Mirerani. Watoto wa jamii ya wachimbaji wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, watanufaika na elimu baada ya Serikali kutoa Sh330 milioni za kuanza ujenzi wa shule ya awali, msingi hadi ya kidato cha sita.
Katika eneo hilo linalotegemea uchumi wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani itakuwa shule ya kwanza ya Serikali kujengwa itakayosomesha watoto kuanzia chekechea, shule ya msingi hadi kidato cha sita sekondari.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga akizungumza na Mwananchi Digital Septemba 4, 2025 amesema shule hiyo mpya itakuwa ya mfano katika eneo hilo pindi ikikamilika.

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga (katikati) akifurahia na wanafunzi wa shule ya sekondari Mirerani B.W.Mkapa, baada ya kukagua ujenzi wa shule mpya ya awali, msingi na sekondari ya kidato cha sita. Picha na Joseph Lyimo
Sendiga amesema Serikali imeshatoa fedha Sh330 milioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule hiyo itakayoanza kwa ngazi ya awali, msingi, hadi sekondari kidato cha sita.
Amewapongeza viongozi wa kata ya Endiamtu kwa kutunza maeneo ya wazi na kupatikana sehemu ya kujenga shule ya awali, msingi na sekondari ya kidato cha sita.
“Tunashukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hii ya mfano,” amesema Sendiga.
Mkuu wa shule ya sekondari Mirerani B.W.Mkapa, Samwel Kaitira amesema fedha za ujenzi wa shule hiyo mpya wamezipokea Julai Mosi, 2025.
Mwalimu Kaitira amesema majengo ya shule hiyo yatakayojengwa ni ya utawala na madasara sita ya shule ya msingi.
Ametaja majengo mengine ni vyumba viwili vya madarasa ya awali, chumba maalumu cha wasichana na kichomea taka, matundu 20 ya vyoo vya madarasa ya awali, shule ya msingi na vya walimu.
Mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa shule ya sekondari Mirerani B.W. Mkapa, Andrew Lyimo amesema ni hatua nzuri kwa ujenzi wa shule hiyo mpya.
“Tunampongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea shule hiyo mpya ya chekechea, msingi na sekondari ya kidato cha sita,” amesema Lyimo.
Mkazi wa kata ya Endiamtu, Sokota Mbuya amesema ujenzi wa shule hiyo mpya utasababisha mageuzi makubwa ya kielimu kwa wanafunzi wa eneo hili.
“Hatujawahi kuona shule ya namna hii mwanafunzi unaanza chekechea, shule ya msingi hadi sekondari kidato cha sita, hapa Mama Samia, RC wetu Sendiga na Diwani wa kata Lucas Zacharia wamefanya kazi nzuri mno,” amesema.