Samia awataja wakulima akiahidi kongani za viwanda

Mbalizi.  Leo ikiwa ni siku ya nane tangu kuzinduliwa kwa kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025, mgombea wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameendelea kutoa ahadi kwa wananchi endapo watamchagua.

Katika maeneo yote aliyopita, mgombea huyo amekuwa akitoa ahadi zinazolenga kuchochea maendeleo na ustawi wao hasa katika huduma za kijamii na shughuli za kiuchumi.

Leo Septemba 4, 2025 akiwa katika mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya akiendelea na ziara yake ya kampeni, Samia amesema Serikali yake ikipatiwa ridhaa kwa mara nyingine, itaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima nchini.


Mgombea huyo ameahidi kuendelea kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo huku akisema  matokeo ya ruzuku hizo ni makubwa hususani kwa Mkoa wa Mbeya wanakozalisha zaidi mazao ya pareto, mahindi, mpunga na maparachichi na asilimia 85 ya wananchi wake ni wakulima.

Amewahakikishia uwezo wa Serikali kutoa ruzuku bado upo, hivyo amewataka wajisajili na kutunza namba za siri huku akionya mbolea za ruzuku siyo kwa ajili ya kuuzwa.

“Nakumbuka nilipokuja hapa mlinieleza hitaji lenu kubwa ni mbolea. Nililifanyia kazi, mbolea imegawiwa na wakulima wamenufaika. Lengo letu tuzalishe, tujilishe na ziada tuuze kama mazao ya biashara. Tanzania tuna ziada ya chakula, niwashukuru sana wakulima.

“Niwaombe sana wakulima, mkajisajili kupata ruzuku ya pembejeo kwani uwezo wetu wakutoa ruzuku upo. Mbolea tunazotoa kwa ruzuku siyo kwa ajili ya kuuzwa, msishirikiane na waovu kuuza vitu vinavyotolewa kwa ruzuku,” amesema mgombea huyo.

Kwa upande wa mifugo, Samia ameahidi kukamilisha ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Utengule.

Pia, ameahidi kuitambua mifugo yote iliyopo nchini na kuichanja ili kujihakikishia soko la nyama la nje linalozingatia viwango vya ubora.


“Niwahakikishie ndugu zangu, huko nje kuna soko kubwa la nyama, lazima tujipange kutumia fursa hiyo,” amesema Samia kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi.

Akizungumza wakati wa mkutano wake wa kampeni katika Jimbo la Mbeya Mjini, ukiwa ni mkutano wake wa pili mkoani hapa baada ya ule uliofanyika Mbalizi, Jimbo la Mbeya Vijijini, ameahidi kuanzisha kongani za viwanda katika Mkoa wa Mbeya ili kuwawezesha vijana kuongeza thamani mazao yao kabla ya kuyapeleka sokoni.

 Amesema kongani hizo zitakuwa za mazao tofauti kama kilimo, mifugo au madini, lengo likiwa ni kuwaongezea vijana uwezo wa kushindana na kunufaika na shughuli zao za uzalishaji.

“Tunakwenda kuweka kongani za viwanda ili vijana wa Mbeya waongeze thamani mazao yao na wanayokwenda kuyauza sokoni, wapate faida zaidi,” amesema Samia.

Amesema kuelekea mwaka 2030, kuna ajenda ya kuifanya sekta ya kilimo ikue kwa asilimia 10 kutoka asilimia sita ya sasa.

“Ndiyo maana tunachukua hatua za kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima ili tuweze kufikia asilimia hizo 10 ifikapo mwaka 2030,” amesema Samia.


Mgombea aomba halmashauri

Mgombea ubunge Jimbo la Mbeya Vijijini, Patali Shida Patali amemuomba mgombea urais wa CCM akiingia madarakani, aupandishe hadhi mji mdogo wa Mbalizi ili uwe halmashauri ya mji, jambo ambalo amesema litachochea maendeleo kwa wananchi.

Amesema Mbalizi ni mji wa biashara, uko karibu na Uwanja wa Ndege wa Songwe na pia utapitiwa na mradi wa barabara nne kutoka Igawa kwenda Tunduma, hivyo una kila fursa ya kukua na kuwa na hadhi ya mji.

“Ukitupa mji kamili, utakuwa umetupa motisha kwa kazi kubwa unayoifanya,” amewasilisha ombi hilo kwa mgombea urais wa CCM, Samia.

Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, mbunge mstaafu wa viti maalumu, Sophia Mwakagenda amemuomba Samia kuupandisha hadhi mji wa Mbalizi ili kutoka mji mdogo na kuwa halmashauri ya mji wa Mbalizi.

“Mheshimiwa, Mbalizi ni mji mdogo, tunaomba uwe mji kamili. Tunajua ukisema neno moja, mambo yanakuwa,” amesema Mwakagenda ambaye alikuwa mbunge wa viti maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Akijibu ombi hilo, Samia amewataka kuendelea na mchakato wa maombi ya kupandishwa hadhi kwa mji mdogo wa Mbalizi, muda ukifika wataamua.

“Kwenye hili, nadhani michakato ya ndani imeanza, nimeambiwa hapa. Lipelekeni Tamisemi na likikamilika tutaangalia itakavyokuwa,” amesema Samia ambaye ni mgombea urais wa CCM.


Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa machifu wa Mbeya Vijijini, Shayo Masoko ameeleza kusikitishwa na watu wanamtukana Samia mitandaoni licha ya kazi kubwa aliyoifanya ya kuleta katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Amesema wananchi wanachotakiwa kumpatia ni shukrani kwa kazi kubwa aliyoifanya, lakini machifu wanasikitishwa na matusi mitandaoni, hivyo amewataka machifu wengine kote nchini kuchukua hatua za kimila kuwaadabisha watu hao wanaotukana mitandaoni.

“Machifu wote Tanzania, tuchukue hatua dhidi ya hawa wapuuzi…tutumie mambo yetu ya kimila, mpuuzi wa namna hii alaaniwe,” amesema Chifu Masoko huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Dk Tulia na kura za heshima

Mgombea ubunge wa Jimbo la Uyole Dk Tulia Ackson amesema wananchi mkoani humo wameahidi kumpa kura za heshima kwa kuwa ameituliza Mbeya kwa kuwapa wananchi shughuli za kufanya na hivyo kuondoa maandamano.

Dk Tulia aliyekuwa Spika wa Bunge lililopita, amesema sababu za kumpa Samia kura za kishindo ni kutokana na fedha za miradi ya maendeleo alizozipeleka Mbeya kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya, vifaa tiba (MRI) katika hospitali ya rufaa, huku elimu ikiwa ni zaidi ya Sh1 bilioni.

“Shule za sekondari za Shewa, Airport, Mwashinga na nyingine ni sehemu ya utekekelezaji wa ilani ya CCM. Kwa upande wa maji, katika Jiji la Mbeya pekee, Sh30 bilioni zimeletwa; Sh16 bilioni ya mapato ya ndani zimesaidia kata kupata maji, kuna miradi ya maji ya Itagano, Mwansekwa na Mwashari, yote inaendelea.

“Kuna mradi mkubwa wa maji wa Mto Kiwira ambao utaenda kumaliza kero ya maji, kuna mradi wa Tactic ambao unajenga stendi kuu ya mabasi kwa Sh21 bilioni, Soko Matola Sh6 bilioni miradi inayoenda kuamsha shughuli za wananchi,” amesema.


Kabudi, Chongolo watia neno

Mgombea ubunge Jimbo la Kilosa ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema wakati akitembelea miradi katika mkoa huo, akimwakilisha Rais, ameshuhudia kasi kubwa ya maendeleo vijijini ambako vituo vya afya vya kisasa, vyenye vifaa, vimejengwa.

Kwenye sekta ya kilimo, Profesa Kabudi amesema Mbeya inafanya vizuri katika uzalishaji wa pareto, iliifanya Tanzania kushika nafasi ya pili kwa uzalishaji wa zao hilo baada ya Australia, akieleza kuwa, hayo ni matokeo ya ruzuku ya pembejeo inayotolewa na Serikali.

“Hilo limewezekana ndani ya miaka mitatu iliyopita. Tena niwaambie Australia wajiandae, Tanzania inakwenda kuwa ya kwanza kwa uzalishaji wa pareto,” amesema Profesa Kabudi.

Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Daniel Chongolo amesema Samia ni mtu mwenye dhamira ya dhati katika kuwaletea wananchi maendeleo na kwamba amedhihirisha hilo kwenye utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya 2020 – 2025.

“Kushinda kwa kishindo, kwako ni uhakika kutokana na kazi kubwa ambayo umeifanya. Nikuombe, usitumie sauti kubwa kuomba kura, sisi ambao ni wanufaika wa kazi uliyofanya, tutapaza sauti kukuombea kura,” amesema Chongolo.