Ulaji maini kupita kiasi watajwa hatari kwa mjamzito

Geita. Maini ni miongoni mwa vyakula vinavyosifika kwa kuwa na virutubisho vingi muhimu, ikiwemo chuma, protini na vitamini A.

Hata hivyo, kwa mama mjamzito, ulaji wa maini kupita kiasi unaweza kusababisha madhara makubwa kwa mtoto tumboni.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), vitamini A aina ya retinol ikizidi mwilini hasa wakati wa ujauzito, huongeza hatari ya kasoro za kimaumbile kwa mtoto.

Madhara hayo ni pamoja na matatizo ya moyo, macho, ini, mfumo wa neva na hata ulemavu wa viungo.

Wataalamu wa afya wanashauri wanawake wajawazito wasitumie zaidi ya vitamini A 10,000 IU kwa siku.

Pia, inaelezwa maini ya ng’ombe na kondoo yanatajwa kuwa na kiwango kikubwa cha vitamini A ikilinganishwa na nyama nyingine.

Daktari bingwa wa. magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Waja Ernest Selestine .



Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi katika Hospitali ya Waja iliyopo Manispaa ya Geita, Dk Ernest Selestine anasema ulaji mwingi wa maini unaweza kuathiri ukuaji wa mtoto ndani ya wiki nne za mwanzo za ujauzito.

“Vitamini A aina ya retinol ikipita 15,000 IU kwa siku, huongeza hatari ya kuathiri mfumo wa uti wa mgongo, moyo, ini na macho ya mtoto,” anasema Dk Selestine.

Anasema changamoto kubwa ipo kwenye elimu duni ya lishe miongoni mwa wajawazito mijini na vijijini.

 “Wengi huambiwa wale maini kwa sababu yana chuma, bila kujua kuwa vitamini A ikizidi ni hatari. Tunashauri pia watumie vyanzo vingine vya chuma kama mboga za majani, maharage na vidonge vya kuongeza damu vinavyotolewa kliniki.”

Tahadhari muhimu kwa wajawazito

Wataalamu wanashauri wajawazito kuepuka vyakula vyenye vitamini A nyingi kupita kiasi hasa katika miezi mitatu ya kwanza, kipindi ambacho viungo muhimu vya mtoto vinakua.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Rufaa ya Geita, Isaack Ajee, anasema maini yana vitamini A aina ya ‘retinol’ ambayo hufyonzwa haraka na mwili ukilinganisha na ile ya mimea.

Anasema maini ni chanzo kikubwa cha retinol, lakini ukizidi husababisha ukuaji ulinganifu hivyo kushauri endapo mjamzito akihitaji kula maini, ni vema asizidishe mara mbili kwa wiki na ahakikishe yameandaliwa na kuiva vizuri.”

Dk Selestine anasema ingawa miongozo ya afya Tanzania na WHO inasisitiza utolewaji wa elimu ya lishe kwa wajawazito, bado changamoto ni nyingi.

“Elimu mara nyingi haitolewi kwa kila mjamzito kutokana na uhaba wa watumishi na wingi wa wajawazito wanaofika kliniki, lakini mila, tamaduni na uchumi duni pia huchangia lishe duni.”

Anashauri Serikali, taasisi binafsi na jamii kushirikiana kuelimisha wajawazito na kuunda makundi ya elimu ya lishe kwenye maeneo yao ili elimu hiyo iweze kuwafikia wengi.

Kwa mujibu wa utafiti wa Tanzania Demoghraphic Suvey (TDHS) ya mwaka 2015/16 idadi ya kina mama wanaohudhuria kliniki imeongezeka hadi kufikia asilimia 98 ya wajawazito wanaohudhuria angalau mara moja.

Kiwango cha mahudhurio yanayopendekezwa ya mara nne kwa kipindi chote cha ujauzito yameongezeka kutoka asilimia 48 mwaka 2015/16 hadi kufikia asilimia 65 mwaka 2022.