KOCHA wa timu ya taifa ya Walemavu, Tembo Warriors, Ivo Mapunda amesema timu hiyo itaondoka nchini kesho kwenda Bujumbura, Burundi kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati ya Soka kwa Watu wenye Ulemavu (CECAAF).
Mashindano hayo yatakayofanyika kwa siku saba kuanzia Septemba 8-14, yamegawanywa katika makundi mawili. Tembo Warriors ikipangwa Kundi B pamoja na Kenya na Uganda, huku Kundi A likiwa na Zambia, DRC Congo na wenyeji Burundi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mapunda aliyewahi kuwa kipa wa Simba, Yanga, Azam FC na Taifa Stars, amesea maandalizi ya wiki mbili yalikwenda vizuri, akibainisha kuwa mechi mbili za kirafiki zimempa mwanga wa maeneo yenye mapungufu.
“Tulikuwa na maandalizi mazuri Uwanja wa Yombo Makangalaw, tulipata mechi mbili za kirafiki. Ijumaa tunaanza safari ya kuelekea Bujumbura kwa ajili ya mashindano, na mechi ya kwanza tutacheza na Kenya Septemba 9,” amesema Mapunda.
Baada ya awali kuita kikosi cha wachezaji 25, kocha huyo alifanya mchujo na kupata kikosi cha wachezaji 15 watakaoliwakilisha taifa kwenye mashindano hayo.
Wachezaji walioteuliwa ni: Ally Juma, Bashra Alombile, Abdulakreem Khalifa, Hassan Vuai, Richard Swai, Emmanuel Mrefu, Ally Cheche, Juma Kidevu, Rojas Vicent, Kassim Mbarouk, Frank Ngairo, Julius Ole Keika, Salim Chambo, Salehe Mwipi na Modrick Mohammed.
Tembo Warriors ndio watetezi w taji baada ya kutwaa taji hilo mwaka jana kwa kuifunga Uganda, huku Kenya ikimaliza nafasi ya pili.
Pamoja na kufanya vizuri kwenye mashindano hayo, timu hiyo inakabiliwa na changamoto za kifedha kugharamia mahitaji muhimu yakiwemo safari, vifaa tiba na dawa.
“Sisi tuna changamoto kubwa. Hatuna vifaa tiba, dawa, kwa ufupi kila kitu kinachohitajika kwenye soka tuna upungufu. Tunaomba msaada na Watanzania waendelee kutusapoti kwa kutuchangia chochote ili tuweze kushiriki mashindano hayo. Tunawaahidi tutafanya vizuri,” amesema Mwenyekiti wa Chama cha Soka kwa Walemavu Mkoa wa Arusha (ARAFA), Daudi Mnongya.