Russia. Pingili za mgongo ni mifupa muhimu katika usaidizi wa muundo na shughuli za mwili.
Huunda safu ambayo hutumika kama mhimili wa kati wa mwili na kutoa usaidizi kwenye kichwa, shingo na kiwiliwili.
Mpangilio wake huruhusu kupinda na kujipinda kupitia diski za katikati na maungio yake. Mfereji wa pingili hulinda uti wa mgongo na mishipa ya fahamu inayojichomoza katika matundu.
Pingili zimeunganishwa moja kwenda na nyingine kwa tishu ngumu za ligament idadi yake zikiwa 220 na misuli 120 ikijipachika. Pingili hizi kwa pamoja na misuli, ligament na santuri zinaunda maungio yanayofikia 100.
Ni moja ya muundo mgumu, wenye vipengele vingi vilivyounganishwa na vinavyotegemeana.
Kwa mujibu wa madaktari wa mifupa duniani asilimia 80 ya matatizo ya mgongo hayahitaji matibabu.
Matatizo ya pingili ya mara kwa mara ni pamoja na kusinyaa, kulika au kumomonyoka, kuteguka, kuvunjika, kukosa udhibiti baada ya ligamenti kukwanyuka na kuhama kwa diski.
Wakati tunapozaliwa, mgongo huwa na pingili aina 33 kutoka katika aina tano za pingili. Tunapozeeka pingili za ‘sacral’ na za ‘coccygeal’ huungana.
Zipo pingili 12 katika eneo la kifuani kwa nyuma, pingiri tano katika eneo la nyuma ya tumbo na eneo la shingo linajumuisha pingiri saba.
Jambo la kushangaza ni kwamba wanadamu wana idadi sawa ya pingili saba za shingo kama twiga, ingawa za twiga ni kubwa zaidi.
Uti wa mgongo unagandana siku nzima, na kukufanya uwe mfupi kidogo jioni, hali hii inabadilika nyakati za usiku tunapopumzika.
Kwa kawaida unakuwa na urefu wa sentimeta 1-2 asubuhi kuliko mwisho wa siku. Hii ni kwa sababu diski za uti wa mgongo hunyonya maji na kujaa usiku kucha, hali hii hupungua kutokana na shinikizo wakati wa mchana.
Kuzeeka na kuzorota, uharibifu wa pingili za uti wa mgongo unaohusiana na umri. Ni kawaida watu wengi kuonyesha dalili za kudhofika kwa pingili na santuri bila maumivu yoyote.
Diski za uti wa mgongo ni sponji na hutoa uegemeo kwa pingili huku ikiwa ni mnyonyaji wa shinikizo. Lakini hazina mtawanyiko mzuri wa damu hivyo kufanya afya zao kutegemea mambo ya nje.
Ili kudumisha uti wa mgongo wenye afya, simama na ujinyooshe kila baada ya dakika 30 ili kupunguza shinikizo kwenye uti wa mgongo wako na kuboresha mzunguko wa damu.
Fanya mazoezi ya kawaida yasiyo na madhara kama vile kutembea, kukimbia na kuogelea ili kuimarisha misuli ya msingi, kuboresha kunyumbulika na kufanya mazoezi ya mkao mzuri.
Dhibiti uzito, pata usingizi mzuri wenye godoro la ugumu wa wastani, na kula lishe bora iliyo na omega-3s, madini na vitamini C kwa wingi na epuka msongo wa akili. Fika mapema katika huduma za afya unapopata maumivu ya mgongo.