Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mtwara imemhukumu Issa Kaunda adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe Elimina Severine Januari 2, 2024, katika Kijiji cha Lukula, wilayani Nanyumbu, Mkoa wa Mtwara.
Kwa mujibu wa mashahidi sita na vielelezo vinne vilivyowasilishwa, ikiwemo ushahidi wa daktari, marehemu alipatikana na jumla ya majeraha saba ya kuchomwa shingoni, kifuani na tumboni, yakionesha kifo hakikuwa cha asili.
Katika maelezo ya awali, mshtakiwa alikiri kumuua mkewe akidai alimsema vibaya mtaani. Hata hivyo, mahakamani alijitetea kwa madai tofauti akisema alikuta akifanya mapenzi na mwanaume mwingine. Lakini, Jaji Martha Mpaze alibainisha kuwa utetezi huo ulikuwa wa kubuni, kwani mshtakiwa mwenyewe alikiri kuchukua kisu na kumchoma mkewe kutokana na hasira.
Aidha, ushahidi ulibainisha kuwa kabla ya tukio, mshtakiwa aliandika wosia na kuchukua kisu kutoka nyumbani kwake, hatua iliyoonesha nia ya makusudi ya kuua.
“Kutokana na ushahidi uliotolewa, ni dhahiri mshtakiwa alihusika moja kwa moja na mauaji haya,” alisema Jaji Mpaze, kabla ya kutoa hukumu Septemba 2, 2025. Alisisitiza kuwa ungamo la mshtakiwa mwenyewe lilitosha kuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.