Sababu za kushamiri kwa matumizi kadi za kielektroniki nchini

Miaka michache iliyopita, tulipozungumza kuhusu kadi za malipo, wengi tungefikiri kuwa ni kadi ya plastiki inayotolewa na benki inayotumika kutoa pesa kwenye mashine ya ATM au kupangusa kwenye mashine maalum madukani.

Lakini taswira hiyo sasa inabadilika kwa kasi. Ongezeko la matumizi ya simu janja limefanya kadi hizo zisiwe tena kipande cha plastiki kinachoweka mfukoni au katika pochi, bali kwa sasa ni kadi za kidijitali unayoweza kutengeneza na kuitumia ndani ya simu.

Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania kuhusu mwenendo wa mifumo ya malipo nchini kwa mwaka 2024 inaonesha kuwa idadi ya kadi za kielektroniki (virtual cards) zilizotolewa imeongezeka kwa kasi kufikia jumla ya kadi 820,832 kutoka 511,826 mwaka 2023 uliopita. Hii ni sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 60 kwa mwaka mmoja tu. Kadi hizi zilifanikisha miamala milioni 4.51 yenye thamani ya Sh220.15 bilioni na Dola za Marekani 187.33 milioni.

Nyuma ya takwimu hizi kuna maisha halisi ya watu: kijana anayelipia tiketi ya ndege mtandaoni, mzazi akigharamia masomo ya mtoto, mfanyabiashara akinunua bidhaa kutoka nje, na wengineo. Unaweza kusema ongezeko la matumizi ni ishara ya kukua kwa mahitaji ya watu kufanya malipo kwa kadi hizo.

Kwa nini sasa? Kwanza, sababu kubwa muhimu ni kuenea kwa matumizi ya simu janja kumechangia pakubwa, kitakwimu sasa idadi ya simu hizo nchini ni zaidi ya milioni 23.

Kupitia simu, mtumiaji anaweza kubadilisha salio la fedha lililopo kwenye akaunti yake ya mtandao wa simu kuwa kadi ya kimataifa, inayoonekana kama Visa au Mastercard, na kulipia huduma au bidhaa yoyote papo hapo bila kuhitaji kubadili fedha ya kigeni. Shukrani kwa huduma za kifedha mitandao ya simu ambazo zimetoa fursa ya kutengeneza kadi hizo wakati wowote na kuitumia mtandaoni.

Pili, ni kukua kwa biashara mtandaoni (e-commerce). Kadiri maduka na huduma mbalimbali zinavyohamia mtandaoni mathalani nguo, huduma za malazi, chakula, gharama za safari, na nyingine, kadi za kielektroniki zimekuwa ngao ya usalama na urahisi katika kufanya malipo. Huhitaji kwenda popote; unatengeneza na kulipa mara moja.

Na tatu, unaweza kuongezeka kwa uelewa wa matumizi ya mifumo ya malipo katika mfumo wa kidijitali.

Hata hivyo, bado tunaweza kusema matumizi ya kadi hizi hayajawa ya kawaida kwa Watanzania wote. Takwimu zinaonesha ni asilimia 19 pekee ya kadi zote ndizo zinazotumika mara kwa mara. Na hata hizo, nyingi zinabaki mikononi mwa kundi dogo la watu wenye simu janja na uwezo wa kulipia gharama za intaneti.

Zaidi ya hapo, mwenendo wa kadi za ndani (local brand cards) unayumba. Mwenendo unaonesha matumizi yake yameporomoka kwa karibu asilimia 28, huku Watanzania wengi wakihama kwenda kwenye kadi za kimataifa kama Visa na Mastercard. Kwa maneno mengine, kadi hizo zinapigwa na dhoruba kali ya upepo na wimbi katika bahari ya ushindani wa huduma za malipo kidijitali.

Mwelekeo huu unaonesha wazi kwamba kadi za kielektroniki si mtindo wa mpito, bali ni sehemu ya mustakabali wa malipo nchini. Ukuaji wake ni ishara kwamba Tanzania ipo kwenye njia ya uchumi wa kidijitali unaopunguza kwa hatua matumizi ya fedha taslimu.

Iwapo jitihada za kuongeza ujumuishaji wa kifedha, elimu ya kifedha, na uwekezaji kwenye miundombinu ya malipo zitaendelea, bila shaka itabadilisha namna tunavyoishi, kushiriki kwenye uchumi, na kufanya malipo ya mahitaji yetu ya kila siku.

Wasiliana nami kwa namba  0678745333 au