Dar es Salaam/Tanga. Viongozi wa dini na Serikali wamewahimiza wananchi kudumisha amani na wajitokeze kwa wingi kupiga kura kuwachagua viongozi watakaowaletea maendeleo.
Wito huo umetolewa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali wakati wa kuadhimisha Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), huku wakiwatakapia kuepuka vitendo vya dhihaka dhidi ya viongozi.
Kwa Tanzania Bara, Baraza la Maulid limefanyika wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga mgeni rasmi akiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Pia, kwa upande wa Zanzibar, kongamano la Baraza la Maulid limefanyika katika ukumbi wa Polisi Ziwani mgeni rasmi akiwa, Dk Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar.
Rais Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuepuka siasa za chuki, mifarakano, ubaguzi na lugha za matusi, akihimiza mshikamano, amani na maadili mema katika jamii.
Majaliwa kwa upande wake, amesema katika mitandao ya kijamii kumeshuhudiwa baadhi ya Watanzania wakitoa maneno yasiyofaa kwa viongozi na wengine kuwatengenezea picha za mnato ambazo wakati mwingine hazina ukweli, kwa lengo la kuwachafua.

Amesema kitendo hicho ni kinyume na maadili ya jamii kwani nchi hiyo imejengwa kwa misingi ya maadili iliyojengwa na viongozi mbalimbali waliotangulia.
Majaliwa amesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kushirikiana na wazazi pamoja na walezi katika kuendeleza malezi na mafundisho ya maadili kwa watoto, pamoja na watu wazima, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuwajengea misingi bora ya tabia na kuwaandaa kuwa viongozi waadilifu wa baadaye.
“Hapa lengo ni kuhakikisha tunaweka misingi ya mshikamano, elimu bora na kujenga jamii ambayo itakuwa na maadili mazuri kwenye jamii, hivyo niwaombe mjenge hata vyuo vikuu vya Kiisalamu ambavyo vitaendelea kutoa vijana wazuri,” amesema Majaliwa.
Pia, Majaliwa amewasisitiza wananchi kuwa tayari kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi, kwani Serikali inaendelea kuhakikisha amani itakuwepo na wananchi wasihofu.
Pia amewaomba wananchi wajitokeze kwenye mikutano ya kampeni kwa ajili ya kusikiliza sera ambazo wanazinadi wagombea, ambazo zitawasaidia kujua ni vitu gani wagombea watakwenda kuwafanyia.
“Nendeni kwenye mikutano ya hadhara mkasikilize sera za wagombea na muweze kujua nani ataweza kuwafaa, maana wapo wengine ni wazuri katika kuongea ila kwa upande wa utendaji inawezekana wasiwe vizuri, hivyo kuhudhuria kwenu mikutano mtaweza kuwatambua,” amesema Majaliwa.
Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, akizungumza katika baraza hilo, amewataka masheikh kote nchini kusimamia kwa dhati suala la amani katika maeneo yao, akieleza kuwa amani ni msingi muhimu katika kila eneo la jamii na inapaswa kulindwa kwa bidii.
Aidha, amewasihi masheikh kutumia majukwaa yao kusisitiza umuhimu wa amani, na pale wanapobaini viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani, wachukue hatua za haraka na kukemea waziwazi, badala ya kungoja hali hiyo kuota mizizi.
“Mchukue hatua kwenye majukwaa yenu, mkiona kiashiria chochote cha uvunjifu wa amani, mchukue hatua za haraka msisubiri mpaka kuharibika, kila mmoja kwenye eneo lake ahakikishe anasimamia hilo kwa nguvu zote,” amesema Mufti Zubeir.
Pia, amewasisitiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura muda utakapowadia, akieleza kuwa kufanya hivyo ni haki yao ya msingi ya kikatiba.
Awali, akitoa salamu za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Katibu Mkuu wa baraza hilo, Nuhu Jabir Mruma, amesema hatua madhubuti zinahitajika kuchukuliwa kutokana na mmomonyoko wa maadili unaoendelea kukithiri kupitia mitandao ya kijamii.
Mruma amesema baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakitumia majukwaa hayo kuwatukana viongozi waziwazi bila kuzingatia heshima na hadhi ya wale wanaowazungumzia.
Amesisitiza kuwa Bakwata inalaani tabia hiyo kwani ni kinyume na maadili ya dini zote.
Mruma amewataka watumiaji wa mitandao kuwa waadilifu, wenye maadili mema na kuacha mara moja tabia ya kutoa lugha chafu dhidi ya viongozi au mtu yeyote yule.
“Tumeona siku za hivi karibuni kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili kwenye jamii, watu hawawatii viongozi wao waliopo madarakani, wanatoa lugha za matusi ambazo kwa mwongozo wa maadili ya dini hawatakiwi kufanya hivyo,” amesema Nuhu.
Katika baraza hilo, mwakilishi wa viongozi wa dini zote kutoka Wilaya ya Korogwe, Padri Casmil Mahimbo, amesema ushirikiano miongoni mwa viongozi wa dini ni jambo jema na linapaswa kuendelezwa.
Amesema mikutano ya pamoja kama hiyo ni kielelezo cha mshikamano wa kidini, na ni msingi muhimu wa kudumisha amani, mshikamano na maendeleo ya kijamii na kitaifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Buriani, pia amesisitiza umuhimu wa kulinda na kudumisha amani, akieleza kuwa mkoa huo uko salama hali iliyowezesha maandalizi ya shughuli ya kitaifa ya Baraza la Maulid kufanyika kwa mafanikio.
Amesema kuwa juhudi za Serikali katika kusimamia amani zimechangia kuwepo kwa mazingira bora ya shughuli za kiuchumi na kijamii, ikiwemo uhuru wa wananchi kufanya ibada zao bila bughudha yoyote. Hivyo, amewahimiza wananchi kuendelea kuilinda na kuithamini amani iliyopo.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, akihutubia kwenye kongamano la Baraza la Maulid Zanzibar Unguja, amewataka viongozi wa dini kutumia majukwaa yao kupaza sauti na kuwakumbusha wanasiasa kuwa katika kipindi cha kampeni ni muhimu kuepuka siasa za chuki, mifarakano, ubaguzi na matusi.
Amesema badala ya kueneza maneno ya uchochezi, wanasiasa wanapaswa kueleza kwa uwazi mipango na sera zao kuhusu namna watakavyowahudumia wananchi, ili kusaidia kulinda amani, mshikamano na utulivu wa nchi.
Pia, amesema jukumu la kulinda amani ya nchi si la wanasiasa pekee, bali ni la kila mmoja, wakiwemo viongozi wa dini, waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.
Dk Mwinyi amesema tayari baadhi ya wanasiasa wameanza kutoa matamshi yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi, hivyo ni wajibu wa viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kukemea kauli hizo mapema kabla hazijasababisha madhara makubwa.
“Sio vyema kunyamaza katika hili kwani kuvunjika kwa amani hakuanzi na bunduki bali kunaanza na viashiria, ikiwemo maneno na kauli za vitisho kutoka miongoni mwetu, tuendelee kufanya hivyo ili wale wanaohimizwa kutoka kwenda kuvunja amani wasikubali kufanya hivyo,” amesema.
Dk Mwinyi amesema ni wajibu wa kila mmoja kuwa mstari wa mbele kuilinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi na kujiepusha na kila kitakachovunja amani iliyopo.
Akizungumzia mada zilizowasilishwa katika kongamano hilo ikiwemo ya viashiria vya uvunjifu wa amani, amesema zinaendana na wakati uliopo wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Hivyo, amewaomba wananchi kwa umoja wao kujitahidi kuilinda amani yao kwa nguvu zote bila ya kuchoka kwani kufanya hivyo watakuwa wameihami neema hiyo aliyowaruzuku Mola wao.
“Tuzingatie kuwa tupo katika maadhimisho ya kuzaliwa Mtume (SAW) tuendelee kuonyesha mapenzi yetu kwake kwa kufuata mwenendo wake hasa wa kudumisha amani, jambo ambalo alituhimiza sana sisi wafuasi wake,” alisisitiza.
Awali, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Zanzibar, Shekh Khalid Ali Mfaume, amesema maadhimisho ya kuzaliwa Mtume ni lazima kuyaingiza katika maisha yao ya kila siku, kwani kutofanya hivyo ni kwenda kinyume na amri yake.
Amewasisitiza vijana kuacha kutumika vibaya kuvuruga amani ili kuhakikisha nchi inaendelea kubaki na tunu hiyo.
“Kila chama kinachohitaji dola ni lazima kumwaga sera na sio chuki na mifarakano ambavyo itapelekea kupotea kwa amani yetu,” amesema.
Imeandikwa na Rajabu Athumani (Tanga), Mariam Mbwana (Dar es Salaam) na Jesse Mikofu (Zanzibar)