Tumaini jipya teknolojia ikifanikiwa kutafsiri mawazo ya binadamu

Dar es Salaam. Wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani, wamefanikiwa kutafsiri mawazo ya binadamu kwa kutumia teknolojia ya kipandikizi cha ubongo kinachounganishwa na akili unde (AI).

Teknolojia hiyo inayojulikana kama Brain-Computer Interface (BCI), imeibua tumaini kwa wagonjwa waliopoteza uwezo wa kuzungumza kutokana na ulemavu wa kimwili au ugonjwa wa mishipa ya fahamu.

Uwezo wa kusoma mawazo ya mtu moja kwa moja, ambao kwa muda mrefu ulionekana kuwa jambo la kisayansi, sasa unazidi kuwa halisi, na unaweza kubadilisha maisha ya watu wengi.

Teknolojia hii inatajwa kuwa mapinduzi katika sekta ya afya, ikitoa fursa mpya kwa watu wasio na uwezo wa kuzungumza. Kwa kutumia kipandikizi cha ‘microelectrodes’ kilichowekwa katika sehemu ya ubongo inayoitwa motor cortex.

Watafiti wameweza kusoma mawimbi ya ubongo na kuyageuza kuwa maneno, jambo ambalo limekuwa ndoto kwa wengi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa Agosti 21, 2025 kwenye jarida la kisayansi Cell, watafiti walipandikiza microelectrodes katika sehemu ya ubongo inayoitwa motor cortex, ambayo inahusiana moja kwa moja na uwezo wa binadamu kuzungumza.

Wagonjwa wanne waliokuwa wamepooza kutokana na kiharusi na ugonjwa wa mishipa ya fahamu (ALS) walishiriki katika utafiti huo.

Watafiti walimuomba kila mshiriki kufikiria kusema maneno au sentensi fulani. Microelectrodes zilizopandikizwa zilirekodi mawimbi ya ubongo, na kisha mifumo ya AI ikaivunja mawimbi hayo kuwa lugha na kutengeneza maneno na sentensi.

Kwa mara ya kwanza, sentensi ambazo hazijasemwa kwa sauti zilitafsiriwa kwa kiwango cha usahihi cha asilimia 74 kwa wakati halisi, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa kabla.

Profesa Frank Willett, mtaalamu wa upasuaji wa neva kutoka Stanford, amesema teknolojia hii inaweza kuwa suluhisho la baadaye kwa watu wasio na uwezo wa kuzungumza.

“Iwapo vifaa na programu vitaboreshwa zaidi, tunaweza kurejesha uwezo wa kuzungumza kwa haraka, kwa urahisi na kwa faraja kupitia mawazo pekee,” amesema Willett aliponukuliwa na Financial Times.

Faragha ya mawazo na haki za binadamu

Hata hivyo, mafanikio haya yamefungua mjadala kuhusu faragha ya mawazo na haki ya binadamu kulinda akili yake isije ikasomwa bila ridhaa.

Licha ya mafanikio hayo, watafiti waligundua changamoto ambapo kipandikizi kilinasa mawazo ambayo washiriki hawakutakiwa kuyawaza. Hali hiyo ilizua hofu kwamba mawazo ya mtu binafsi yanaweza kuvuja pasipo ridhaa yake.

Profesa Nita Farahany, mtaalamu wa sheria na falsafa kutoka Chuo Kikuu cha Duke, Marekani, amesema “Tunapozidi kusukuma mbele tafiti hizi, ndivyo akili zetu zinavyokuwa wazi zaidi. Hii ni enzi mpya ya uwazi wa ubongo ambayo inatulazimisha kujiuliza, je, tunalindaje haki ya mtu kufikiri bila kudukuliwa.”

Hofu hii imeibua mjadala kuhusu neurorights, haki mpya za kulinda maisha ya kiakili dhidi ya uvamizi wa teknolojia. 

Pamoja na mafanikio haya, wanasayansi wanasema bado yapo mapungufu. Lugha inayoweza kutambuliwa na teknolojia hii ni ndogo, usahihi bado si wa juu kila wakati, na vipandikizi vinahitaji mafunzo marefu kwa watumiaji. Aidha, upandikizaji wa microelectrodes ubongoni ni uvamizi mkubwa (invasive) unaohitaji upasuaji maalumu.

Kwa sasa, teknolojia hiyo inachukuliwa kama uthibitisho wa dhana (proof of concept) na huenda ikachukua miaka kadhaa kabla ya kufikia matumizi ya kawaida hospitalini.