KUFUATIA kuwepo kwa idadi ndogo ya kesi zinazohusu wanawake katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCPHR), Mahakama hiyo imelazimika kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kuboresha uelewa wao kuhusu taratibu za Mahakama na nafasi ya wanawake na wasichana katika kupata Haki.
Kwa mujibu wa Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Grace Kakai kongamano hilo limekutanisha wadau mbalimbali ikiwemo watendaji wa serikali, wanasheria kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wataalamu wa sheria.
Akizungumza Jana Septemba 3, 2025 mahakamani hapo ikiwa ni siku ya kwanza ya kongamano hilo, Grace amesema lengo kuu la kongamano hilo ni kuhakikisha wanawake na wasichana wanajumuishwa ipasavyo katika kazi za mahakama ili kuimarisha upatikanaji wa haki zao.
“Mahakama imebaini kupitia rekodi zake tangu kuanzishwa kwake idadi ya kesi zinazohusu haki za wanawake na wasichana ni ndogo hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na wadau pamoja na wataalamu wa sheria kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu taratibu za uendeshaji wa mahakama hiyo,”Amesema.
Amesema wakati wa ufunguzi wa shughuli za Mahakama mwezi April mwaka huu, kulifanyika semina iliyokuwa na kaulimbiu ya “Tengeneza haki kupitia fidia”, ambapo mojawapo ya mapendekezo yaliyotolewa ni kuwapa wadau elimu ya kina kuhusu taratibu za mahakama ili kuchochea uwasilishaji wa kesi zaidi zinazohusu haki za wanawake na wasichana.
Meneja wa Programu ya Ushawishi katika Kituo cha Utafiti wa Ukatili na Upatanisho Mary Izobo amesema kongamano hilo ni hatua muhimu kwa sababu linatoa nafasi kwa wanawake kushirikiana moja kwa moja na mahakama.
Amessema wanawake wengi hukumbana na vikwazo vya kimfumo wanapojaribu kufuata haki zao, ikiwa ni pamoja na unyanyapaa, ukosefu wa uelewa wa haki zao, gharama kubwa za kifedha na urasimu wa taratibu za mahakama.
“Ni muhimu kuhakikisha hali halisi zinazowakumba wanawake na wasichana zinafikishwa kwenye mijadala ya kikanda na bara zima, sambamba na kuwepo kwa taratibu zinazozingatia manusura ili kufanikisha upatikanaji wa haki endelevu,” Amesema Izobo.
Aidha alisema wanawake kupata haki siyo upendeleo bali ni haki ya msingi ambayo kila mtu anatakiwa kuhakikisha inatekelezwa kikamilifu.
“kituo chetu kimeingia makubaliano ya ushirikiano na Mahakama ya Afrika (MOU) kwa lengo la kuimarisha ushawishi na kufanya tafiti zitakazosaidia wanawake hasa walioko vijijini na maeneo yaliyosahaulika kupata uelewa wa haki zao na taratibu za mahakama,” amesema.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Haki za Binadamu na Maendeleo Afrika, Michael Nyarko amesema upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana ni jambo la msingi na ndiyo sababu taasisi yake imeshiriki kikamilifu katika kongamano hilo.
“ Bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto kubwa za ukiukwaji wa haki za wanawake na wasichana ikiwemo ubaguzi, ukatili wa kijinsia, ukosefu wa ushiriki wa kisiasa, pamoja na vikwazo katika upatikanaji wa fursa za kijamii na kiuchumi, ikiwemo haki za uzazi, “amesema Nyarko na kuongeza
“Haki hizo zimetambuliwa katika nyaraka mbalimbali za kimataifa na kikanda, zikiwemo zile zilizopitishwa na Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na hata Umoja wa Ulaya ambazo nchi za Afrika zimezitia saini, changamoto kubwa imekuwa ni utekelezaji na uwajibikaji,”.
Amesema dhima kuu ya mifumo ya haki za binadamu ya Afrika ni kuhakikisha kuna uwajibikaji na kutoa mwongozo kwa nchi wanachama ili ziweze kutekeleza wajibu wao ipasavyo chini ya mikataba hiyo.