Dar es Salaam. Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kimesema kikipata ridhaa ya wananchi ya kuongoza nchi miaka mitano ijayo, wanafunzi kuanzia elimu ya awali hadi sekondari watasafiri bure kwenye mabasi.
Hatua hiyo imeelezwa ni kutokana na tabu wanayopata wanafunzi wanapokwenda shuleni na wanaporejea nyumbani.
Ahadi hiyo imetolewa leo Septemba 4, 2025 na mgombea urais wa chama hicho, Yustas Rwamugira wakati wa uzinduzi wa kampeni za TLP uliofanyika Manzese, jijini Dar es Salaam.

Vilevile, ameahidi elimu ya ufundi itaanza kufundishwa kuanzia darasa la awali hadi chuo kikuu, elimu ikiwa miongoni mwa mambo manne ya kipaumbele ya chama hicho. Mengine ni kilimo, afya na kuwainua wananchi kiuchumi.
Amesema utoaji elimu ya ufundi unalenga kila kijana anapomaliza shule awe na maarifa jambo litakalomsaidia kujiajiri na kuajiriwa.
“Vijana kuanzia chekechea (darasa la awali) hadi vyuo lazima wajifunze ufundi kwa kusoma na kufanya kwa vitendo. Kama ni kujenge wajenge, kulima walime, kwa nini tuite wataalamu kutoka nje,” amehoji na kuongeza:
“Hatutahitaji wawekezaji waje kuwekeza wakati tuna vijana hawana kazi.”
Kuhusu afya amesema matibabu yatakuwa bure na kila mmoja atakuwa na bima ya afya awe boda au bajaji.
“Kuna mtoto wa rafiki yangu ni dereva bodaboda alipata ajali akavunjika mguu, hela ya kujitubu akawa hana na kazi hana, lakini endapo angekuwa na bima ingemsaidia,” amesema.

Akizungumzia uwezeshaji wananchi kiuchumi, amesema wanataka kuona wenye maduka wote wanapewa nguvu na uwezo kwa kuwa na benki yao, huku kazi ya Serikali itakuwa kukusanya kodi kwao.
Katika miradi mikubwa amesema anataka kuona wajenzi wazawa wakipewa kazi na hakutakuwa na kutoa asilimia 100 kwa mtu mmoja.
Amesema wageni wataangaliwa katika kazi ambazo wazawa hawaziwezi au hawana mitaji ya kufanya.
Mgombea huyo amesema fedha za ujenzi wa miundombinu zinazotoka zinapaswa zisimamiwe vizuri na katika utawala wake atahakikisha analipa madeni yote ya makandarasi yatakayoachwa na mtangulizi wake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TLP, Richard Lyimo amesema wastaafu wanaidai Serikali, hivyo chama hicho kitakapoingia madarakani watahakikisha wanayalipa madeni yao yote.

“Serikali inadaiwa na wastaafu hawalipwi, wakiwamo askari wa akiba ambao waliambiwa wafungue hadi akaunti lakini mpaka leo hawajalipwa, hivyo tukiingia madarakani hayo yote yatashughulikiwa walipwe kwa sababu wameshafanya kazi na imeshakamilika,” amesema.
Amesema chama hicho kitaimarisha uhuru wa kutumia rasilimali, kwa kuwa na kiwanda kila wilaya ambacho watakitafutia masoko ndani na nje ya nchi, huku wakidhibiti ufujaji wa rasilimali za nchi ili kila mmoja anufaike nazo.
Lyimo amesema vijana wa bodaboda na bajaji watawahakikishia vyombo hivyo vya moto vinakuwa si vya mkataba.
Amesema pia kuna haja ya fedha za mkopo kutoka nje kusaidia Watanzania ikiwamo kuwawezesha kupata milo mitatu kwa siku.
Mgombea mwenza wa urais, Amana Suleiman Mzee, amewataka wananchi kutosusia kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu OKtoba 29, 2025.
Amesema chama hicho kimejiandaa kufanya kampeni za kistaarabu zisizo za matusi.
Akiizungumzia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), amesema imefanya kazi vizuri ndiyo maana katika chama hicho wameteuliwa madiwani na wabunge kushiriki uchaguzi, hivyo kazi ya wananchi ni kuwachagua.