Jela miaka 20 kwa kukata nyaya za Tanesco, kulipa Sh273 milioni.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu wafanyabiashara wawili, Ally Kibope (25 ) na Athuman Omary (40) kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kuingilia Miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kulisababishia hasara shirika hilo ya Sh273 milioni.

Mbali na adhabu hiyo, mahakama hiyo imeamuru washtakiwa hao kulipa hasara waliyoisababishia Tanesco ambayo ni Sh273 milioni.

Kibope, mkazi wa Keko Mwanga na Omary ambaye ni mkazi wa Ilala Bungoni, wanadaiwa kukata nyaya za umeme zilizotandazwa ardhi, jambo lililopelekea shirika hilo kupata hasara ya Sh273 milioni.

Hukumu hiyo imetolewa jana Alhamisi, Septemba 4, 2025, na Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi, ambaye alisema mahakama hiyo imewatia hatiani kwa makosa mawili ambayo ni kuingilia miundombinu ya Tanesco na kusababisha hasara.

Hakimu Mushi alisema wametiwa hatiani baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi tisa na vielelezo vitano, vilivyotolewa Mahakama hapo na upande wa mashtaka.

“Mahakama imewatia hatiani kama walivyoshtakiwa washtakiwa wote baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi,” alisema Hakimu Mushi.

Awali, kabla ya kupewa adhabu, washitakiwa hao waliiomba mahakama isiwape adhabu kali kulingana na muda waliokaa mahabusu na waliomba wahukumiwe kifungo cha nje.

Hata hivyo, upande wa mashtaka, kupitia Wakili wa Serikali Tumaini Mafuru, waliiomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya washtakiwa hao ili iwe fundisho kwa sababu Serikali inatumia fedha nyingi kupeleka huduma kwa wananchi na wao wanaharibu miundombinu hiyo.

“Kitendo cha uharibifu wa miundombinu ya Tanesco kilichofanywa na washtakiwa hakikubaliki na wanapaswa kupewa adhabu kali ili iwe fundisho kwao na kwa watu wengine” alidai Wakili Mafuru.

Hakimu Mushi alitupilia mbali maombi ya washtakiwa hao na kukubaliana na maombi ya upande wa mashtaka.

Akitoa hukumu, Hakimu Mushi alisema kwa kosa la kuingilia miundombinu, watatumikia kifungo cha miaka 15 gerezani na kosa la kusababisha hasara watatumikia kifungo cha miaka 20 gerezani.

Alisema adhabu hizo zitakwenda pamoja, hivyo watatumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja.

” Mahakama inawahukumu kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya kuingilia miundombinu na haki ya kukata rufaa ipo wazi iwapo hamjaridhika ya uamuzi uliotolewa” alisema Hakimu Mushi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Kibope na Omary, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 49 ya mwaka 2022.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa Julai 7, 2022 eneo la Banda la Ngozi, Chang’ombe jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu waliingilia miundombinu inayotumika kutoa huduma muhimu.

Siku hiyo, watuhumiwa hao walikata nyaya za Tanesco vipande viwili vya Milimita 400 zilizokuwa zimetandazwa chini ya ardhi, huku wakijua ni kosa kisheria.

Katika shitaka la pili , siku na eneo hilo washtakiwa hao, kwa kitendo chao cha kukata nyaya hizo, waliisababishia Tanesco hasara ya Sh273 milioni.