YANGA jana ilikuwa uwanjani kupima ubavu na timu moja ya jeshi, lakini kabla ya hapo, juzi kati ilivaana na Tabora United na kupata ushindi wa mabao 4-0, huku mmoja wa manahodha wa timu hiyo akiishuhudia akiwa nje ya uwanja, kisha akawaambia wenzake kwamba kikosi hicho kina watu.
Nahodha huyo alisema kwa jinsi timu ilivyoongezwa na inavyocheza ni wazi makombe yataendelea kujazwa kwenye kabati la klabu hiyo kama ilivyofanya msimu uliopita ilipotwaa mataji matano kwa mpigo, yakiwamo Ngao ya Jamii, Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho (FA) na Kombe la Muungano.
Dickson Job ambaye kwa sasa yupo na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars jijini Brazzaville, Congo kwa ajili ya mechi ya kuwania kufuzu ushiriki wa Fainali za Kombe la Dunia 2026 akiwa na wenzake wengine watano, ndiye aliyasema hayo alipozungumza na Mwanaspoti na kusema Yanga ya sasa ina watu kwelikweli.
Job na wenzake, Ibrahim Bacca, Mudathir Yahya, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Edmund John na Clement Mzize bado hawajafanya mazoezi chini ya kocha mpya, Romain Folz lakini timu hiyo ilipocheza dhidi ya Tabora wote walikuwa nje ya uwanja wakiishuhudia mechi hiyo ya kirafiki.
Akizungumza na Mwanaspoti, nahodha msaidizi huyo wa Yanga, alisema, alikuwa nje akiutazama mchezo dhidi ya Tabora, kisha akajiridhisha bado wana timu ya kuchukua makombe zaidi.
Job alisema amefurahishwa na namna ya usajili ulivyofanyika licha ya kuondokewa na Stephanie Aziz KI, Khalid Aucho, Clatous Chama, Nickson Kibabage na Kenneth Musonda waliokuwa mastaa muhimu kikosini, lakini bado wachezaji wapya walioingia ni bora na wamempa mzuka.
“Bado sijaanza mazoezi na timu labda tukimaliza hizi mechi mbili za kuwania kushiriki fainali za Kombe la Dunia nikiwa na Stars, ndipo tutajiunga lakini ni kweli nilikuwapo katika ile mechi tukiwaangalia wenzetu wakipambana na Tabora United,” alisema Job na kuongeza;
“Nilikuwa makini sana kumfuatilia mchezaji mmoja mmoja na kusema ukweli nina amani kubwa. Unajua waliotoka ni wachezaji bora na wote tunajua hilo, lakini hawa waliokuja pia wako moto sana, naweza kusema kwa kuthibitisha kabisa timu bado ipo ya kuendelea kuchukua makombe.
“Wachezaji waliokuja wana ubora mkubwa, wataleta ushindani wa ndani, lakini wataongeza kitu wakiungana nasi waliotukuta katika timu, wananchi wenyewe watajionea tukishakuja mbele yao.
Aidha, Job ambaye ndiye aliyeiongoza Yanga kwa kucheza mechi nyingi kama nahodha kutokana na nahodha mkuu Bakari Mwamnyeto kutocheza mara kwa mara, aliongeza kuwa mbali na wachezaji wapya pia, amefurahia mbinu za kocha Folz akisema ni kitu kingine bora ambacho kimeongezeka kwenye timu yao.
“Sio tu wachezaji, kuna kocha pia, nina furaha kuona namna kocha alivyoibadili timu, kuna mambo ya kisasa zaidi ameyaongeza, kama tukishakamilika wote nadhani baada ya muda tutakuwa na timu bora zaidi.”
Yanga inajiandaa na tamasha la Kilele cha Wiki ya Mwananchi ikitarajiwa kuvaana na Bandari ya Kenya, kisha kucheza Ngao ya Jamii dhidi ya Simba kuzindua msimu wa mashindano ya ndani na baadaye kusafiri kwenda Angola kuvaana na Wiliete Banguela katika Ligi ya Mabingwa Afrika.