Aliyeua mke akidai kusemwa vibaya mtaani, kunyongwa hadi kufa

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mtwara imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Issa Kaunda baada ya kumtia hatiani kwa mauaji ya mkewe, Elimina Severine.

Mahakama ilielezwa alimchoma visu mwilini akidai mkewe alikuwa akimzungumzia vibaya mtaani.

Katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa na maelezo ya ziada inadaiwa baada ya kumuua mkewe kutokana na hasira alikimbilia porini alipofukuzwa na watu.

Akijitetea mahakamani mshtakiwa alidai alimkuta mkewe akifanya tendo la ndoa na mwanamume mwingine na alipomhoji alimjibu kwa ujeuri, hivyo akampiga kwa gogo na kutumia kisu alichokikuta eneo hilo kumchoma.

Jamhuri ilieleza tukio hilo lilitokea Januari 2, 2024 katika Kijiji cha Lukula wilayani Nanyumbu, mkoani Mtwara nyumbani kwa kina Elimina (marehemu).

Katika maelezo ya onyo mshtakiwa alikiri kwenda kwa kina Elimina (mkewe) alikomkuta akiwa na mama yake mzazi na ndugu zake wengine wakiwa wamekaa mbele ya nyumba yao.

Baada ya salamu aliomba wazungumze na mkewe pembeni, hivyo walizunguka nyuma ya nyuma jirani na choo, huku yeye akiwa amembeba mtoto wake, Aisha Mustafa.

Katika ya mazungumzo alieleza alimuuliza mkewe kwa nini anamzungumza vibaya mtaani, akamjibu kwa ukali kuwa, alivyosikia ndivyo ilivyo.

Katika maelezo alisema alipandwa jazba akachomoa kisu na kumchoma mkewe, cha kwanza kikiwa kufuani lakini vingine hakumbuki alimchoma wapi kutokana na hasira.

Jaji Martha Mpaze aliyesikiliza kesi hiyo katika hukumu aliyoitoa Septemba 2, 2025 amesema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kosa pasipo kuacha shaka.

Jaji Mpaze amesema kwa vyovyote vile, hakuna ushahidi bora zaidi kuliko ungamo la mshtakiwa aliyekiri alimchoma kisu Elimina (marehemu).

“Kwanza, kutofautiana kati ya utetezi wake wa mdomo na ungamo lake la awali na taarifa za ziada za kimahakama kunadhoofisha dai lake katika taarifa za awali, hakutaja kushuhudia tendo lolote la ngono au tukio mahususi ambalo linaweza kusababisha uchochezi,” amesema na kuongeza:

“Alitaja tu kutukanwa. Hii inaonyesha kwamba hadithi ya uchochezi ilikuwa tu mawazo ya baadaye, iliyoundwa ili kupunguza hatia yake.”

Issa aliyekuwa akiishi na Elimina (marehemu) nyumba moja kama mke na mume alishtakiwa kwa kosa la mauaji, shtaka alilolikana.

Jamhuri ilikuwa na mashahidi sita akiwamo Joyce Yohana, mama mzazi wa Elimina aliyekuwa shahidi wa kwanza katika kesi hiyo. Pia ulikuwa na vielelezo vinne.

Jamhuri ilikuwa na jukumu la kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa, Elimina alifariki dunia, kifo chake hakikuwa cha asili, kilisababishwa na nia mbaya iliyofikiriwa mapema na mtuhumiwa ndiye aliyesababisha kifo.

Katika utetezi wake mshtakiwa alieleza: “Kutokana na maumivu na hasira niliyokuwa nayo, wakati nikipekua pembeni niliona kisu kikiwa chini, nikakiokota na kumchoma nacho. Sijui nilimchoma kisu mara ngapi wala sehemu gani ya mwili. Baada ya hapo, niliondoka tu mahali pale… naomba mahakama iniachie huru kwa sababu sikukusudia kufanya kitendo cha mauaji.”

Jaji Mpaze amesema kutokana na utetezi huo, ni dhahiri mshtakiwa alikiri kumchoma kisu Elimina, lakini alitaka kuhalalisha kitendo chake kwa kudai alifanya hivyo kwa hasira na bila nia ya kumuua.

Amesema mbali ya utetezi, pia amezingatia maelezo ya onyo ya mshtakiwa na maelezo ya ziada ya kimahakama, ambayo yote yalikubaliwa bila pingamizi.

Mpaze amesema suala la kuwa Elimina amefariki dunia limethibitishwa na shahidi wa nne ambaye ni daktari aliyechunguza mwili wake, pia mama mzazi wa marehemu aliyeeleza baada ya uchunguzi aliruhusiwa kuuzika.

Iwapo kifo chake si cha asili, jaji amesema ushahidi wa daktari uliotolewa mahakamani ulieleza baada ya uchunguzi wa mwili wa marehemu yalibainika majeraha saba ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Shahidi alitaja majeraha yalikuwa shingoni, mawili kwenye titi la kushoto, moja kifuani upande wa kulia, moja upande wa kushoto wa tumbo, majeraha mawili kwenye mapaja (kushoto na kulia) na moja mguu wa kushoto.

“Kulingana na ushuhuda huu, pamoja na kukiri kwa mshtakiwa ni dhahiri kifo hakikuwa cha asili, bali ni matokeo ya kitendo cha ukatili. Kwa hiyo, upande wa mashtaka umethibitisha kipengele cha pili cha kosa bila shaka yoyote,” amesema.

Kuhusu mshtakiwa ndiye aliyesababisha kifo hicho, amesema alikiri kumchoma kisu jambo linalothibitishwa na vielelezo viwili (maelezo ya onyo na maelezo ya ziada) na alikimbia baada ya tukio hilo.

“Kutokana na ushahidi huo, inadhihirika kuwa mshtakiwa alikuwa kwenye eneo la tukio na alihusika moja kwa moja na kitendo cha mauaji,” amesema.

Iwapo kulikuwa na nia mbaya ya mshtakiwa kutenda kosa hilo, Jaji amenukuu sehemu ya maelezo ya onyo ya Issa aliyeeleza aliazimia kumuua mkewe ili wakapate hukumu kwa Mungu na siku ya tukio akiwa nyumbani kwake alichukua karatasi na kalamu.

Alieleza kuandika wosia kuwa atamuua Elimina kisha akaiweka karatasi hiyo kwenye mfuko wa kaptula aliyokuwa amevaa. Akavaa fulana ya rangi nyekundu na kuchukua kisu chenye ncha kali kilichokuwa na mpini wa bluu na kukiweka kiunoni.

“Katika mazungumzo mimi nilimuuliza kwa nini ananiongelea vibaya mtaani? Yeye akanijibu kiukali kama nilivyosikia ndivyo hivyo, kwa kweli jazba ilipanda mara mbili ya ile niliyokuwa nayo, nikajikuta nimechomoa kisu palepale na kuanza kumchoma nacho,” amenukuliwa mshtakiwa katika maelezo yake.

Jaji amesema kutokana na sehemu ya maelezo hayo ni dhahiri mshtakiwa alihusika katika mfululizo wa hatua za makusudi na zilizohesabiwa kabla ya shambulio hilo.

“Kwanza aliandika wosia akieleza nia yake ya kumuua na sababu zake za kufanya hivyo, akionyesha mawazo na mipango. Kisha alivaa kwa kukusudia akichagua mavazi maalumu na kujihami kwa kisu, ambacho alikificha kwa uangalifu,” amesema.

Kutokana na uchambuzi huo, Jaji Mpaze alihitimisha kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.

Mahakama ikamtia hatiani mshtakiwa na kumhukumu kunyongwa hadi kufa.