Warundi kunogesha Mashujaa Day Jumapili

KIKOSI cha Mashujaa FC kinatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Vital’O FC Septemba 7 mwaka huu maalum kwa ajili ya kutambulisha kikosi chao cha msimu wa 2025/26.

Kocha Mkuu wa Mashujaa, Salum Mayanga ameupongeza uongozi wa timu hiyo kuandaa mchezo huo ambao amesema kuwa ni kipimo sahihi kwao kabla ya kuanza kwa msimu mpya ambao wanatarajia kuikaribisha JKT Tanzania katika mchezo wa kwanza wa ligi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mayanga alisema ni kweli wametaarifiwa kuwa watacheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa na wao wanaendelea kujiweka tayari kwani wanaamini mchezo huo utatoa picha ya kikosi chao msimu huu.

“Mashabiki wa Mashujaa tukio hili ni kubwa na ni la kwanza kufanyika hivyo naomba mjitokeze kwa wingi kuishuhudia timu yenu bora msimu huu ambayo naamini itakuwa timu shindani kutokana na mandalizi na pia ubora wa mchezaji mmoja mmoja,” alisema na kuongeza;

“Nina kikosi kizuri na timu ambayo tumeipata kwa ajili ya mchezo wa kirafiki ni nzuri itatupa kipimo sahihi kuelekea msimu mpya wa ligi ambao matarajio utakuwa mzuri na wa ushindani kutokana na usajili uliofanyika.”

Akizungumzia maandalizi kwa ujumla, Mayanga alisema wao kama Mashujaa wanaendelea vizuri na wapo tayari kukabiliana na timu yoyote kutokana na kujiimarisha kila eneo.

“Huo hautakuwa mchezo wetu wa kwanza tayari tumecheza mechi nyingi za kirafiki na tumebaini upungufu na ubora wetu lakini kuelekea mchezo huo naamini wachezaji wangu wataonyesha ubora wao na kuwapa imani mashabiki wao ambao ndio watakaokuwa wanawapa nguvu kwenye mechi za ligi msimu huu.”

Baadhi ya mechi za kirafiki walizocheza hadi sasa ni dhidi ya Fountain Gate wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 na Al Hilal na Singida Black Stars ambazo walitoka suluhu.