Senegal. Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika, (African Food System Forum 2025) umeendelea leo ijini Dakar Senegal ambapo ujumbe wa Tanzania umekutana na wawekezaji ambao walihitaji kuzisikia fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta kama madini, kilimo, utalii, uvuvi na ufugaji na maeneo mengine ya kibiashara.
Akizungumza leo Alhamisi Septemba 4, 2025, Meneja Mtafiti kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Anna Lyimo amewaambia wawekezaji hao kuwa kwa sasa Tanzania inafanya vizuri na Serikali imeondoa vikwazo vyote vinavyokwamisha uwekezaji wenye tija nchini.
Amesema kuna kituo cha utaratibu wa huduma kwa pamoja yaani (One Stop Center) inayomwezesha mwekezaji anaweza kufanya taratibu zote sehemu moja, kuanzia masuala ya uhamiaji, leseni, maswala ya kikodi, ajira.
Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na jopo la wawasilishaji waliokutana na wawekezaji liliongozwa na Waziri Mkuu mstaafu na mshauri wa Rais masuala ya kilimo, Mizengo Pinda, Katibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, na Dk Stephen Nindi ambaye ni Naibu Katibu wa Wizara ya Kilimo. Naibu Katibu wa Wizara ya Kilimo, Nindi amewaelezea wawekezaji miradi mbalimbali ya kilimo hasa mradi wa vijana wa Build Better Tomorrow (BBT) ambao unagusa vijana na tayari umeanza kuonyesha matunda.
Mkutano huo wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula (AFSF2025) ulioanza Agosti 31, unatarajiwa kuhitimishwa kesho Ijumaa na umewakutanisha watu zaidi ya 6,000 wakiwemo wakuu wa nchi mbalimbali, mawaziri, wafanyabishara wakubwa, wawekezaji na mashirika makubwa duniani.