Dar es Salaam. Timu ya wanafunzi sita kutoka vyuo vikuu vitatu vya Tanzania imeshinda mashindano ya kimataifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), ikiibuka kidedea dhidi ya timu 167 kutoka nchi 48 duniani.
Wanafunzi hao waliowakilisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), walitangazwa kuwa washindi wakuu wa Huawei Global ICT Competition ya mwaka 2024/25.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Huawei Technologies yalijikita zaidi katika matumizi ya kivitendo ya akili bandia (AI) na mifumo ya mitandao.
Ushindi huo ulitangazwa rasmi leo Septemba 4, 2025 katika hafla ya kila mwaka ya Huawei Tanzania ICT Talent.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Dk Florence Rashid kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ameipongeza timu hiyo, ambayo ilihusisha wanafunzi watatu walioshiriki katika kitengo cha cloud computing na watatu katika kitengo cha mitandao.
“Wanafunzi wetu katika taasisi za elimu ya juu wanaonesha uelewa mzuri wa dhana za ICT na ujuzi wa kivitendo,” amesema Dk Rashid.
“Mashindano haya yalikuwa ya kivitendo zaidi, na kushinda kwake kunathibitisha kwamba Tanzania inapiga hatua kubwa katika teknolojia na elimu ya ICT.
Aliwahimiza wanafunzi wengi zaidi nchini kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa kama haya ili kupata uzoefu na fursa za ajira.
“Tunawahimiza wanafunzi kufanya kazi kwa bidii na kushiriki kwenye mashindano kama haya. Yanaleta sio tu uzoefu wa kimataifa, bali pia kufungua milango ya fursa za baadaye katika sekta ya teknolojia,” aliongeza.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu amesema ushindi huo umetuma ujumbe mzito kuhusu uwezo unaokua wa nchi katika ICT.
“Ushindi huu unathibitisha kwamba Tanzania haishiriki tu, bali inafanya vizuri kwenye majukwaa ya kimataifa ya ICT,” amesema Dk Nungu.
“Kwa kuboreshwa kwa miundombinu katika taasisi zetu, tunaona matokeo ya kutia moyo.”
Amesema serikali inayo dhamira ya serikali ikuendelea kuwaunga mkono wavumbuzi na wanafunzi wanaotengeneza teknolojia zinazoshughulikia changamoto halisi za kijamii.
“Tunawahimiza wanafunzi kushiriki kila mara nafasi hizi zinapojitokeza. Kama serikali, tutaendelea kuwaunga mkono wanaotumia teknolojia kutatua matatizo ya jamii,” amesema.
Mashindano ya Huawei ICT ni miongoni mwa mashindano makubwa zaidi duniani ya teknolojia kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, yakiwa na lengo la kutambua na kukuza vipaji vya ICT pamoja na kuhamasisha ushirikiano na ubunifu wa kimataifa.
Ushindi wa Tanzania ni hatua kubwa katika safari ya nchi kuelekea kuwa mshindani wa kweli kwenye anga la teknolojia duniani.
Mmoja wa wanafunzi walioshinda, Sigfrid Michael ameeleza kwamba mashindano hayo yalikuwa na changamoto kubwa, hasa kutokana na msisitizo wake katika ujuzi wa vitendo huku akibainisha kuwa mafunzo ya kivitendo waliyopewa vyuoni kwao yaliwaandaa ipasavyo.
“Mashindano yalikuwa magumu na ya kivitendo, lakini hayakuwa magumu sana kwetu kwa sababu vyuo vyetu vinatilia mkazo zaidi mafunzo ya vitendo,” amesema.
“Tumejifunza mambo mengi kupitia uzoefu huu. Funzo kuu tulilolipata ni umuhimu wa kujikita kwenye eneo maalumu. Kwa mfano, kama ni mitandao, bakia kwenye mitandao.
Amesema moja ya kitu alichojifunza ni namna China inayovyowaandaa wanafunzi wake kuwa wabobevu katika eneo moja badala ya kufundishwa vitu vingi.
“Sisi hapa mara nyingi tunajifunza kila kitu kidogo kidogo, jambo linalotufanya tushindwe kuwa wataalamu wa kweli,” amesema.