Ericsson, Siemens kuongeza uwekezaji kwenye mtandao na nishati nchini

Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi amefanya ziara katika  makao makuu ya kampuni za Ericsson na Siemens Energy za Sweden kujadiliana kuhusu kuongeza uwekezaji na kuendelea kuleta teknolojia zao nchini.

Balozi Matinyi aliitembelea kampuni ya Ericsson Septemba 2, 2025, jijini Stockholm na kuzungumza na viongozi na wataalamu wao, wakiongozwa na Ola Bergstorm, mkurugenzi wa sera za serikali na uhamasishaji,.

Siku iliyofuata (Septemba 03) Matinyi alizitembelea ofisi za Siemens Energy mjini Finspang na kupokewa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Gunnar Wik, akiwa na timu yake ya menejimenti na wataalamu.

Kampuni ya Ericsson ilieleza na kuonyesha kwa vitendo mapinduzi ya teknolojia ya mtandao wa intaneti wa 5G unavyotumika kwa pamoja na akili unde (AI) kutoa huduma za kitaalamu kwenye sekta mbalimbali.

Mhandisi wa Ericsson Jon Gamble alisema nchini Sweden wanatumia teknolojia hiyo kwenye huduma za magari ya wagonjwa, zimamoto na polisi, na pia kwenye kilimo, elimu, afya na uendeshaji wa miundombinu ya reli, bandari, viwanja vya ndege, usafirishaji umeme na uchimbaji madini.

Ericsson pia ilieleza utayari wake kuisambaza tekinolojia ya 5G nchini kote ambako mtandao huo haujafika kwa kushirikiana na kampuni za simu Tanzania.

Nayo kampuni ya Siemens Energy ilionyesha teknolojia yake kutengeneza mitambo ya kufua umeme kwa kutumia gesi ambayo pia inatumika nchini katika kituo cha kufua umeme cha Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Kampuni ya Siemens imesema inataka kuendelea kushirikiana na Tanzania katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi katika miradi ya kimkakati ya Kinyerezi, Mkuranga, Somanga, Dodoma na Mtwara.

Sambamba na ziara hiyo, Matinyi pia alizungumza na wataalam 12 wa Tanesco waliopo Siemens kupata mafunzo maalumu ya uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme kwa njia ya gesi kuanzia Agosti 24 hadi  Septemba 13, 2025.

Aliwataka wataalam hao kujifunza kwa bidii teknolojia hiyo kwani taifa linawategemea wao tu katika kujihakikishia usalama wa nishati.

Ziara hizo mbili ni kielelezo cha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Sweden, hususan katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.