“NITAKWENDA.”
“Basi nitakuja twende sote.”
“Sawa. Nitakusubiri.”
Saa nane mchana Raisa akaja nyumbani. Nikakaa naye hadi saa tisa tulipoondoka kwenda Hospitali ya Bombo iliyoko eneo la Raskazoni pembezoni mwa Bahari ya Hindi.
Ukiwa hospitalini hapo unaweza kuiona bahari na bandari ya Tanga. Tulipofika hospitalini hapo, muda wa kutazama wagonjwa ulikuwa umewadia. Tukaingia ndani na kufika katika wodi aliyokuwa amelazwa mama.
Mama yangu alikuwa akiendelea vizuri na alifurahi alipoona nimefika nikiwa na rafiki yangu Raisa ambaye alikuwa akimfahamu tangu tulipokuwa tunasoma shule ya sekondari.
Tulizungumza naye kwa karibu saa nzima kabla ya muda wa kutazama wagonjwa kumalizika. Tukaagana naye na kuondoka.
Tulipanda daladala ambayo ilitufikisha eneo la stendi ambapo niliagana na Raisa. Yeye alipanda daladala nyingine inayoelekea mitaa kwao. Alikuwa akiishi eneo la Kwaminchi.
Kama saa kumi na mbili jioni hivi ndipo nilifika nyumbani. Nilipofika tu nikampigia simu Raisa. Tukapiga stori hadi salio langu likaisha, tukaagana.
Siku iliyofuata mama alitolewa hospitali baada ya afya yake kuwa nzuri. Aliporudi nyumbani tulikunywa naye chai kisha nikampigia Raisa kumjulisha kuwa mama yangu alikuwa ametoka hospitali. Akanieleza kuwa angekuja jioni kumjulia hali.
Jioni yake Raisa akaja nyumbani, tukazungumza hadi saa kumi na mbili jioni, akaenda zake.
Baada ya kupita siku tatu na mimi nikaenda kwao. Nilienda asubuhi, nikashinda huko hadi jioni niliporudi nyumbani.
Mwishoni mwa wiki ile Sufiani akanipigia simu. Nilipopokea simu yake aliniambia:
“Nipo Tanga.”
“Umekuja lini?” nikamuuliza.
“Nimeingia leo alfajiri.”
Kitu cha kwanza kukikumbuka ni ile ahadi yetu ya kuniletea zawadi.
“Umeniletea zawadi yangu?” nikamuuliza.
“Ndiyo maana nimekupigia simu. Sijui tutakutana wapi?”
Moyo wangu ukafarijika. Nikamuuliza haraka:
“Niambie wewe tutakutane wapi?”
“Kwani wewe unaishi wapi?”
“Mimi naishi Sahare.”
Sufiani akawa kimya kwa muda kisha sauti yake ikasikika tena:
“Nilikuwa nafikiria tukutane wapi ili nisikusumbue.”
“Kwani wewe sasa hivi uko wapi?”
“Niko nyumbani kwangu Chumbageni. Lakini saa sita tutakuwa tumeegesha lori katika mkahawa mmoja pale Gofu tukipata chakula. Baada ya hapo tunaelekea Mombasa nchini Kenya. Tuna mzigo unaokwenda Mombasa.”
“Huo mkahawa unaitwaje?”
“Ni pale Saba Saba. Ukifika tu utaliona lori letu.”
“Sawa basi nitafika.”
“Unaweza kuchukua bodaboda. Nitailipia mimi.”
“Sawa. Nitafika na bodaboda.”
Dakika chache kabla ya saa sita mchana bodaboda ikanishusha Gofu nyuma ya lori analoendesha Sufiani. Mwenyewe nilikutana naye kwenye mkahawa, tukazungumza sana. Mwisho akanipa kiboksi kilichokuwa na simu mpya ambayo aliniambia ni zawadi aliyoninunulia.
Mwisho wa mazungumzo yetu tukaagana na kuondoka.
Baada ya kutokeza barabarani niliangalia nyuma kulitazama lori la Sufiani ambalo bado lilikuwa limesimama, kisha nikaendelea na safari kuelekea upande wa Kwaminchi alikokuwa akiishi rafiki yangu Raisa.
Nilipofika katika kituo cha bodaboda nikabadili mawazo ya kwenda kwa Raisa. Nikapanda bodaboda iliyonirudisha nyumbani Sahare.
Nilipofika nyumbani niliingia chumbani mwangu nikakitoa kile kiboksi cha simu, nikakifungua na kuitoa simu iliyokuwamo ndani. Nikaitazama-tazama kuona jinsi ilivyokuwa nzuri na ya kifahari.
Wakati ninaitazama nilikuwa ninatabasamu peke yangu kwa furaha. Niliifungua nikaitazama kwa ndani. Niliporidhika nayo niliifunga tena, nikaichaji kwa saa sita.
Baada ya muda huo nilitoa laini yangu iliyokuwa katika simu nyingine, nikaitia katika simu mpya kisha nikaiwasha.
Niseme ukweli kuwa sikuwahi kumiliki simu nzuri kama ile maishani mwangu.
Niliijaribu kwa kuanza kumpigia Raisa. Raisa alipopokea simu, nilipiga naye stori kwa karibu dakika tano. Baada ya Raisa niliwapigia marafiki zangu wawili watatu kisha nikaagana nao. Katika marafiki zangu hao hakukuwa na yeyote aliyegundua kuwa nilikuwa najaribu simu yangu mpya niliyozawadiwa na Sufiani, dereva wa malori ambaye nilijuana naye siku chache zilizopita.
Siku zikapita ila Sufiani hakuondoka kichwani mwangu. Nilikuwa nikimuwaza wakati wote. Baada ya wiki moja hivi Sufiani akanipigia simu. Ilikuwa ni usiku, nikijiandaa kulala.
Nilipoona namba yake nikaipokea simu haraka.
“Vipi Sufiani, uko Tanga au Mombasa?” nikamuuliza.
“Mombasa nilisharudi tangu juzi, niko Tanga na kesho asubuhi naondoka kwenda Dar,” Sufiani akaniambia kwenye simu.
“Hivi tangu juzi uko hapa Tanga?”
“Niko Tanga. Nilikuwa na pilikapilika ndio maana hatukuwasiliana.”
“Pilikapilika za nini?” nikamuuliza.
“Ah, ni mambo ya familia tu.”
“Ukiondoka kesho unarudi lini tena?”
“Sina hakika lakini tutakuwa tunawasiliana.”
“Sawa. Nashukuru kwa kunikumbuka na nakutakia safari njema hapo kesho.”
“Asante. Usiku mwema.”
“Na kwako.”
Waswahili wana msemo kwamba panapofuka moshi panaficha moto. Hatimaye moto ulijitokeza. Kumbe Sufiani alikuwa ni mbovu kwangu tangu siku ile aliponipa lifti kuja Tanga. Siku zote alikuwa akitafuta namna ya kusuhubiana na mimi.
Lakini hakuwa akijua kuwa alikuwa ameshanitia mkononi kutokana na zawadi alizokuwa akinizawadia. Baada ya ile simu alinipa zawadi nyingi ikiwemo pesa.
Yeye hakutaka longolongo, alijiingiza moja kwa moja kwa kuniambia kuwa ninafaa kuwa mke wake.
Na mimi sikuficha hisia zangu, nikamwambia hata yeye anafaa kuwa mume wangu kwa sababu nilikuwa nimeshampenda kutokana na tabia yake ya ukarimu.
Niseme ukweli kuwa yule mwanaume sikuwahi kutembea naye hata siku moja. Ni upumbavu wangu tu, nilikuja kuyaharibu na Mungu akaniangaza. Halafu mashoga si watu wazuri.
Siku ile nilipomkubalia Sufiani niwe mke wake, siku ya pili yake akaleta barua ya posa nyumbani kwetu. Aliwatuma wazee watatu maarufu walioleta barua. Kwa vile nilishampa mama ujumbe kuhusu watu hao, walipofika wakakaribishwa vizuri.
Barua ilifunguliwa na baba na kusomwa hapo hapo.
Katika majibu yake, baba aliwambia kuwa ameipokea barua kwa mikono miwili na ataitolea majibu baada ya wiki moja.
Wageni walipoondoka baba alimuita mama kisha aliniita mimi akaniuliza kama nilikuwa namfahamu Sufiani.
“Namfahamu,” nikamjibu.
“Anafanya kazi gani?”
“Ni dereva wa malori, anakwenda Rwanda, Burundi, Zambia na nchi nyingine.”
“Nimekuuliza kazi yake tu mwanangu, sikutaka kujua anakwenda wapi,” baba akanitayariza.
“Si nakueleza tu baba!”
“Haya tumeshasikia. Kwa hiyo kabla ya kuleta hii barua mlishazungumza kuhusu hili suala?”
“Ndiyo, tulilizungumza.”
“Akakwambia kuwa anataka kukuoa?”
“Ndiyo.”
“Huyu mtu hana mke?”
“Hana mke.”
“Na umejuana naye kwa muda gani sasa?”
Hapo nikasema uongo:
“Kama mwaka mmoja hivi.”
“Umeridhika na tabia zake?”
“Tabia zake ni nzuri.”
“Na umempenda?”
“Yaani mpaka nimemruhusu alete barua ni kuwa nimempenda.”
“Sawa.”
Baba akamtazama mama.
“Mamake, umemsikia mwanao?” baba akamuuliza mama.
“Nimemsikia.”
“Unasemaje, tuipokee hii posa?”
“Tuipokee. Kama wenyewe wamependana, tuwaozeshe tu.”
“Sawa.”
Baada ya wiki moja wale wazee waliotumwa na Sufiani walifuata majibu, wakaambiwa posa imekubaliwa.
Baba aliwatajia wazee hao kilichokuwa kinatakiwa ikiwa ni pamoja na mali na mahari yangu.
Siku ya pili yake tu Sufiani akaleta kiasi alichotakiwa kukitoa. Baada ya hapo ndipo mipango ya harusi yangu ilipofanywa.
Namshukuru sana shoga yangu Raisa kwa kusimama kidete siku ya harusi yangu na kuhakikisha harusi inafana. Nikaolewa na Sufiani.
Sufiani alinipangishia nyumba nyingine katikati ya mji. Ilikuwa ni hizi nyumba za Msajili wa Majumba. Ilikuwa ya ghorofa moja na iligawanywa sehemu nne. Chini kulikuwa na sehemu mbili na juu kulikuwa na sehemu mbili. Kwa jumla tulikuwa wapangaji wanne tuliochangia nyumba hiyo kila mmoja akiwa na upande wake.
Siku ile nilipoolewa ndipo tulianza maisha katika nyumba hiyo.
Ili nisikae bure nyumbani, Sufiani alinifungulia saluni maeneo ya mjini ambayo zamani yalifahamika kwa jina la Uzunguni.
Asubuhi huwa nakwenda zangu saluni ambapo ninarudi usiku. Baada ya kuboresha saluni yangu, niliajiri wafanyakazi wanne. Kwa vile nilikuwa na wafanyakazi, nilikuwa naweza kuondoka na kuwaacha wakiendelea na kazi.
Mara nyingi siku mume wangu akiwa nyumbani na mimi hubaki nyumbani. Siku akisafiri ndiyo hushinda kazini kwangu.
Niliendesha saluni yangu kwa miezi sita nikapata kiasi fulani cha pesa. Nikamuomba Sufiani aniongezee pesa zingine ili ninunue gari. Nilikuwa natamani sana kumiliki gari.
Sufiani akaniambia nisubiri. Nikasubiri. Baada ya miezi miwili akaniuliza nilitaka aniongezee kiasi gani. Nikamtajia kiasi nilichokuwa nahitaji, Sufiani akaniongezea. Nikaenda naye Dar kununua gari.
Nilikuwa nimejifunza kuendesha gari tangu nilipokuwa VETA lakini sikuwa na gari la kuendesha.
Baada ya kupata lile gari nikakata leseni na kuanza kuliendesha. Lilinisaidia sana katika nyendo zangu kama vile kwenda sokoni, madukani, kazini kwangu na sehemu zingine.
Hata yeye Sufiani alikuwa akilitumia kwa shughuli zake. Aliwahi kwenda nalo Dar mara kadhaa. Hata hivyo Sufiani ndiye aliyekuwa akilitia mafuta na kulifanyia matengenezo kila ilipohitajika.
Maisha yetu na Sufiani yalikuwa mazuri sana.