Shilingi yaendelea kuimarika licha ya kuwa katika kipindi cha uchaguzi

Dar es Salaam. Kwa kawaida, shilingi ya Tanzania huwa inapoteza thamani inapokaribia kipindi cha uchaguzi mkuu, ikiporomoka kwa kasi dhidi ya sarafu kuu za kigeni.

Mwelekeo huo ulidhihirika wazi katika chaguzi za mwaka 2015 na 2020.

Mwaka 2015, thamani ya shilingi ilishuka kutoka Sh1,754.7 kwa Dola moja ya Marekani mwezi Januari hadi Sh2,180.1 kufikia Oktoba katika Soko la Ndani la Kubadilishana Fedha za Kigeni (IFEM).

Kabla ya uchaguzi wa 2020, shilingi ilianza kudorora kutoka Sh2,258.2 Machi mwaka 2018 hadi Sh2,300.46 mwaka mmoja baadaye, na kushuka zaidi na kufikia Sh2,309.06 wakati wa kampeni.

Hali hiyo ililazimisha mamlaka kuingilia kati kwa kufunga baadhi ya maduka ya kubadilisha fedha yaliyobainika kukiuka kanuni.

Hata hivyo, mwaka huu hali imekuwa tofauti, Tanzania inapokaribia kufanya uchaguzi mkuu wa 2025, takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha shilingi kuwa Juni 2025 ilikuwa na wastani wa Sh2,666.79 kwa dola, sasa imeimarika na kufikia kati ya Sh2,257.05 na Sh2,481.63.

Wataalamu na maofisa wa Serikali wanahusisha uthabiti huu wa kipekee na nidhamu ya sera za kifedha na bajeti, ongezeko la mapato ya fedha za kigeni, uboreshaji wa mauzo ya nje pamoja na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji.

Nidhamu ya sera za kifedha

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema uimara wa shilingi unatokana na utekelezaji wa sera kwa ushirikiano wa karibu.

“Sera thabiti ya fedha, ikisaidiwa na usimamizi mzuri wa bajeti, imehakikisha upatikanaji wa dola katika soko rasmi,” amesema Tutuba katika mahojiano na The Citizen.

“Tumeweza kudhibiti ukwasi, viwango vya riba na mfumuko wa bei ndani ya malengo tuliyojiwekea, na yote haya yamechangia uthabiti wa shilingi,” ameongeza.

Aidha, mapato ya fedha za kigeni kutoka sekta za utalii, madini na kilimo yameongezeka. Mauzo ya dhahabu, tumbaku, matunda na mboga yamepanda kwa kasi, huku sekta ya utalii ikionekana kurejea kwa nguvu baada ya janga la Uviko 19.

Gavana pia ametaja uamuzi wa Serikali wa kununua dhahabu na kuongeza akiba ya fedha za kigeni kuwa umechangia pakubwa hali hii.

Tanzania, ikiwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika, imefaidika kutokana na bei ya dhahabu kufikia rekodi ya takribani Dola 3,559 kwa wakia. BoT imeongeza ununuzi wa dhahabu kutoka ndani ya nchi ili kuimarisha akiba na kupunguza utegemezi wa sarafu ngumu.

Nakisi ya biashara ya nje kupungua

Kwa mujibu wa Gavana, nakisi ya biashara ya nje imepungua na sasa ni asilimia 2.6 ya Pato la Taifa (GDP) kutokana na uuzaji bidhaa kwenda nje kuzidi uagizaji.

“Uboreshaji huu katika mizania ya malipo ni kiashiria muhimu cha uimara wa shilingi,” amesema.

Aidha, BoT imeimarisha usimamizi wa soko kwa kudhibiti biashara ya fedha kwenye masoko yasiyo rasmi. Sheria mpya sasa inataka yeyote mwenye zaidi ya Dola milioni moja kuziuza kupitia benki za kibiashara kwenye soko la IFEM.

Pia, sheria ya mwaka 2025 inayotaka miamala yote ya ndani kufanywa kwa shilingi imesaidia kupunguza mahitaji ya dola.

Wachambuzi wamesema mazingira ya kimataifa na ya ndani yamechangia uthabiti huu. Wakati Benki Kuu ya Marekani (Fed) imepandisha viwango vya riba, wawekezaji wa kimataifa wamekimbilia dhahabu kama njia salama ya kuhifadhi thamani, hali inayosaidia Tanzania kupata mapato zaidi ya kigeni.

Mchumi huru, Christopher Makombe, amesema uthabiti wa shilingi katika mwaka wa uchaguzi ni jambo la kipekee.

“Safari hii ni tofauti. Bei za juu za bidhaa, utulivu wa kisiasa na upinzani mdogo wa kisiasa vimejenga mazingira ya kujiamini kwa wawekezaji,” amesema.

Makombe ameongeza kuwa baadhi ya wawekezaji wa kigeni wananunua hisa katika masoko ya ndani, jambo linaloashiria hatari ndogo ya mabadiliko ya sera.

Pia, uwekezaji unaoendelea kwenye miradi mikubwa ya kimkakati kama Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere unatarajiwa kupunguza utegemezi wa mafuta kutoka nje, hivyo kupunguza gharama za nishati na kuimarisha shilingi kwa muda wa kati.

Shirika la kimataifa la ukadiriaji wa uwezo wa kulipa madeni, Fitch Ratings, limeendelea kuipa Tanzania alama ya B+ kwa mtazamo imara, hali inayoongeza imani ya wawekezaji kuhusu usimamizi wa uchumi wa nchi.

Profesa Abel Kinyondo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema mienendo ya msimu pia imechangia.

“Kwa kawaida, shilingi huimarika kati ya Aprili na Septemba wakati wa msimu wa utalii. Mwaka 2020, janga la corona lilikomesha utalii na kupunguza mapato ya fedha za kigeni. Hivi sasa, bei ya dhahabu ni ya juu na sekta ya utalii imerejea kwa nguvu, hali inayoiimarisha zaidi shilingi,” ameeleza.