KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge amesema mechi ya kesho dhidi ya Mbeya City itatoa picha ya ushindani kwa ajili ya Ligi Kuu Bara inayoanza Septemba 17, huku akiweka wazi utakuwa mchezo mzuri kutokana na utayari wa wachezaji wa kikosi hicho.
Azam itashuka uwanjani kesho katika pambano la kirafiki la kusindikiza tamasha la Mbeya City Day linalofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya ambalo wenyeji waliorejea katika Ligi Kuu baada ya kuikosa misimu miwili iliyopita watatambulisha jezi na kikosi kipya cha timu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge alisema ni anaamini mechi hiyo ya kesho ni sehemu ya maandalizi na watapata changamoto ya ushindani huku akiamini kuwa kupata mchezo huo na moja ya timu zinazoshiriki ligi kutampa mwanga wa wapi anatakiwa kuboresha kabla ya msimu kuanza.
“Tumemaliza kambi yetu ya maandalizi ya msimu wachezaji wangu wapo fiti na mechi zote tulizocheza zimenipa picha kamili ya kikosi nilichonacho na Jumamosi nitapata mwanga kamili kwani ndio utakuwa mchezo wa mwisho wa kirafiki kabla ya kuanza ushindani,” alisema Ibenge na kuongeza;
“Tumepata bahati ya kucheza mechi nyingi za kirafiki nimeona upunguvu na kuufanyia kazi na naamini kukosea na kupatia kumeonekana hii inanipa nafasi ya kufanyia kazi zaidi upungufu kuliko ubora Jumamosi nitapata picha kamili ya utayari wa wachezaji wangu.”
Ibenge alisema kila mchezo kwake ni bora na amekuwa akiupa nafasi ya kuisoma timu bila kujali anakutana na timu ya aina gani, anaamini Mbeya City itawapa kipimo kizuri zaidi kabla ya kuanza mechi za mashindano.
“Wachezaji wangu wanafahamu umuhimu wa mchezo huo na watatakiwa kuonyesha ni kwa namna gani walikuwa wanafanyia kazi mbinu na maandalizi tuliyoyafanya katika kambi mbili tofauti tukipata nafasi ya kucheza mechi za kirafiki,” alisema na kuongeza;
“Kwa ujumla matarajio yangu ni makubwa kutokana na namna wachezaji wangu wamekuwa wakifanyia kazi maelekezo ambayo nimekuwa nikiwapa, tunakutana na timu ambayo inarudi Ligi Kuu baada ya kufanya makosa kwa kushuka daraja hivyo hatutarajii mchezo rahisi.”
Alisema anaamini anaenda kukutana na timu yenye utimamu mzuri wa mwili kutokana na kutoka kucheza ligi ya daraja la chini na sasa wamepanga kucheza ligi ya ushindani hivyo utakuwa mchezo wenye picha bora na kipimo sahihi kwa kila mmoja.
Azam inajiandaa na mechi za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa kuvaana na El Merrikh Bentiu ya Sudan Kusini na ikivuka hapo itakutana na mshindi wa mechi kati ya KMKM na AS Port ya Djibouti.