STRAIKA wa zamani wa timu ya taifa ya Zambia, Tapson Kaseba amefariki dunia leo mchana katika Hospitali ya Mafunzo ya Chuo Kikuu (UTH), baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Rais wa Shirikisho la soka Zambia, (FAZ) Keith Mweemba ametangaza kifo cha straika huyo akiandika; “Tumesikitishwa na kifo cha Tapson Kaseba tuliyemfahamu kama mchezaji wa zamani wa timu ya taifa na klabu nyingi katika ligi yetu. Mawazo yetu yako na familia yake,” ameandika Mweemba.
Waziri wa Vijana, Michezo na Sanaa, Elvis C. Nkandu ameandika kwa masikitiko makubwa; “Serikali inasimama na wapendwa wake na familia kubwa ya soka katika kipindi hiki kigumu. Roho yake ipumzike kwa amani ya milele,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Awali, Kaseba alilazwa katika Kituo cha Tiba cha Maina Soko kwa siku chache kabla ya kuruhusiwa, lakini baadaye hali yake ya kiafya ilibadilika na kurudishwa tena hospitali ambako alifariki dunia.
Katika maisha yake ya soka, Kaseba aliwahi kuchezea klabu mbalimbali ikiwemo Lime Hotspurs, Kansanshi Dynamos, Kabwe Warriors, Green Eagles, NAPSA Stars, Buildcon na Konkola Blades.
Akiwa na Green Eagles, alifanya vizuri msimu wa 2018/19 akifunga mabao 18
na kushika nafasi ya pili kwenye ufungaji mbele ya nyota wa zamani wa Azam FC, Idriss Mbombo aliyeweka kambani mabao 21 akiwa na Zesco United.
Ubora aliouonyesha katika msimu huo ulimfanya kocha Aggrey Chiyangi kumpa nafasi katika timu ya taifa ya Chipolopolo na mwaka 2019 alifunga bao pekee kwenye fainali ya COSAFA Cup dhidi ya Botswana, Zambia ikishinda 1-0.