Dar es Salaam. Uwekezaji katika mifuko ya uwekezaji ya taasisi ya Serikali inayosimamia na kuendeleza mifuko ya uwekezaji wa pamoja UTT Amis umetajwa kuwa bora, hakika na salama zaidi huku ukiwa na utajiri wa faida ya mtaji.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi ya Septemba 4, 2025 wakati wa mjadala wa Mwananchi Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Limited wenye mada; Uelewa wa uwekezaji: Nafasi ya UTT AMIS katika kukuza mitaji.
Mjadala huo umekuja baada ya Serikali kubaini ongezeko la uhitaji miongoni mwa Watanzania wa kuwa na utamaduni wa kuweka akiba, ambapo wengi wao bado wanatumia njia za asili kama vile vibubu wakati zipo njia bora zaidi ya kuwekeza.
Hali hiyo imeifanya Serikali kuanzisha na kusimamia mifuko ya uwekezaji wa pamoja, kupitia taasisi hiyo ambayo hadi sasa kuna mifumo sita ya uwekewzaji ili kuwawezesha wananchi kuwekeza kwa njia salama, yenye tija na faida ya muda mrefu.
Ofisa Mwekezaji kutoka UTT Amis, Abdulwahab Mwalim amewahamasisha Watanzania kujifunza kuhusu fursa zilizopo katika mifuko hiyo kwa kuwa kuna faida pia inawahusisha makundi yote kuanzia watoto, vijana na wazee.
“Ukiwekeza Sh10, 000 kwenye kibubu huipi thamani kwa sababu ukija baada ya miaka kumi itakuwa ni hiyo hiyo. Pesa hiyo ukiiwekeza japokuwa unaona ni ndogo ukiwekeza katika mifuko ya UTT itazaa maana yake utaipa thamani,” amesema.
Amewahamasisha Watanzania kupata kwanza elimu ya uwekezaji kisha kuanza kuwekeza ili kuipa pesa thamani. Amesema UTT ni jukwaa linalompa mtu uhuru wa kuwekeza na kupata faida bila kuhitaji kujihusisha moja kwa moja na shughuli za kila siku.
Uwekezaji huo humwezesha mwekezaji kuwa na uhuru wa kifedha, ambapo fedha zake zinaendelea kuzalisha mapato hata akiwa nyumbani.
Ufafanuzi huo umetolewa na Mwalim, kwamba UTT Amis ni sehemu inayompa mtu uhuru wa kuwekeza na kuendelea kupata fedha pasipo kujishughulisha.
Kuhusu ofisi za UTT Amis, amesema zipo maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Dar es Salaam, Zanzibar, Kahama (Shinyanga), Morogoro, Mbeya na katika maeneo ambayo hawana ofisi, wawekezaji wanaweza kuwapata kupitia Benki ya CRDB kama wakala wa UTT Amis.
Pia, amesema wanapatikana katika mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na kwa simu ya ofisi kupitia namba 0800112020.
Ofisa Uendeshaji na Maendeleo ya Biashara wa UTT Amis, Esther Kahabi amesema hadi sasa taasisi hiyo inasimamia mifuko sita ya uwekezaji wa pamoja yenye malengo mbalimbali, ikiwemo kukuza thamani ya fedha za wawekezaji, kuongeza mitaji na kutoa gawio kwa wanachama wake.
Ameitaja mifuko hiyo kuwa ni Umoja, Wekeza Maisha, Watoto, Kujikimu, Bond, na Ukwasi ambayo uwekezaji wake unakwenda hadi kwenye uwekezaji wa hisa.
“Mwananchi hauna sababu ya kuweka fedha zako ndani ambapo hazikui, unaweza kuwekeza kwenye mifuko hiyo ili kuipa thamani, kupata na faida na magawio,” amesema.
Esther amesema uwekezaji kwenye UTT Amis hauna milolongo mirefu kama inavyohofiwa, ni rahisi na nyaraka zinazotakiwa hazina ugumu kuzipata huku akitoa ufafanuzi wa taratibu zinazotakiwa kufuatwa na makundi mbalimbali yanayotaka kuwekeza.
Kahabi amefafanua kwamba mtoto anahitaji cheti cha kuzaliwa, kitambulisho, huku kwa upande wa kikundi, wanahitaji cheti cha usajili wa ujasiriamali pamoja na vitambulisho vya wanachama wake.
“Mtu anapojiunga, ataweka akaunti yake kama ni kikundi au taasisi nao watawasilisha akaunti ambayo pesa zao tunaweka humo wanapohitaji kutoa pesa,” amesema.
Amefafanua kuwa mfuko wa Ukwasi hukamilisha mchakato ndani ya siku tatu za kazi na ndani ya siku kumi kwa mifuko mingine.
Uelewa kuhusu uwekezaji kwenye mifuko ya uwekezaji unaendelea kuongezeka siku baada ya siku, hali inayowavutia watu wengi kutaka kupata elimu hiyo na hatimaye kuwekeza ili kukuza vipato vyao.
Mtoa elimu ya kifedha aliyethibitishwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Charles Ligonja Ligonja amesema uelewa wa kuwekeza kwenye mifuko ya uwekezaji unaendelea kuongezeka siku hadi siku hali inayovutia wengi kutaka kupata elimu hiyo kisha kuwekeza kukuza vipato vyao.
Amesema yeye huwa anazungumza kwenye majukwaa namna ya maandalizi ya kustaafu ambapo ametolea mfano ikitokea mstaafu amepata Sh60 milioni anamuuliza je ajenge au awekeze.
“Wastaafu kama hawa nawapa elimu ya kuwekeza ambapo watapata fedha kila baada ya muda kisha apime mwenyewe,” amesema.
Hata hivyo, ameshukuru vyombo vya habari na mitandao ya kijamii jinsi vinavyoeneza elimu ya fedha ikiwemo uwekezaji wa pamoja.
Amesema watu wengi wamekuwa na shauku ya kutaka kujua kuhusu UTT Amis ili kuwekeza.
Aidha amesema, wawekezaji wametakiwa kuwa na subira na kuepuka tamaa ya mafanikio ya haraka, kwani ukosefu wa utulivu wa kifedha na kihisia unaweza kuathiri maamuzi yao ya uwekezaji na kuwanyima fursa ya kupata faida endelevu.
“Mtu anawekeza leo, akikaa kidogo tu anaenda anachomoa laki moja, akikaa kidogo anachomoa tena, hiyo chomoachomoa hauwezi kufanikiwa,” amesema.
Amesisitiza kuwa, mwekezaji anapaswa kujiwekea malengo ya muda mrefu na kuweka kiwango kizuri cha mtaji ili kunufaika na fedha yake.
Ligonja amesema faida zaidi itategemea na aina ya mfuko aliofungua akaunti, kiwango cha mtaji na kiwango cha faida kinachozalishwa na mfuko huo.