Dar es Salaam. Wadau kutoka sekta mbalimbali katika ukanda wa Afrika Mashariki wameungana kuanzisha juhudi za pamoja za kukabiliana na uvuvi haramu, ambao unaendelea kuwa tishio kwa rasilimali za bahari, mazingira na maisha ya mamilioni ya watu wanaotegemea uvuvi kwa ajili ya kipato na lishe.
Hayo yamebainika katika kongamano la Sauti za Buluu lililofanyika hivi karibuni, likihusisha washiriki kutoka nchi wanachama wa ukanda huo.
Washiriki walikubaliana kuwa uvuvi haramu hauathiri tu wavuvi binafsi, bali pia una madhara makubwa kwa usalama wa chakula, bioanuwai ya baharini na uchumi wa eneo hili linalotegemea sana shughuli za uvuvi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa katika kongamano hilo, ukanda wa Afrika Mashariki unapoteza zaidi ya Dola za Marekani 415 milioni kila mwaka kutokana na uvuvi haramu.
Hasara hiyo inaathiri moja kwa moja maisha ya zaidi ya watu milioni tatu wanaotegemea rasilimali za baharini kwa mahitaji yao ya kila siku.
Wadau hao walisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa njia ya vitendo, ikiwemo kubadilishana taarifa, teknolojia na uzoefu, pamoja na kuendeleza kampeni za uelimishaji wa jamii kuhusu madhara ya uvuvi haramu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Msemaji wa Mradi wa Jahazi, Michael Mallya alisema mshikamano wa kweli wa kikanda ndio msingi wa suluhisho la kudumu dhidi ya uvuvi haramu.
“Tunahitaji ushirikiano wa kweli, sio wa maandishi tu, bali wa vitendo unaojengwa juu ya misingi ya uwazi, teknolojia na sheria. Ni kwa njia hiyo pekee tutaweza kulinda rasilimali zetu za baharini kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Ukanda huu wa Afrika Mashariki una moja ya ikolojia tajiri zaidi duniani, lakini vitendo vya uvuvi haramu vinaendelea kupunguza idadi ya samaki, kuharibu makazi ya viumbe na kuhatarisha usalama wa chakula. Suluhisho lazima liwe la pamoja,” alisema Mallya.
Kwa upande wake, Dk Baraka Sekadende kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tanzania, alisema kuwa Serikali ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na uvuvi wa baruti, lakini changamoto ya rasilimali bado ni kubwa.
“Tulikuwa tukishuhudia milipuko 20 hadi 30 kwa siku, lakini sasa hali hiyo imedhibitiwa kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, bado tunahitaji usaidizi wa kikanda ili kuimarisha juhudi hizi,” alisema Dk Sekadende.
Dk Matthew Silas kutoka Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA), alieleza kuwa Tanzania tayari imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Port State Measures (PSMA) unaolenga kuzuia meli zinazojihusisha na uvuvi haramu kutumia bandari za nchi wanachama.
“Tunatumia teknolojia kama VMS, AIS na picha za satelaiti kufuatilia vyombo vya uvuvi. Ushirikiano wa kimataifa ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote,” alisema Dk Silas.
Kwa upande wake Lydia Mgimo kutoka shirika la Sea Sense alionya kuhusu athari za kijamii zinazotokana na uvuvi haramu, ikiwa ni pamoja na familia kusambaratika na watoto kuacha shule kutokana na kushuka kwa kipato cha familia.
“Ukiharibu chanzo cha chakula, unahatarisha maisha ya jamii nzima. Tunahitaji kuwekeza zaidi katika elimu na uhamasishaji wa jamii za pwani,” alisema Mgimo.
Kongamano hilo limetoa mwanga kuhusu umuhimu wa juhudi za pamoja, ambapo wadau wameazimia kuendeleza mashirikiano ya kieneo na kimataifa, ili kulinda na kuhifadhi rasilimali za baharini kwa vizazi vya sasa na vijavyo.