Baresi awaonya mastaa Kagame Cup 2025

WAKATI bingwa wa Ligi Kuu Zanzibar, Mlandege akiwa na kibarua kizito kesho Jumamosi cha kucheza dhidi ya APR ya Rwanda katika michuano ya Kagame, kocha wa kikosi hicho, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ amewataka wachezaji kutofanya makosa kama ilivyokuwa dhidi ya KMC.

Baresi alisema mechi ya kwanza dhidi ya KMC waliyopoteza kwa mabao 3-2 imetoa somo kwa wachezaji wa kikosi hicho akiwataka kusahau haraka yaliyopita na kuelekeza nguvu dhidi ya APR.

“APR si timu ya mchezo mchezo, wana kikosi kilicho na nidhamu kubwa ya kiufundi na wachezaji wenye uzoefu wa mashindano makubwa. Tunapaswa kuwa bora zaidi kuliko tulivyokuwa dhidi ya KMC, makosa ya kizembe yakitokea tena yatatugharimu,”€  alisema Bares.

Kocha huyo alisema kuwa tatizo kubwa lililowasumbua dhidi ya KMC lilikuwa ni udhaifu wa safu ya ulinzi ambao mara kadhaa uliteleza na kutoa mianya kwa wapinzani, pia washambuliaji walishindwa kutumia nafasi ambazo walitengeneza hasa katika kipindi cha kwanza.

“Niliona mabeki wangu wakikosa mawasiliano, jambo hilo tumejitahidi kufanyia kazi, hivyo tunaweza kuona mabadiliko, hizi mechi zinatujenga kuhakikisha tunafanya vizuri kimataifa,” aliongeza.

Mlandege inatarajiwa kuingia uwanjani ikiwa na matumaini makubwa kwa mastaa wao wapya akiwamo Davi Nascimento na Vitor de Souza ambao ni raia wa Brazil na Enzo Claude kutoka Ufaransa. 

Kocha huyo alisema mashabiki wa Zanzibar bado wanaamini kikosi hicho kinaweza kufanya kitu kikubwa na jukumu la kurejesha imani hiyo liko mikononi mwa wachezaji wake.

“Mashabiki wetu hawajakata tamaa, wanataka kuona mapambano. Hili si jambo rahisi lakini naamini vijana wangu wakijituma, tunaweza kuishangaza APR,” alisema.

APR ambayo itakutana na Mlandege ni wanafainali wa msimu uliopita wa michuano hiyo wakipoteza kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Red Arrows ya Zambia baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Mbali na kuwa wanafainali wa msimu uliopita ni mabingwa mara tatu wa michuano hiyo, wakitwaa mwaka 2004, 2007 na 2010.

Mafanikio makubwa kwa Mlendege katika Kombe la Kagame ni ile ya mwaka 1998 ilipofika fainali na kupoteza kwa mabao 2-1 mbele ya Rayon Sports ya Rwanda, michuno ikifanyikia Zanzibar.

Kabla ya Mlandege kucheza dhidi ya APR, mechi ya mapema itakuwa kati ya Bumamuru dhidi ya KMC. Bumamuru ilianza mashindano hayo kwa kuchapwa kwenye mechi yake ya kwanza dhidi ya APR kwa mabao 2-0 huku KMC yenyewe ikianza kwa kuifunga Mlandege.