Angalizo watumiaji mafuta ya kujikinga na miale ya jua

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya ya ngozi wametoa tahadhari kufuatia ongezeko la kasi la biashara ya bidhaa za kukinga miale ya jua, maarufu kama ‘sunscreen’, wakisisitiza kuwa kuna umuhimu wa ngozi kupata miale ya jua kwa kiwango cha kutosha kila siku.

Biashara ya bidhaa hizo imeonekana kushamiri kwenye maduka ya vipodozi na mitandaoni ambapo kumekuwa na hamasa kubwa kwa watu kuweka bidhaa hiyo kwenye mahitaji yao ya kila siku ya ngozi.

Hata hivyo, inaonekana wengi hawajui matumizi sahihi ya bidhaa hizo hivyo kuhatarisha usalama wa afya ya ngozi.

Kajlima Sefu ambaye ni mmoja wa watumiaji amesema anahakikisha wakati wate ngozi yake inakuwa na ‘sunscreen’ kwa kila alichodai anakabiliana na miale ya jua.

“Mimi naishi na kufanya kazi sehemu yenye jua kali, hivyo siwezi kuacha kutumia kila siku na wakati wote ni lazima nipake kwa ajili ya kulinda ngozi yangu,” amesema.

Mmoja wa wauzaji wa bidhaa hizo katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, Halima Juma, amesema mauzo ya ‘sunscreen’ yameongezeka mara dufu katika miaka miwili iliyopita.

“Wateja wangu wengi ni vijana, hasa wanawake, ambao wanajali sana urembo wa ngozi. Ukweli ni kwamba wengi wao hawajui tofauti ya aina za ‘sunscreen’ na jinsi ya kuzitumia wakija hapa ndiyo tunawachagulia kwa kutumia uzoefu na bidhaa tulizonazo,” amesema.

Kufuatia hilo wataalamu wamewataka wauzaji kuhakikisha wanatoa elimu sahihi kwa wateja kuhusu matumizi ya bidhaa hizo, huku wakisisitiza kuwa jamii iendelee kutambua nafasi ya miale ya jua kama sehemu ya afya bora.

Akizungumza na Mwananchi, Daktari wa ngozi Asha Mrope amesema matumizi ya ‘sunscreen’ yamekuwa yakiongezeka kwa kasi hususan mijini kutokana na uelewa unaoongezeka kuhusu madhara ya miale ya jua, ikiwemo saratani ya ngozi na mikunjo ya mapema.

Hata hivyo, ameonya kuwa tabia ya watu kujifungia ndani au kutumia bidhaa hizo bila mpangilio sahihi inaweza kuathiri afya kwa muda mrefu.

“Ni kweli ‘sunscreen’ inalinda ngozi dhidi ya miale ya UVA na UVB, lakini ngozi pia inahitaji mwanga wa jua angalau dakika 20 kwa siku ili kusaidia mwili kuzalisha vitamini D. Vitamini hii ni muhimu kwa mifupa imara, kinga ya mwili na hata afya ya akili,” amesema Dk Mrope na kuongeza.

“Jua husaidia ngozi kuwa na mwonekano mzuri, husaidia pia katika kudhibiti matatizo ya ngozi kama vile chunusi kwa kuwa huua baadhi ya vijidudu vinavyosababisha magonjwa ya ngozi. Kwa hiyo ukijiziba na ‘sunscreen’ muda wote unakosa faida hizi.”

Kwa nini miale ya jua ni muhimu

Mtaalamu wa afya ya ngozi Dk Donard Mshiu amesema miale ya jua hasa la asubuhi na jioni ina umuhimu mkubwa katika ngozi ya binadamu.

“Mwanga wa jua ni chanzo kikuu cha vitamini D, hivyo ngozi inapopigwa na miale ya jua, hasa ile ya asubuhi, huzalisha vitamini D kupitia mchakato wa kimaumbile unaohusiana na kolesteroli,” amesema na kuongeza:

“Vitamini D ni mhimili wa mifupa imara kwa sababu husaidia kufyonza madini ya kalsiamu na fosforasi. Bila mwanga wa jua wa kutosha, watu hupatwa na magonjwa kama vile udhaifu wa mifupa (osteoporosis) na hata kasoro za ukuaji wa mifupa kwa watoto.”

Amesema mwanga wa jua huchangia pia katika kuboresha mzunguko wa damu na kusisimua mfumo wa kinga ya mwili huku tafiri za kisayansi kionyesha kuwa kuwa jua linapopiga ngozi, huzalisha kemikali zinazoongeza mzunguko wa damu na kusaidia mwili kupambana na maradhi mbalimbali.

“Mwanga wa jua husaidia pia katika afya ya akili. Ngozi inapopata mwanga, mwili huchochea utolewaji wa homoni ya ‘serotonin’ ambayo huchangia mtu kuwa na furaha na kupunguza mfadhaiko.

Watu wanaokaa muda mrefu bila kupata mwanga wa jua mara nyingi hukumbwa na huzuni, uchovu na hata msongo wa mawazo. Hii ndiyo sababu hata wagonjwa wa msongo wa mawazo huwa wanashauriwa kuota jua la asubuhi.

Hata hivyo, mtaalamu huyo ametahadharisha kuwa licha ya umuhimu huo, jua linapokuwa kali sana linaweza kusababisha uharibifu wa ngozi.

Amesema ni vyema kupata mwanga wa jua kwa kiasi kinachofaa na hasa nyakati salama kama asubuhi kabla ya saa nne na jioni baada ya saa kumi.