KUNA pongezi nyingi ambazo kijiwe kimeamua kutoa kwa TFF na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuandaa semina elekezi kwa marefa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao ya namna ya kupambana na vitendo vya rushwa.
Ni jambo zuri ndiyo maana tunalipongeza kwa vile marefa ni watu muhimu sana katika kuendeleza au kudumaza mchezo wa soka kwa sababu wao ndio wamepewa mamlaka ya mwisho ya kuzitafsiri Sheria 17 za soka uwanjani.
Ni lazima kuwepo na semina kama hizo maana zinawafanya marefa wetu wapate ufahamu mpana kuhusu rushwa michezoni na athari zake, hivyo itasaidia kupunguza au hata kuondoa kama jambo hilo lipo kwenye soka letu na hata kama halipo basi itafanya waamuzi wawe na uoga nao.
Baada ya semina hiyo kinachohitajika hivi sasa ni marefa kuanza kuyatekeleza kwa vitendo yale ambayo wamefundishwa na kuelekezwa katika semina hiyo ya juzi.
Hakutakuwa na maana kama watu wamepewa elimu ya kutosha na gharama kubwa imetumika na mamlaka za soka na TAKUKURU halafu wale ambao wamepatiwa wanaenda kinyume kwamba wanajihusisha au kushiriki katika vitendo hivyo.
Dhamana ambayo marefa wamepewa kuhusu sheria za soka ni kubwa sana hivyo wakiruhusu kushiriki vitendo vya rushwa, watakuwa wanauweka rehani mchezo wa soka nchini ambao kiukweli umepiga hatua kubwa.
Lakini hili lisiishie kwa marefa tu, bali pia hata wadau wa soka nao wanatakiwa wasaidie katika shughuli hizi za kupambana na vitendo vya rushwa katika soka hasa katika Ligi Kuu.
Na kundi kubwa la wadau hao ni viongozi wa klabu za soka ambao kuna nyakati baadhi yao wamekuwa wakihusishwa na utoaji wa rushwa kwa waamuzi ili wawarubuni wawapendelee katika mechi zao.
Tunahitaji mpira wa miguu ambao unachezwa katika mazingira ya usafi ili timu zipate matokeo ya halali, pia kukuza zaidi soka letu.