambao unahisiana na udhamini wa Rotary unaosaidia miradi ya maji na usafi wa mazingira.

Alisema kuwa klabu ya Bahari pia imekuwa na mchango mkubwa katika kulea klabu zingine za Rotary, ikiwemo Rotary Club ya Kwanza, kwa kuendeleza wakufunzi wanaoweza kufanya kazi na shule za mijini na vijijini.

“Wakufunzi hawa wamekuwa wakiwahamasisha wanafunzi kukumbatia STEAM, Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Sanaa na Hisabati, masomo muhimu kwa kuwaandaa vijana wa Tanzania kwa maisha ya baadaye,” amesema.

Miongoni mwa miradi mikubwa ni Mradi wa STEAM, ambao tayari umefikia wanafunzi zaidi ya 800 jijini Dar es Salaam na Zanzibar.

Kupitia mafunzo ya walimu na “bootcamps,” mradi huu umewahamasisha vijana kuchunguza fursa za kazi katika sayansi na teknolojia huku ukiwapa ujasiri na stadi za kushindana katika dunia inayobadilika haraka.

Amesema pia Rotary Bahari pia imeacha alama katika afya. Mradi wa ‘You and Me for Her’ wa uhamasishaji kuhusu saratani ya shingo ya kizazi umehusisha zaidi ya wajitoleaji 40, waliotoa elimu, kuhamasisha uchunguzi na kushajiisha chanjo kwa ajili ya kugundua mapema na kuzuia ugonjwa huo.

“Zaidi ya hapo, mpango wa ‘Rotary Family Health Day’ umeimarisha mchango wa klabu hiyo katika afya ya jamii kwa kutoa huduma zaidi ya 10,000 kwa wanajamii 1,022.

Afya ya mama na mtoto inaendelea kuwa kipaumbele cha juu. Mradi wa Tricycle Ambulance, ambao tayari unafanya kazi, unakabiliana na changamoto za usafiri kwa akina mama wajawazito katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.

Kufuatia mafanikio hayo, klabu sasa inapanga kuzindua motorbike ambulances chini ya Ambulance Access Initiative, mradi unaotarajiwa kunufaisha zaidi ya akina mama na watoto wachanga 5,000 kwa mwaka.

Kwa upande wake, Rais mteule wa Rotary Club ya Bahari, Irene Bizere amesema kuwa miradi mingi ya klabu hiyo imezingatia mahitaji ya jamii huku ililenga zaidi mabadiliko halisi katika maisha ya watoto, wanawake.

Amesema kuwa wanajivunia kufanikisha miradi mingi pamoja na kutambua kuwa wanakazi kubwa mbele yao kutokana na mahitaji.

“Rotary Bahari imejizatiti kuongeza juhudi katika elimu ya STEAM, afya ya mama na mtoto, na uhifadhi wa mazingira. Tunataka kuhakikisha kila mradi tunaoufanya ni endelevu na unaacha athari ya kudumu, amesema.”

Kwa kuunga mkono dira hiyo, klabu imewekeza katika uhifadhi wa mazingira. Imeotesha miti 1,360 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuzindua miradi ya “micro-forest” mashuleni.

Miradi hii, Gavana Kawooya alibainisha, “inaonyesha dhamira ya Rotary kwa ustawi na maisha bora ya vizazi vijavyo.”

Amesema elimu inabaki kuwa nguzo kuu ya klabu hiyo. Miongoni mwa miradi yake muhimu ni Udhamini wa Sh5 milioni wa Maji wa Rotary, unaounga mkono programu ya shahada ya uzamili katika Maji na Usafi wa Mazingira.

“Udhamini huu unaonyesha jinsi Rotary inavyoweza kuchangia katika kukuza uwezo wa muda mrefu kwenye sekta muhimu,” amesema Gavana Kawooya.

Kwa kuangalia mbele, Rotary Club ya Bahari imebainisha vipaumbele vinne vikuu kwa mwaka huu: Ambulance Access Initiative kwa kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto, STEM Train-the-Trainer Program kwa kuwawezesha walimu, kampeni ya upandaji miti mashuleni na kwenye jamii na Mradi wa Incinerator katika Shule ya Msingi Toangoma, unaonufaisha wanafunzi zaidi ya 3,000 wakiwemo 35 wenye ulemavu.

Kwa uanachama imara na historia ya huduma zenye athari tangu ilipoanzishwa mwaka 1988, Rotary Club ya Bahari inaendelea kujitokeza kama moja ya klabu zenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Tanzania, ikibaki mwaminifu kwa kaulimbiu ya Rotary ya “Service Above Self, Huduma Zaidi ya Nafsi.”