Tanesco yaja na teknolojia ya matengenezo bila kukata umeme

Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limefanya matengenezo kinga kwenye njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovoti 220 kutoka Kituo cha kupoza umeme Chalinze hadi Kituo cha Kinyerezi Dar es Salaam bila kuzima umeme (live line).

Teknolojia hiyo ya ‘live line’ inalenga kupunguza upotevu wa umeme kutokana na kuzima laini pamoja na kuondoa malalamiko ya wateja wa maeneo husika ambao hapo awali walilazimika kukosa huduma ya umeme kwa muda ili kupisha matengenezo kinga.


Matengenezo hayo yamehusisha ubadilishaji wa vikombe (insulator) ambavyo vilionekana kuwa na changamoto katika ukaguzi uliofanywa kwenye njia hiyo ya kusafirisha umeme ambapo hapo awali ingelazimu kuzima umeme kwenye laini hiyo ambapo ingesababisha maeneo yanayopata umeme kupitia njia hiyo kukosa huduma kipindi cha matengenezo.

Akingunzumza wakati wa zoezi hilo Mhandisi kutoka Kitengo cha usafirishaji umeme Philemon Tirukaizile amesema teknolojia hiyo imeondoa kero ya kukatika umeme kwa wananchi wakati wa matengenezo.


“Bila kuwa  na teknolojia hii  ya  kufanya matengenezo bila  kuzima  umeme, tungeweza  kuzima  njia yetu  ya kusafirisha umeme  kwa muda wa saa sita. Inamaana baadhi ya wateja wetu kuanzia hapa Chalinze kuelekea Mlandizi mpaka maeneo ya Kibaha wangeweza kukosa huduma ya umeme,” amesema Tirukaizile.

Akifafanua namna wanavyotekeleza zoezi hilo, msimamizi wa timu ya usafirishaji Mkoa wa Pwani Sadiki Sadiki amesema zoezi hilo linatekelezwa na mafundi wabobezi wenye mafunzo kwa kuzingatia usalama wa hali ya juu.


“Kabla hatujaanza kazi yetu huwa tunafanya mawasiliano ya watu wetu wa Kituo cha kupoza umeme ili waweze kupewa kibali cha kufanya zoezi hili. Baada  ya hapo tunakua na kiongozi wa timu husika na  kila mmoja  anakuwa akizingatia usalama lakini kiongozi wa timu  ndiye   anatuma  maelekezo  nani afanye nini na wakati gani,” ameeleza. 

Kwa upande wake Bahati Ramadhani ambaye ni fundi katika kitengo hicho amesema ujuzi huo ameupata kupitia mafunzo maalumu aliyoyapata ndani ya Shirika.

“Shirika  limenijenga  kwa sababu  kabla  ya  kuanza  kazi  hii nilianza na mafunzo  kwenye msongo mkubwa  wa  njia  ya  kusafirisha umeme ya  Kilovoti 400 kutoka Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), na mafunzo yanaendelea. Kwa kweli ni fahari yetu mteja kuwa na umeme wakati wote,” amesema Bahati.