Dk Mwinyi awapa jukumu viongozi wa dini ulinzi wa amani

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amewataka viongozi wa dini kutumia majukwaa yao kupaza sauti na kuwakumbusha wanasiasa kuwa katika kipindi cha kampeni ni muhimu kuepuka siasa za chuki, mifarakano, ubaguzi na matusi.

Amesema badala ya kueneza maneno ya uchochezi, wanasiasa wanapaswa kueleza kwa uwazi mipango na sera zao kuhusu namna watakavyowahudumia wananchi, ili kusaidia kulinda amani, mshikamano na utulivu wa nchi.

Pia, amesema jukumu la kulinda amani ya nchi si la wanasiasa pekee, bali ni la kila mmoja, wakiwemo viongozi wa dini, waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.

Ametoa wito kwa makundi hayo kujiepusha na kauli au vitendo vyovyote vinavyoweza kuashiria au kusababisha uvunjifu wa amani, hususan katika kipindi hiki cha kampeni.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo, Septemba 5, 2025, wakati akihutubia katika kongamano la Baraza la Maulid Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Polisi Ziwani.

Amesema tayari baadhi ya wanasiasa wameanza kutoa matamshi yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi, hivyo ni wajibu wa viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kukemea kauli hizo mapema kabla hazijasababisha madhara makubwa.

 “Sio vyema kunyamaza katika hili kwani kuvunjika kwa amani hakuanzi na bunduki bali kunaanza na viashiria ikiwemo maneno na kauli za vitisho kutoka miongoni mwetu, tuendelee kufanya hivyo ili wale wanaohimizwa kutoka kwenda kuvunja amani wasikubali kufanya hivyo,” amesema Dk Mwinyi. 

Dk Mwinyi amesema ni wajibu wa kila mmoja kuwa mstari wa mbele kuilinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi kujiepusha na kila kitakachovunja amani iliyopo ili kudumu katika neema hiyo adhimu.

Hata hivyo, amebainisha kuwa taifa lolote duniani haliwezi kuwa salama wala kuendelea bila ya kuwa na amani na hiyo inaonesha wazi kuwa amani ndio moyo wa kila mafanikio ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.

Akizungumzia mada zilizowasilishwa katika kongamano hilo ikiwemo ya viashiria vya uvunjifu wa amani amesema zinaendana na wakati uliopo wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.

“Nimefarijika kuona wengi wetu tunazugumza kauli moja ya kuhimiza amani katika Taifa, hatua ambayo ni dalili ya kila mmoja wetu kutambua umuhimu wa kuienzi na kuidumisha neema hii ambayo ndio msingi mkubwa wa mafanikio,” amesisitiza.

Hivyo, amewaomba wananchi kwa umoja wao kujitahidi kuilinda amani yao kwa nguvu zote bila ya kuchoka kwani kufanya hivyo itakuwa wameihamisha neema hiyo aliyowaruzuku Mola wao mlezi na kuitunza kwake ni namna ya kumshukuru Mungu.

“Tuzingatie kuwa tupo katika maadhimisho ya kuzaliwa Mtume (SAW) tuendelee kuonesha mapenzi yetu kwake kwa kufuata mwenendo wake hasa wa kudumisha amani jambo ambalo alituhimiza sana sisi wafuasi wake,” alisisitiza.

Rais Mwinyi alilipongeza Baraza la Maulid kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti kuandaa kongamano hilo ambalo linahimiza amani, umoja na mshikamano.

Awali, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Zanzibar, Shekh Khalid Ali Mfaume, amesema maadhimisho ya kuzaliwa Mtume ni lazima kuyaingiza katika maisha yao ya kila siku kwani kutofanya hivyo ni kwenda kinyume na amri yake na mafundisho mema.

Amewasisitiza vijana kuacha kutumika vibaya kuvuruga amani ili kuhakikisha nchi inaendelea kubaki na tunu hiyo.

“Kila chama kinahitaji dola ni lazima kumwaga sera na sio chuki na mifarakano ambayo itapelekea kupotea kwa amani yetu,” amesema.

Awali, akitoa salamu Mwenyekiti wa Baraza la Maulid Zanzibar, Abubakar Mohammed Mussa, amesema shughuli hiyo sio ya kujenga kiimani tu bali pia  imelenga kuendeleza utamaduni wao wa Kiislam na kijamii katika uzazi wa Mtume Muhammad (SAW)..

Alimpongeza Dk Mwinyi kwa kushirikiana nao kwani uwepo wake unatoa moyo kwa Wanzanzibar na ishara ya dhati ya Serikali kuu kuunga mkono kazi hiyo.

Katika kongamano hilo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo amani yetu ni neema kutoka kwa Allah tusiichezee na viashiria vya uvunjifu wa amani.