Serikali yawasilisha ombi lingine kesi ya Boni Yai, Malisa

Dar es Salaam. Wakati kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni inayomkabili Boniface Jacob maarufu Boni Yai na mwanaharakati Godlisten Malisa, ikisubiri uamuzi wa Mahakama Kuu ili kuendelea na usikilizwaji, Jamhuri imeomba kufanya mabadiliko ya kielelezo katika kesi hiyo.

Usikilizwaji bado haujaanza baada ya Jamhuri kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kukataa ombi lake la kulindwa mashahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo.

Uamuzi huo ulitolewa Mei 5, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo aliyesikiliza ombi hilo. Katika uamuzi aliotoa alitupilia mbali ombi la upande wa mashtaka akieleza halina mashiko.

Jacob, meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam na Malisa, mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kutoa taarifa za uongo mitandaoni.

Wawili hao wanadaiwa kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii ya X na Instagram kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015, wakilihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia.

Leo Alhamisi Septemba 4, 2025 wakati kesi ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa, Wakili wa Serikali, Cathbert Mbiling’i alieleza kesi imeitwa kwa ajili ya kutajwa na bado wanasubiri uamuzi wa Mahakama Kuu kutokana na rufaa waliyokata dhidi ya uamuzi uliotolewa Mei 5, 2025 na Mahakama ya Kisutu.

“Washtakiwa wapo mbele ya mahakama, shauri hili limeitwa kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka tusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu. Kule Mahakama Kuu maombi yetu yamepangwa kutajwa Septemba 16, 2025, hivyo tunaomba utupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amesema Mbiling’i.

Wakati huohuo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekubali ombi la upande wa mashtaka na kuruhusu kitabu cha Polisi cha usajili wa vielelezo vya kutumika Mahakamani (PF16) cha mwaka 2023/2024 kirejeshwe kwa Jeshi la Polisi ili kuendelea kutumika kwa kazi za jeshi hilo.

Kitabu hicho ni kielelezo namba tatu cha upande wa mashtaka na kilishapokewa na Mahakama wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.

Baada ya kuchukuliwa kitabu hicho halisi, mahakama imebaki na nakala yake.

Wakili Mbiling’i baada ya kesi kutajwa aliomba kufanya mabadiliko katika kielelezo hicho namba tatu cha upande wa mashtaka kwa kuwasilisha nakala ili kitabu halisi kirudishwe Polisi kuendelea na kazi nyingine.

Alieleza sababu ya kuwasilisha ombi hilo ni kuwa, kitabu hicho kimebeba vielelezo vyote vya mwaka 2023 na 2024.

Baada ya ombi kutolewa, Hakimu Swallo aliwauliza washtakiwa iwapo wana pingamizi kuhusu mabadiliko hayo. Jacob na Malisa walisema hawana pingamizi.

Hakimu Swallo amesema kwa kawaidia kitabu hicho huwa hakikai mahakamani, badala yake hutolewa nakala ya kitabu halisi na kurudishwa Polisi kiendele na kazi nyingine, hivyo alikubali ombi la upande wa mashtaka.

Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 15, 2025 itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Tayari mashahidi watano wa Jamhuri wameshatoa ushahidi mahakamani.

Washtakiwa katika kesi ya jinai namba 11805/2024 wanastakiwa kwa makosa matatu wanayodaiwa kutenda kati ya Machi 19 na Aprili 22, 2024 jijini Dar es Salaam.

Wanadaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mitandao yao ya kijamii ya X na Instagram kinyume cha sheria, wakidaiwa kulihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya mkazi wa Dar es Salaam, Robert Mushi maarufu Babu G na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, wilayani Karatu mkoani Arusha, Omari Msemo.

Jacob anadaiwa kuandika licha ya ndugu kutoa taarifa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, lakini kila siku Polisi walikuwa wakisema hawajapata taarifa wala fununu zozote na kuwataka ndugu waendelee kuwa wavumilivu wakiendelea kumtafuta.

Hata hivyo ndugu walidokezwa na msiri akiwataka waende Hospitali ya Polisi Kilwa Road wakachungulie vyumba vya kuhifadhi maiti ambako walikwenda wakamkuta ndugu yao akiwa ameuawa na wahusika wa hospitali walidai maiti ilipelekwa tangu Aprili 10, 2024 na askari wa Jeshi la Polisi.

Katika andiko lake alihoji: “Maiti ina siku 12 Hosptali ya Polisi Kilwa Road haijui bila Jeshi la Polisi kujua ipo hapo? Polisi walioipeleka maiti ni wa nchi gani?”

Kwa mara ya kwanza washtakiwa walifikishwa mahakamani Mei 6, 2024 na kusomewa mashtaka matatu, mawili kati ya hayo yanamkabili Jacob, huku Malisa akikabiliwa na shtaka moja.