Wajasiliamali wachangamkia fursa mkutano wa Samia Mbeya

Mbeya. Wananchi na makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya wamejitokeza kwa wingi kuhudhuria mkutano wa mgombea urais wa Chama hicho, Samia Suluhu Hassan.

Mgombea huyo ambaye pia ni Rais wa sasa, anatarajia kufanya mikutano minne mkoani hapa baada ya kumaliza ziara yake mkoani Songwe jana Septemba 3, 2025.

Kiongozi huyo akiwa mkoani hapa ataanza na mkutano mdogo katika mji wa Mbalizi, kisha mkutano mkubwa viwanja vya Old Airport kwa siku ya leo.

Ziara ya mgombea huyo inatarajia kuendelea kesho Septemba 5, 2025 kwa mkutano mdogo mji wa Tukuyu kisha kuhitimisha wilayani Mbarali kwa mkutano mkubwa wa kampeni.


Hadi sasa wananchi wameonekana kujitokeza kwa wingi huku makundi mbalimbali yakimsubiri kiongozi huyo.

Wajasiliamali nao ni sehemu ya wananchi waliofika viwanjani hapo wakiwa na bidhaa zao kwa ajili ya kupata chochote kwa maisha yao.

Kuhusu ulinzi na usalama, Jeshi la Polisi limeonekana kuwa imara huku ukaguzi kwa wanaoingia getini nao ukiendelea kuhakikisha kila mmoja anashiriki na kumaliza salama tukio hilo.

Endelea kufuatilia Mwananchi Digital kwa habari zaidi.