Wadau wa kilimo, mashirika ya kimataifa wakutana katika warsha, wajadiliana Dar

Wadau wa sekta ya kilimo kutoka Serikali ya Tanzania, Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), pamoja na wadau wengine kama benki, taasisi za kibiashara, TANTRED na wazalishaji wa viuatilifu wamekutana katika warsha ya Mradi wa Kuimarisha Huduma za Afya ya Mimea na Usalama wa Chakula (STREPHIT) jijini Dar es Salaam tarehe 2 Septemba 2025. 

Lengo la kikao hicho ni kujadili namna ya kuimarisha mifumo ya afya ya mimea ili kukuza usalama wa chakula na biashara endelevu ya mazao ya kilimo.

Akizungumza katika ufunguzi wa warhsa hiyo, Mkurugenzi wa Kilimo kutoka Zanzibar,  Mohamed Dhamir amesema mradi huo umefanikisha mambo makubwa ikiwemo kutungwa kwa kanuni mpya za afya ya mimea.

Pia, kuanzishwa mifumo ya kidijitali ya ukaguzi na ufuatiliaji, ukarabati wa maabara na maabara ndogo mipakani, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa kama ndege nyuki (drone) na portable DNA sequencer.                                                                       

Ameongeza kuwa kama nchi bado tunakabiliwa na changamoto za uhaba wa fedha za kugharamia mifumo ya muda mrefu, uendelevu wa uchunguzi wa magonjwa ya mimea, ushawishi mdogo wa matumizi ya viuatilifu asilia (biopesticides) na changamoto za uchafuzi wa mazingira. Aidha, alisema warsha hiyo inalenga kutafuta mikakati na mapendekezo ya kisera yatakayohakikisha mafanikio yaliyopatikana yanaendelezwa hata baada ya mradi kukamilika.

Msimamizi wa Programu kutoka Umoja wa Ulaya, Silvia Giner Salvia, amesema Umoja wa Ulaya unaona STREPHIT kama nguzo muhimu ya mageuzi ya kilimo nchini Tanzania.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya mradi si ya kitaalamu pekee bali pia ni uwekezaji wa kimkakati katika usalama wa chakula, maendeleo ya vijijini na ukuaji wa uchumi. Aliahidi kuwa EU itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mifumo ya kidijitali, uvumbuzi wa kiteknolojia na kuimarisha uwezo wa taasisi.
                                                                                                              Mwakilishi Mkazi wa FAO nchini Tanzania, Dk Nyabenyi Tipo amesema mafanikio ya STREPHIT lazima yawekwe kwenye mifumo ya kitaasisi ili yadumu na kuleta manufaa kwa wakulima, wafanyabiashara na sekta binafsi. 

Amesisitiza kuwa kazi hii si ya kiufundi pekee bali ni jitihada za pamoja kuhakikisha wakulima wadogo wanapata masoko salama na yenye faida, huku Tanzania ikijiimarisha zaidi katika ushindani wa masoko ya kimataifa ya kilimo.