KOCHA wa KMC, Márcio Máximo amesema ushindi wa mabao 3-2 walioupata dhidi ya Mlandege katika mechi yao ya kwanza wa mashindano ya Cecafa Kagame ni sehemu ya mchakato wa kukijenga zaidi kikosi hicho.
Máximo alieleza alifurahishwa na nidhamu ya wachezaji wake kwa dakika 80 za mwanzo, lakini alikiri dakika 10 za mwisho walipoteza umakini na kuruhusu wapinzani kurejea kwenye mchezo kwa mabao mawili ambayo walifungwa ndani ya dakika mbili.
“Kwa dakika 80 za mwanzo tulicheza vizuri, tulidhibiti mchezo na kuonyesha mbinu tulizopanga. Lakini katika dakika 10 za mwisho tulipoteza umakini na tukaruhusu mabao mawili. Hili ni somo kubwa kwa wachezaji wangu,” alisema kocha huyo raia wa Brazil.
Máximo aliongeza, bado anaendelea kuwatengeneza wachezaji wake wapya na kurekebisha maeneo yenye mapungufu. Kwa mtazamo wake, mechi dhidi ya Mlandege imekuwa kipimo kizuri kuelewa changamoto zinazohitaji marekebisho kabla ya kuanza kwa msimu.
“Tuna wachezaji wengi wapya ambao bado wanajifunza mbinu zetu. Mechi hizi za Kagame ni maandalizi mazuri, zinatupa nafasi ya kuona udhaifu wetu na kuyarekebisha mapema kabla ya ligi kuanza,” aliongeza.
Kocha huyo aliwapongeza wapinzani wao Mlandege kwa upinzani waliouonyesha, hasa katika dakika za mwisho walipofanikiwa kupunguza tofauti ya mabao.
Hata hivyo, alisema matokeo hayo yanaonyesha wazi KMC inaweza kufanya vizuri zaidi iwapo itaongeza umakini na nidhamu ya kiufundi kwa dakika zote 90.
“Mpira wa miguu unahitaji umakini wa kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho. Tumetangulia kwa mabao matatu, lakini kuruhusu mabao mawili ya haraka dakika chache, ni jambo ambalo haliwezi kukubalika. Ni lazima tujifunze kutokana na hili,” alisema Máximo.
Mabao ya KMC katika mechi hiyo yalifungwa na Juma Sagwe dakika ya 19, Rashid Chambo dakika ya 48 na Abdallah Said ‘Lanso’ dakika ya 87, mabao ya Mlandege yalifungwa na Abed Ama dakika 89 na Aimar Hafidh dakika ya 90.