Kinshasa. Mamlaka za afya za Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimetangaza mlipuo mpya wa ugonjwa wa Ebola, ambapo hadi sasa umeua watu 16, wakiwepo wahudumu wanne wa afya.
Pia zimeeleza kuwa hadi sasa watu 28 wameripotiwa kuambukizwa ugonjwa huo na baadhi yao wanaendelea na matibabu.
Maeneo yaliyoathirika zaidi na mlipoko wa ugonjwa huo yanatajwa kuwa ni Bulape na Mweka.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo mgonjwa wa kwanza kuripotiwa safari hii ni mjamzito mwenye umri wa miaka 34, aliyeanza kuonesha dalili za ugonjwa Agosti 20, 2025 na kufariki dunia siku tano baadaye.
Sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa baadhi ya wagonjwa na kupimwa na Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Baiolojia, zimethibitisha kuwa na virusi aina ya Ebola Zaire.
Tayari hadi sasa timu ya kukabiliana na majanga nchini humo kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) zimechukua hatua za dharura kwa kupeleka wataalamu wa afya kwa ajili ya kuimarisha haraka ufuatiliaji, matibabu na udhibiti wa maambukizi katika vituo vya afya.
Wataalamu wengine wamesambazwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa huo na namna sahihi ya kujikinga.
Aidha, WHO imetoa tani mbili za vifaa vya dharura, ikiwemo vifaa vya kujikinga (PPE) na vya maabara vinavyohamishika pamoja na dawa.
Taarifa hiyo pia imeeleza nchi hiyo tayari ina akiba ya dawa na dozi 2,000 za chanjo ya Ervebo Ebola, iliyothibitika kuwa na ufanisi dhidi ya aina hiyo ya Ebola.