UVCCM CHATO WATAKA WANASHERIA KUKEMEA UPOTOSHAJI DHIDI YA RAIS SAMIA

Wa pili kutoka kulia ni mwanasheria wa UVCCM wilaya ya Chato, Yohana Misungwi,akitoa tamko kwa niaba ya Jumuia hiyo.

……….

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Chato mkoani Geita umewataka wanasheria na wazee wastaafu wa Chama hicho kujitokeza hadharani kukemea upotoshwaji mkubwa unaofanywa na baadhi ya wanachama wa Chama hicho wanaodai kukiukwa kanuni za uteuzi wa mgombea urais kupitia CCM.

Mbali na hao, UVCCM ngazi zote wanapaswa kusimama kidete kuwatetea wagombea wote waliopitishwa katika kinyang’anyiro cha uteuzi ndani ya CCM mwaka 2025 kuanzia ngazi ya Udiwani, Ubunge na nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hayo yameelezwa katika tamko rasmi la UVCCM wilaya ya Chato, na mwanasheria wa Jumuia hiyo, Yohana Misungwi, mbele ya waandishi wa habari katika Ofsini ya CCM kata ya Chato, huku wakitumia fursa hiyo kuwaonya wana CCM ambao wameibuka hivi karibuni kukibagaza chama hicho kutokana na maslahi yao binafsi.

Wamesema utaratibu wa kumpata mgombea wa Urais kupitia Chama hicho ulizingatia Kanuni na Utamaduni wa CCM uliozoeleka tangu enzi za Hayati Rais Ally Hassan Mwinyi, kwa kila baada ya miaka mitano ya awamu ya rais aliyepo madarakani kupewa heshima ya kugombea awamu ya pili pasipo kupingwa na wagombea wengine.

Huku wakinukuu kifungu cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 40(4) kinachohalalisha iwapo makamu wa Rais akiapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda usiopungua miaka 3 atahesabiwa kuwa ameongoza awamu moja na atakuwa na haki ya kugombea awamu ya pili.

Na kwamba kutokana na kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kufariki I mwaka 2021 ilitoa uhalali kwa Rais Samia kuhesabiwa kuwa ni rais wa awamu ya sita na kwamba anayo haki kikatiba kuendelea kugombea mhula wa pili.

Kadhalika wamewakosoa vikali wanaodai Rais Samia kupuuza ushauri wao kwa madai kuwa hilo siyo takwa la lazima kama Ibara ya 37(1) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo haimlazimishi Rais kupokea ushauri wa mtu yoyote ispokuwa kwa masharti yaliyowekwa na Katiba pekee.

Vile vile wamesema hakuna kipengere chochote cha Sheria kinachomzuia makamu wa Rais wala Waziri mkuu kugombea nafasi ya Rais wa JMT iwapo akiwa haendelei na wadhifa huo, kama baadhi ya wanachama wanavyopotosha Umma.

Kutokana na hali hiyo wamewataka wapotoshaji hao kuacha wivu na kumchafua mgombea urais kupitia CCM na kwamba ni muda wa wanachama wote kuungana na kushawishi watanzania kumpigia kura nyingi ili aweze kuibuka kidedea na kuendeleza mipango madhubuti ya kuwatumikia wananchi kwa awamu nyingine ya miaka mitano.

Katika taarifa hiyo pia wamemkubushia mgombea urais wa CCM ambaye pia ni Rais wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuipandisha hadhi wilaya ya Chato na kuipatia heshima ya makao makuu ya mkoa mpya unaotazamiwa kwa muda mrefu kwa kuwa ni hitaji muhimu la wananchi wa wilaya hiyo pamoja na wilaya jirani ambazo mara kwa mara zimekuwa zikisubiri tamko rasmi ya serikali kwa lengo la kusogeza karibu huduma za kiserikali na kijamii.

                      Mwisho.