Simu ilivyofanya mapinduzi ujumuishi wa kifedha Tanzania

Fikiria hali ingekuwaje leo hii kama huduma za fedha kwa njia ya simu zisingekuwepo nchini. Bila shaka unaweza kuvuta picha namna ambavyo kungekuwa na foleni kubwa benki na maeneo mengi ya huduma.

Pengine kungekuwa na matukio mengi ya uporaji kutokana na kukithiri kwa matumizi ya pesa taslimu. Suala la kupokea au kutuma fedha kwa ndugu na jamaa hususan wa kijijini lisingekuwa rahisi, mabasi ya abiria, bodaboda, jirani na ndugu ndiyo wangefanikisha muamala huo ambao hivi sasa unaishi mkononi tu.

Huduma za fedha kwa njia ya simu zimeleta mapinduzi makubwa katika mfumo mzima wa kifedha nchini, zikibadilisha maisha ya wananchi mijini na vijijini, na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za mfano barani Afrika katika ujumuishi wa kifedha.

Kabla ya ujio wa huduma za simu za mkononi, benki ndizo zilihesabika kama njia pekee ya kuhifadhi fedha au kufanya miamala mikubwa. Hata hivyo, upatikanaji wa huduma za benki ulikuwa changamoto kubwa, hususan maeneo ya vijijini ambako matawi ya benki hayapo au yako mbali sana.

Lakini sasa simu za mkononi zinakamilisha mambo mengi, mtu anaweza kutuma, kupokea au kulipia bili akiwa kijijini bila kulazimika kusafiri kilomita nyingi kwenda mjini. Hii imepunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa foleni na gharama za usafiri zilizokuwa zikihusiana na kupata huduma za kifedha.

Watoa huduma wanajivunia kuwa sehemu ya safari hiyo, Mkurugenzi wa Biashara wa Mixx by Yas James Sumari anasema miaka 15 ya wao kutoa huduma nchini imegusa maeneo mengi na kubwa zaidi kuwezesha na kurahisisha maisha ya watu.

“Tulianza na huduma ya kutuma na kupokea pesa baadaye tukaongeza huduma za kufanya malipo kidijitali na sasa tunatoa huduma za kifedha,” anasema Sumari ambaye anasimamia biashara ya Mixx by Yas ambayo utawala wake sokoni ni asilimia 30.

Kwa mujibu wa Takwimu za Mawasiliano za Mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) Idadi ya akaunti za pesa mtandao ambazo zilitumika angalau mara moja katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita iliongezeka hadi kufikia milioni 68.1 katika robo ya mwaka iliyoishia Juni 2025.

Mixx inachangia asilimia 30.4 ya miamala milioni 66.5 (20,672,815) huku idadi ya miamala yake kwa mwezi Juni pekee ikiwa 198,289,442 kati ya miamala yote 442,018,792 ilifanyika mwezi Juni 2025.

Sumari anasema hivi sasa watumiaji wa huduma za miamala wanapata huduma nyingi zaidi ya kutuma na kupokea fedha huduma hizi ni kama  kufanya malipo (lipa kwa simu), kupata mikopo (Bustisha na Nivushe) na kuweka akiba kwa faida ya hadi asilimia 6 kwa mwaka (Kupitia huduma ya kibubu).

“Tunafanya mambo mengi kuhakikisha watu wanapunguza matumizi ya pesa taslimu ndiyo maana huduma zetu, zinagusa makundi yote kuanzia watumiaji was imu wa kawaida, wajasiriamali wadogo, wa kati na hata wakubwa huduma zetu zina suluhisho mahsusi kwa ajili yao,” anasema Sumari.

Hata hivyo anatoa tahadhari kwa wakopaji akisema ni muhimu mikopo itumike kwa matumizi yenye tija ili kuweza kufanya marejesho kwa wakati, kwani ulipaji mbaya au mkopo chechefu unaweza kuwa na athari hasi katika rekodi ya mikopo ya mteja.

Kuongeza ujumuishi wa kifedha

Takwimu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania sasa wanatumia huduma za kifedha kupitia simu zao za mkononi. Hii ni hatua kubwa ikilinganishwa na hali ya awali ambapo idadi kubwa ya wananchi hawakuwa na akaunti za benki.

Huduma za simu zimewawezesha watu wengi zaidi kuingia rasmi katika mfumo wa kifedha wakiwemo wakulima wadogo, wafanyabiashara wa mitaani, na wafanyakazi wa kipato cha chini. Kwa mfano, kwa sasa, mkulima anaweza kupokea malipo ya mazao yake moja kwa moja kupitia simu, badala ya kubeba fedha taslimu ambazo ni hatari na gharama kubwa.

Mtaalamu wa huduma za fedha kidijitali kutoka kutoka Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) Yessie Yasin amesema kwa sehemu kubwa huduma za kifedha kwa njia ya simu zimepunguza hofu ya kutoaminiana na kuongeza urahisi wa kupata huduma.

“Bila huduma za fedha kwa njia ya simu ujumuishi ungekuwa chini mno kwani kutumia huduma za kibenki ni gharama kubwa ambazo watu wengi wa kijijini hawawezi kuzimudu, kwanza watoa huduma wake sio wengi hivyo mtua anayetaka kuweka fedha kidogo anatumia fedha nyingi kufanikisha hilo,” alisema Yasin.

Anasema hata ripoti ya takwimu za utafiti wa huduma za fedha (Finscope) za mwaka 2023 zinaonyesha kuwa ujumuishi wa kifedha nchini umefikia asilimia 76 lakini katika idadi hiyo benki zinachangia asilimia 22 tu.

Yasin anasema huduma kwa njia ya simu zimesaidia kuwafikia watu wengi zaidi ambao isingekuwa rahisi kufikiwa na huduma za kibenki kupitia matawi kwani hata kuanzisha matawi ni gharama kubwa tofauti na kuanzisha wakala.

“Simu zimepunguza gharama na muda wa kupata huduma, muhimu ni kuendelea kuwa wabunifu kwa kuwa na huduma ambazo zinaongeza ujumuishi na kutatua changamoto za watu akitolea mfano huduma ya ‘Kibubu’ ambayo inatoa suluhu ya uwekezaji na kumpatia mteja faida,” anasema Yasin.

Sehemu kubwa ya hoja za Yasin ziliungwa mkono na Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Thobias Swai ambaye anasema huduma za miamala zimeongeza ujumuishi kwa kiwango kikubwa na zina nafasi ya kufanya zaidi.

“Huduma za miamala kwa simu zimerahisisha, kutuma, kupokea pesa na mikopo na gharama zake zikiendelea kupungua zitavutia watu wengi zaidi na matumizi ya pesa taslimu yatapungua kwa kiwango kikubwa,” anasema Swai.

Mageuzi kibiashara na kijamii

Huduma za fedha za simu pia zimekuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta ndogo na kubwa za biashara. Maduka makubwa, masoko ya jumla, stendi za mabasi, na hata mama lishe, wengi wao sasa wanakubali malipo kupitia simu. Hii imerahisisha biashara, imepunguza hatari ya wizi na kuongeza uaminifu kati ya wauzaji na wanunuzi.

Vilevile, huduma hizi zimekuwa zikitumika kulipia huduma za umma kama vile umeme wa Luku, maji, ada za shule, na hata kodi za Serikali. Matokeo yake, mapato ya Serikali yameimarika huku ufanisi wa ukusanyaji mapato ukiongezeka.

Zaidi ya shughuli za kibiashara, huduma za fedha kwa simu zimekuwa msaada mkubwa katika jamii. Familia sasa zinatumiana fedha kwa urahisi mzazi anaweza kumtumia mwanafunzi ada akiwa mbali, ndugu anaweza kusaidia gharama za matibabu kijijini, na watu wanaweza kuchangia harusi au misiba papo kwa papo.

Mary John, mkazi wa Dodoma, anaeleza: “Kabla ya huduma hizi, nililazimika kutumia zaidi ya saa tatu kusafiri kwenda mjini kulipa bili ya umeme au ada ya shule ya mtoto. Siku hizi mambo ni rahisi, nalipa kupitia simu yangu nikiwa nyumbani au sokoni. Hata kodi ya serikali nalipa kwa urahisi bila kupoteza muda.”

Aidha, miamala ya simu imekuwa kichocheo cha biashara ndogo na za kati (SMEs). Wafanyabiashara wa rejareja sasa wanapokea malipo kwa njia ya simu kutoka kwa wateja wao, jambo linaloongeza uaminifu na kupunguza gharama za kuhifadhi fedha taslimu.

Lakini pia huduma za fedha kwa njia ya simu zimetoa zimetoa ajira kwa maelfu ya mawakala waliopo kila mtaa na kijiji, hivyo kuongeza fursa za kipato.

Upande wa kilimo, mkulima wa korosho Mtwara anaweza sasa kuuza mazao yake na kulipwa moja kwa moja kupitia simu, badala ya kusubiri malipo kupitia mabenki yaliyoko mjini. Hali hii imeongeza uwazi katika manunuzi na kuondoa hatari ya wizi wa fedha taslimu.

Pamoja na mafanikio haya makubwa, bado kuna changamoto ya udanganyifu na utapeli wa mtandaoni. Akizungumza katika mkutano wa mawakala wa miamala ulioandaliwa na benki ya Equity, Mkuu wa Kitengo cha Malipo wa benki hiyo, Haidary Chamshama alisema kadri huduma za kifedha kwa njia ya kidijitali zinavyokuwa ndiyo utapeli na ulaghai unavyozidi kuongezeka katika eneo hilo.

Sumari anasema ili kushughulikia utapeli na kuhakikisha huduma za miamala ya simu zinakuwa salama watumiaji pamoja na mifumo ya ndani wamekuwa wakisisitizwa kutunza namba zao za siri lakini pia imewekewa mifumo ya mtu kujiridhisha na muamala anaoufanya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya robo ya pili ya mwaka ulioishia Juni, 2025 kampuni Yas ambayo ndiye mama wa Mix by Yas ilikuwa ya pili kwa kuwa na visa vichache vya ulaghai nyuma ya TTCL.