ZIKIWA zimesalia takribani wiki mbili kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-26, uongozi wa Tabora United umesema inataka timu kufanya vizuri zaidi ili kumaliza ligi ndani ya nafasi nne za juu kwenye msimamo tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.
Timu hiyo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kukusanya pointi 38 ikishinda michezo kumi 10 kati ya 30, sare minane na kupoteza 12.
Nafasi ya nne ilishikwa na Singida Black Stars ikikusanya pointi 57, zikiwa ni 15 zaidi ya Tabora United. Nafasi ya tatu ilikuwa Azam, kisha Simba ya pili na Yanga ikabeba ubingwa.
Akizungunza na Mwanaspoti, Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Charles Obiny, amesema katika kipindi hiki cha maandalizi kuelekea msimu wa 2025-26, msisitizo mkubwa ni katika kuimarisha kikosi chenye ushindani zaidi.
Obiny amesema uimara wa kikosi chao utafanya kufikia malengo waliyojiwekea ya kumaliza ligi katika nafasi ya juu zaidi kuanzia ya nne.
“Tunaendelea na maandalizi ya msimu na tuko hapa Manyara kucheza mashindano yaliyoandaliwa na Fountain Gate ikiwa ni sehemu ya kujiweka sawa.
“Ligi inakaribia kuanza na kama unavyofahamu msimu uliopita tulimaliza katika nafasi ya tano, safari hii tunaitaka nafasi ya juu zaidi ya hapo, kila timu huwa na malengo na hayo ndio malengo yetu,” alisema kiongozi huyo.
Obiny alibainisha kuwa, hata usajili walioufanya umelenga kufikia hayo malengo, hivyo anaamini hakuna kinachoshindikana.
“Kuna wachezaji wameondoka hivyo lazima tufanye usajili kuziba hayo mapengo, tunaamini hawa tuliowasajili watatufikisha kule tunapopataka,” amesema Obiny.
Miongoni mwa wachezaji walioondoka Tabora United ni Heritier Makambo na Offen Chikola huku baadhi ya wachezaji waliotua kikosini hapo katika usajili wa dirisha kubwa uliofunguliwa Julai Mosi, 2025 na kutarajiwa kufungwa Septemba 7, 2025, ni Shaban Chilunda, Adam Adam, Abdulaziz Makame na Nnanna Churchil.
Ratiba ya Ligi Kuu Bara 2025-26, inaonyesha Septemba 20, 2025 Tabora United itaanzia nyumbani kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kukabiliana na Dodoma Jiji.