Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imehitimisha mvutano wa kisheria kwa kutoa uamuzi wa rufaa za mapingamizi ya wagombea wa upinzani na chama tawala kwa ubunge na udiwani, uamuzi ulioacha baadhi ya wagombea wakifurahia ushindi huku wengine wakibaki na masikitiko.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima, Septemba 3, 2025, tume hiyo ilipokea jumla ya rufaa 51 za kupinga maamuzi ya wasimamizi wa uchaguzi. Kati ya hizo, rufaa 20 zilihusu ubunge na 31 zilihusu udiwani.
Kailima amesema rufaa 13 kati ya 51 zilishughulikiwa katika kikao cha INEC kilichofanyika Agosti 31, 2025 na katika vikao vyake kuanzia Septemba 1 hadi Septemba 3, 2025, rufaa 38 zilizobaki zilifanyiwa uamuzi.
Kwa upande wa ubunge, INEC imesema imekubali rufaa nne, imezikataa saba na moja kufutwa. Katika ngazi ya udiwani, rufaa tisa zimekubaliwa huku 17 zikikataliwa.
Katika uamuzi huo, imetupilia mbali pingamizi dhidi ya wagombea wa ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Esther Matiko wa Jimbo la Tarime Mjini na Esther Bulaya wa Jimbo la Bunda Mjini mkoani Mara.
Uamuzi huo umetolewa baada ya tume hiyo kukubaliana na hoja zilizotolewa katika rufaa za wagombea hao, na kuthibitisha kuwa uteuzi wao ni halali, hivyo wapo huru kuendelea na kampeni na kuwania nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Awali, Matiko aliweka pingamizi dhidi ya Kangoye Jackson, lakini Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tarime Mjini, Erasto Mbunga, alitupilia mbali pingamizi hilo lakini Matiko alikata rufaa INEC na kushinda.
Matiko, alidai Kangoye alijiunga na ACT – Wazalendo kinyume na taratibu, akibainisha kuwa aliingia kwenye chama hicho kabla ya kutimiza siku saba tangu alipojiondoa CCM, na baada ya mchakato wa ndani wa chama chake kipya kukamilika.
Hata hivyo, baada ya kupitia hoja hizo, msimamizi wa uchaguzi alitupilia mbali pingamizi hilo na kumruhusu Kangoye kuendelea na mchakato wa kugombea ubunge kupitia ACT -Wazalendo katika uchaguzi huo.
Pia, mgombea ubunge katika Jimbo la Bunda Mjini kupitia ACT – Wazalendo, Pius Masuruli alienguliwa kufuatia pingamizi la Bulaya na rufaa aliokata kwa INEC imekataliwa.
Kufuatia maamuzi hayo jimbo la Bunda Mjini limebaki na wagombea watatu kutoka vyama vya CCM, NLD na CUF.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Septemba 4,2025, Matiko amesema uamuzi huo wa INEC umefanyika kwa kuzingatia katiba na kununi za uchaguzi za ACT-Wazalendo ambazo pamoja na mambo mengine, zinaeleza kuwa ili mwananchama aweze kugombea lazima awe amejiunga na chama hicho zaidi ya siku saba.
“Jackson anasema amejiunga na ACT Agosti 6, lakini si kweli kwa sababu yeye alikuwa kiongozi wetu wagombea watano tulioshiriki kura za maoni ndani ya CCM na hatukuridhika na mchakato mzima, hivyo tukakata rufaa kwenye chama,” amesema.
Amesema Agosti 6, Kangoye akiwa kiongozi wa wagombea wengine akiwepo yeye (Matiko) aliwasilisha rufaa yao kwenye uongozi wa CCM wilaya, kabla ya kuwasilisha rufaa hiyo kwenye uongozi wa mkoa Agosti 8, kisha kuiwasilisha kwenye uongozi wa chama taifa Agosti 11.
“Sasa hapo unaweza kuona namna gani hao ACT – Wazalendo walivyokwenda kinyume na katiba yao na kanuni zao kwa sababu kwa muda huo, huyu alikuwa bado ni mwanachama wa CCM na ninaamini alijiunga na ACT- Wazalendo Agosti 24 na si vinginevyo,” amesema Matiko.
Kwa uamuzi huo wa INEC jimbo la Tarime Mjini linabaki na wagombea wanne akiwemo yeye na wagombea wa Chaumma, AAFP na UPDP.
Kwa upande wake Masuruli, amesema uamuzi dhidi yake ni dhuluma kwa wakazi wa Bunda Mjini kwani hawakupewa nafasi ya kumchagua mbunge wanayemtaka.
Masuruli amesema uamuzi huo umefanyika ili kumpa nafasi mgombea wa CCM ili aweze kupita kwa urahisi kutokana na ukweli kuwa yeye anakubalika kwa wakazi wa jimbo hilo na Bunda Mjini, na hivyo uwepo wake kwenye kinyang’anyiro ulikuwa ni tishio kwa CCM na mgombea wake.
“Vitu vyote walivyotaka niwasilishe kutokana na rufaa dhidi yangu niliwasilisha ikiwepo kadi ya uanachama pamoja na kuwasilisha kama jina langu lipo kwenye tovuti ya chama, sasa sijui walitaka nifanye nini,” amehoji.
Amesema uamuzi uliofanywa na INEC ni upendeleo kwa CCM huku vyama vya upinzani vikionewa, jambo ambalo amesema halina afya katika suala zima la demokrasia nchini.
Amesema wagombea wote bila kujali vyama vyao walitakiwa kupewa fursa sawa ili maamuzi yaweze kufanywa na wananchi siku ya uchaguzi.
Amefafanua kuwa ili siasa ziweze kuwa na usawa ni vema kukawepo na mizania ya usawa badala ya chama tawala kupendelewa.
Kwa upande wa ubunge, mbali na zile za Bulaya na Matiko, INEC imetaja rufaa zilizokubaliwa kuwa ni ya Mvungi Felix, mgombea Jimbo la Mwanga (NCCR Mageuzi), aliyekata rufaa dhidi ya msimamizi wa uchaguzi jimbo la Mwanga baada ya kuenguliwa kugombea. INEC imemrudisha kugombea.
Rufaa nyingine zilizokubaliwa ni ile ya Anael Nasari, mgombea Jimbo la Arumeru Mashariki (ACT – Wazalendo) ambaye ameshinda pingamizi alilowekewa na Joshua Nassari wa Chama cha Mapinduzi (CCM), naye amerudishwa.
Nyingine ni ya Ngwada Twaha mgombea ubunge Jimbo la Mafinga Mjini kupitia Chaumma dhidi ya Villa Lutevele Dickson wa CCM.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tume, rufaa saba za ubunge zilizokataliwa ni pamoja na ile ya Gimbi Masaba, mgombea katika Jimbo la Itilima (Chaumma), aliyekata rufaa dhidi ya Njalu Silanga wa CCM.
Rufaa nyingine zilizokataliwa ni ya Omary Badwel, mgombea Jimbo la Bahi (Chaumma), dhidi ya Keneth Nallo wa wa CCM.
Nyingine ni ya Mohammed Juma Haji mgombea wa Jimbo la Chambani (AAFP) dhidi ya msimamizi wa uchaguzi Chambani.
Pia imekataliwa ya Loyce Giboma, mgombea wa u Jimbo la Ubungo (Chaumma), dhidi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo.
Pia Tume imefuta rufaa ya ya Flatei Massay, mgombea ubunge Mbulu Vijijini AСТ-Wazalendo kwa kuwa imepitwa na matukio baada ya kuhamia CCM.
Kufuatia uamuzi huo, Dk Onesmo Kyauke, mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala, nchini amesema mapingamizi yameonekana kuwa machache mwaka huu tofauti na uchaguzi wa 2020, akidokeza kuwa mengi huonekana kuegemea upande wa upinzani, jambo linalotoa taswira mbili.
“CCM wanaonekana kutokuwa na mapingamizi mengi, hii inajenga sura mbili, huwezi kuhukumu moja kwa moja kuwa kuna upendeleo, labda wao wapo makini zaidi, inawezekana wanasheria wao wanawasidia wagombea katika kujaza fomu zao, hapa ni vigumu kuhukumu kwa kuwa hatuwezi kujua misingi ya mapingamizi yaliyowekwa,” amesema.
Amesema ili mtu aseme kuna upendeleo lazima aone kama kuna kesi za kufanana, mgombea mmoja ameenguliwa na mwingine akiruhusiwa.
“Angalau mwaka huu mapingamizi hayajawa mengi zaidi, ningeshauri Tume ifike wakati kama kuna makosa madogo ya ujazaji wa fomu wawe na nafasi kwa mlalamikiwa kurekebesha fomu.
“Watu waenguliwe wakiwa na makosa makubwa ya kisheria kama umri wa kugombea, uraia na mambo mengine yenye mashiko kama mtu kutokuwa mwanachama wa chama kinachomdhamini, tofauti na hapo ni kuwanyima watu haki za kikatiba kuchagua na kuchaguliwa,” amesema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Loisulie, ametoa mtazamo wa pande mbili, kwanza kuwa kilichotokea kinaonyesha ishara ya upendeleo wa mifumo kwa chama tawala kwa misingi kuwa wanaoenguiliwa zaidi ni wagombea wa upinzani, pia ameonyesha hofu kwa wapinzani kutokuwa makini na michakato ya maandalizi ya uchaguzi, ambayo huwapa mwanya CCM kuwawekea pingamizi.
“Inaonyesha kuwa mzani bado haujakaa sawa, bado mzani unaegemea upande wa chama tawala lakini vyama vya upinzani havijajipanga pia vya kutosha, vinatoa mwanya kukatiwa rufaa na kulalamikiwa, wengi wanaibuka ghafla na kujaza fomu haraka. Kujaza fomu za uchaguzi pia kunahitaji umakini wa kutosha, wapinzani wasitoe mwanya, watu watapitia hapo hapo,” amesema na kuongeza:
“Ukiangalia haya yanayofanyika yanafanya uchaguzi unakosa ladha, tangu mwanzo wapo watu wameshakata tamaa siku nyingi tangu chama kikuu cha upinzani, Chadema kiliposhindwa kushiriki uchaguzi, hata mapingamizi haya ni kama hayana kelele nyingi uraiani kwa sababu hiyo,” amesema.