95 wapandikizwa mimba KCMC, daktari ataja sababu kutopata ujauzito

Moshi. Wakati wanawake 95 wamefanikiwa kupandikizwa mimba kutokana na changamoto za uzazi, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) imeeleza namna pande zote mbili – mwanamume na mwanamke – zinavyoweza kuchangia tatizo hilo.

Akizungumza na gazeti hili leo Septemba 5, 2025, Daktari Bingwa wa Uzazi na Magonjwa ya Wanawake KCMC, Dk Tom Kakumbi, amesema hospitali hiyo iliamua kuanzisha huduma za upandikizaji mimba mwaka 2018 baada ya kubaini ukubwa wa changamoto hiyo kwa wanawake wengi.

Akifafanua changamoto zinazochangia kutopata ujauzito, Dk Kakumbi amesema zinahusisha ubora na wingi wa mbegu za kiume, mirija ya uzazi kuziba kwa mwanamke, mvurugiko wa hedhi pamoja na matatizo mengine ya kiafya.

Aidha, amebainisha kuwa kwa wiki hospitali hiyo inapokea kati ya wanandoa au wagonjwa mmoja mmoja 50 hadi 60 wenye matatizo mbalimbali ya afya ya uzazi.

“Baada ya kuona tatizo hili ni kubwa, KCMC tulianza huduma za upandikizaji mimba. Tangu mwaka 2018 hadi sasa tumepandikiza zaidi ya wanawake 95. Kila wiki tunaweza kufanya upandikizaji angalau mara moja, mbili au tatu,” amesema Dk Kakumbi ambaye pia ni mbobevu wa uzazi saidizi.

Aliongeza kuwa kati ya wanawake au wanandoa 10 wanaofika kliniki, watano hadi sita hulalamika ama kushindwa kupata mtoto, au kuwa na changamoto za mvurugiko wa hedhi na mimba kuharibika mara kwa mara.

Pamoja na hilo, Dk Kakumbi ametoa tahadhari juu ya matumizi holela ya dawa za uzazi kwa wanawake, akisema yanaweza kusababisha kupoteza kabisa uwezo wa kupata ujauzito.

“Matumizi ya dawa nyingi ambazo mtu anaweza kujinunulia dukani bila cheti cha daktari, kwa kushauriwa na ndugu au rafiki, yanaweza kuathiri mfumo wa uzazi. Mfano ni P2, ambayo ni dawa maarufu sana. Ikiwa hutumii kwa kufuata vipimo na ushauri wa kitaalamu, madhara yake ni makubwa,” alisema.

Amefafanua kuwa matumizi ya muda mrefu ya P2 yanaweza kuharibu mzunguko wa homoni na kuvuruga hedhi, jambo linalomfanya mwanamke kushindwa kufahamu wakati sahihi wa kupata ujauzito.

Ameshauri wanawake kutumia njia salama na za kitaalamu za kuzuia mimba badala ya kujinunulia dawa kiholela.

Kwa upande wake, mkazi wa Moshi, Doreen Tesha, amesema changamoto ya kutopata uzazi imekuwa kubwa katika jamii na kusababisha madhara makubwa kijamii ikiwemo kuvunjika kwa ndoa.

“Tatizo la kutopata ujauzito limeongezeka sana. Wapo wanawake waliokaa kwenye ndoa zaidi ya miaka mitano bila kupata mtoto. Madhara yake ni kunyanyapaliwa, na wengine wakishindwa kuhimili masimango huishia kuondoka kwa waume zao na kurejea kwa wazazi,” alisema Doreen.