TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kufunguliwa kwa awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026 kuanzia Septemba 3, hadi Septemba 21 mwaka huu.
Pia tume imewasisitiza waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili ama kudahiliwa katika awamu ya kwanza kutokana na sababu mbalimbali kutumia fursa hiyo kwa kutuma maombi yao ya udahili kwa vyuo wanavyovipenda.
Katibu Mtendaji wa TCU, Prof.Charles Kihampa amesema hayo leo Septemba3,2025 alipokuwa akitangaza kukamilika kwa udahili wa awamu ya kwanza na kufunguliwa kwa awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza 2025/2026
Kufuatia kufunguliwa kwa awamu ya pili, tume pia imezielekeza taasisi za Elimu ya juu kutangaza programu ambazo bado zina nafasi huku waombaji wa vyuo pia wakihimizwa kuzingatia utaratibu wa udahili kwa awamu ya pili.
“Waombaji na vyuo wanahimizwa kuzingatia utaratibu wa udahili kwa awamu ya pili kama ilivyooneshwa kwenye kalenda ya udahili iliyotolewa na TCU na kama inavyooneshwa kwenye tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz)”. Amesema Prof.Kihampa.
Aidha Prof.Kihampa amesema kuwa katika awamu ya kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 146,879wametuma maombi ya kujiunga katika vyuo 88 vilivyoidhinishwa kudahili wanafunzi wa Shahada ya kwanza.
Amesema jumla ya programu 894 zimeruhusiwa kudahili ikiilinganishwa na programu 856 za mwaka jana ikiwa ni ongezeko la programu 38 za masomo kwa mwaka huu
Prof. Kihampa amesema kuwa nafasi za udahili zimeongezeka kwa kiasi cha nafasi 6,666 sawa na asilimi 3.3 ikiwa mwaka uliopitiwa nafasi zilikuwa 198,986 na mwaka huu nafasi ni 205,652.
Amesema katika awamu ya Kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 116,596 sawa na asilimia 79.4 ya waombaji wote walioomba udahili, wamepata udahili kwenye vyuo walivyoomba.
Aidha Tume imewataka waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja kuthibitisha udahili wao kwa kuchagua chuo kimojawapo kuanzia Septemba 3,hadi Septemba 21 mwaka huu kwa kutumia namba zao za simu ama barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.